Ndugu Rais, niruhusu nianze kwa kumnukuu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Mwalimu alisema: “Kudumisha uhai wa wanyamapori wetu ni suala linalotuhusu sana sisi sote katika Afrika. Viumbe hawa wa porini pamoja na mapori wanamoishi si tu kwamba ni muhimu kama mambo ya kustaajabisha na kuvutia, bali pia kwamba ni sehemu muhimu ya maliasili yetu na ustawi wa maisha yetu katika siku za baadaye.

Kwa kukubali dhamana ya kuhifadhi wanyama wetu tunatoa tamko la dhati kuwa tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa wajukuu na watoto wetu wataweza kufaidi utajiri na thamani ya urithi huu.

Kuhifadhi wanyamapori na mapori waishimo kunahitaji utaalamu maalumu, watumishi waliofunzwa pamoja na fedha. Tunatazamia kupata ushirikiano kutoka kwa mataifa mengine katika kutekeleza jukumu hili muhimu. Kufanikiwa au kushindwa kwa jukumu hilo kutaathiri si tu Bara la Afrika pekee, bali ulimwengu mzima.”

Julius K. Nyerere

Septemba 1961

Ndugu Rais, nimeyarejea maneno haya ya Mwalimu baada ya kusikiliza maelekezo yako ya Januari 15, mwaka huu ulipotangaza kuzuia amri halali iliyotolewa na mawaziri wenye dhamana na masuala ya uhifadhi, ardhi na mifugo ya kuwaondoa wavamizi kwenye maeneo yaliyohifadhiwa kisheria.

Nimejitahidi niumie kimoyomoyo kutokana na tamko lako, lakini nikiri kuwa nafsi imegoma kabisa. Imegoma hasa niliporejea kauli yako ya mara kwa mara kwamba: “Msema kweli ni mpenzi wa Mungu”. Nisipolisema hili kwako, nitaumia, na kwa kweli nitakuwa mnafiki – sifa ambayo sina.

Ndugu Rais, naamini washauri wako hawawezi kuuvaa ujasiri wa kukusaidia kukueleza madhara ya uamuzi wako huu kwenye maeneo ya uhifadhi. Ni yaleyale ya kikokotoo kwa wale waliopinga kwa nguvu zote wakiamini misimamo yao, hawakuona soni kukupigia makofi ulipotengua uamuzi huo dhalimu.

Kwa taadhima kubwa nakuomba utenge muda wako adhimu uyasome mwenyewe haya ninayokuletea ili kuepuka kulishwa maneno yasiyo ya kweli kutoka kwa wanaodhani kuwa na mtazamo tofauti na wewe ni dhambi. Lililo muhimu ni kuwa nitakushauri kwa staha kama raia mwema na mdau wa uhifadhi kwa Tanzania na Afrika.

Ndugu Rais, kwenye tamko lako umegusia mambo kadhaa mazito. Niruhusu niyataje kwa ufupi. Mosi, umezuia wavamizi kuondolewa maeneo yaliyohifadhiwa kisheria. Pili, umeagiza wataalamu/viongozi wa wizara husika wayatambue maeneo yote yaliyovamiwa yakaanzishwa vijiji 366 yarasimishwe kwa ajili ya shughuli za kibinadamu. Tatu, umeagiza maeneo ya wanyamapori na misitu yasiyo na rasilimali hiyo yagawiwe kwa wafugaji na wakulima! Nne, umeagiza sheria ya vyanzo vya maji iangaliwe ili kutowazuia ‘Watanzania’ wanaozalisha mazao kandokando ya mito. Kwa ufupi, unapinga sheria inayotenga maeneo hayo kwa mita 60 kutoka eneo la chanzo cha maji.

Ndugu Rais, umejenga hoja kuonyesha kwamba amri au maagizo yako yanatokana na ukweli kwamba Watanzania sasa ni zaidi ya milioni 55 ikilinganishwa na milioni 10 wakati wa Uhuru mwaka 1961, pia mifugo imeongezeka hadi milioni 35. Ni kweli kwamba idadi ya watu na mifugo inaongezeka kwa kasi ilhali eneo la malisho na kilimo limeendelea kubaki lilelile.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizo na rasilimali kubwa ya ardhi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Ina vyanzo vingi vya maji – mito, maziwa na mabwawa ya ukubwa wa kila namna.

