Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Tendaguru

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne,Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amewataka watafiti wa masuala ya Malikale kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Taasisi ya Makumbusho ya Taifa la Tanzania kushirikiana katika kufanya tafiti katika eneo la Tendaguru, mkoani Lindi yalipogundulika masalia ya Dainosaria ili kubaini endapo kuna masalia zaidi au aina nyingine ya Dainosaria.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akipokea zawadi kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt. Noel Lwoga baada ya kutembelea eneo la uhifadhi Tendaguru iliopo Mkoani Lindi

Dkt Kikwete ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ametoa agizo hilo Januari 9 alipotembelea eneo la Tendaguru kujionea kazi ya utafiti inayoendelea kufanywa na wataalamu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kushirikiana na wataalamu wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania.

Dkt. Kikwete amewapongeza wataalamu hao kwa kazi ambayo wameanza kuifanya ambapo wamegundua masalia mengine ya Dainasoria hao na kuwataka kuendelea kufanya utafiti kwa kushirikiana ili kugundua masalia mengi zaidi ambayo yanaweza kutunzwa na kuwa kivutio cha utalii nchini.

“Muendelee kufanya utafiti katika eneo hili ili muweze kupata masalia mengi zaidi ya Dainasoria au aina nyingine inayofanana na waliogundulika awali ambayo yakikusanywa na kuhifadhiwa vizuri yatakuwa kivutio cha utalii wa nchi yetu” amesema Mhe. Kikwete.

“Sisi kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tupo tayari kushirikiana na Makumbusho ya Taifa katika kufanya tafiti mbalimbali katika eneo hili,” alisema Dkt.Kikwete.

Mke wa Rais Msataafu wa Awamu ya Nne, Dkt Jakaya Kikwete ambaye ni Mbunge wa jimbo la Mchinga Mhe. Salma Kikwete (Mb) akipokea zawadi kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt Noel Lwoga baada ya kutembelea eneo la uhifadhi Tendaguru iliopo mkoani Lindi

Mnamo mwaka 1908 Wajerumani walifanya tafiti katika eneo hilo la Tendaguru na kugundua mabaki ya mifupa ya Dainasoria hivyo, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amewataka watafiti waendelee kufanya tafiti zao ambazo wamekwisha kuzianza na kugundua masalia mapya na kwa kufanya hivyo watagundua masalia mengi zaidi.

Awali, akitoa salamu za Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi. Dkt. Pindi Chana, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt Noel Lwoga alimshukuru Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt Jakaya Kikwete kwa Kutembelea eneo la Tendaguru na kusema kuwa wao kama Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Makumbusho ya Taifa la Tanzania wako tayari kushirikiana na watafiti kutoka Chuo kikuu cha Dar es Salaam..

By Jamhuri