Ndugu Rais, naomba niseme waliokushauri wamekupotosha. Nitajibu hoja hizi kwa takwimu. Tanzania ina eneo la ukubwa wa kilomita za mraba 965,000.

Hekta milioni 44 ni ardhi inayofaa kwa kilimo, lakini kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2017 ni asilimia 23 pekee ya eneo hilo ndilo hutumika kwa kilimo. Hapa utaona kuwa tatizo si ardhi bali ni mipango mibovu ya kuitumia ardhi tuliyonayo.

Ndugu Rais, kati ya eneo lote la Tanzania, eneo la hifadhi zote kwa ujumla wake ni kati ya asilimia 28! Hii ina maana asilimia 72 ya ardhi yote ya Tanzania si ya hifadhi.

Kwa takwimu hizi utaona kuwa Tanzania haina uhaba wa ardhi ya kilimo wala ufugaji. Tunayo ardhi kubwa isiyotumika kisayansi ili kuleta tija kwa wakulima, wafugaji na makundi mengine ya uzalishaji.

Ndugu Rais, kwa hali kama hiyo, ni jambo la kuumiza kuona leo hii tunakubali kuliacha eneo la asilimia 72 na kwenda kuvamia au kumega eneo ndani ya eneo dogo la asilimia 28 lililotengwa kwa ajili ya ustawi wa nchi?

Wakulima wengi wanalima kijima. Wanatumia jembe la mkono. Hawatumii mbolea, na hata pale wanapoihitaji wameipata kwa bei ghali. Wataalamu wa ugani hawatoshi. Upungufu huu unatoa jibu kuwa suala si ardhi, bali ni namna ya kuitunza hiyo iliyopo.

Hili linathibitishwa na kauli yako mwenyewe uliposema: “Wanafuata maeneo yenye rutuba.”

Ndugu Rais, nilipata kufika Misri. Nikaona namna jangwa lisiloota jani wala kupata tone la mvua kwa mwaka mzima, linavyogeuzwa na kuzalisha mazao mengi na mazuri yanayouzwa hadi Ulaya na Marekani. Wasaidizi walichopaswa kukushauri ni namna ya kubadili kilimo chetu kutoka cha kijima kuwa cha kisasa.

Zamani zile tulifundishwa kilimo cha marejea na mimea jamii ya kunde. Tuliambiwa faida zake kwa kuhuisha ubora wa ardhi iliyochoka. Leo nani anasisitiza kilimo cha marejea? Hawapo na kama wapo ni wachache. Matokeo yake mkulima anapoona ardhi imechoka anachofanya ni kuingia kwenye msitu wa hifadhi kuandaa shamba jingine. Kwa staili hii, hifadhi gani itabaki salama?

Ndugu Rais, kilimo chetu ni duni pia kwa maana ya kusubiri mvua za kudra za Mwenyezi Mungu. Mvua za msimu hazipo. Dunia imekwisha kubadilika. Kilimo chenye tija ni cha umwagiliaji. Kwanini tusianzishe mashamba makubwa ya umwagiliaji yatakayowezesha kuzalisha na kutoa ajira kwa Watanzania? Dunia gani inayosonga mbele ambayo badala ya asilimia 10 ya watu kulilisha taifa, asilimia 80 ndiyo inayofanya kazi hiyo. Hatuwezi kukwamuka kwa staili hii.

Tunacho Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA). Kinatoa wataalamu wengi kila mwaka. Tunawatumiaje? Juzi ulisema bila kumng’unya kuwa Tanzania inao wataalamu wengi wenye sifa kedekede, lakini wamekuwa hawatumiki. Wewe umeamua kufuta kasoro hiyo. Je, uamuzi huu unaakisi dhamira yako kwenye hili la kumega maeneo yaliyohifadhiwa?

Ndugu Rais, Mwalimu Julius Nyerere akizungumza na viongozi wa Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) na wa serikali mkoani Kilimanjaro; Agosti 10, 1975 [mwaka ambao Ndugu Rais ulikuwa kidato cha kwanza] alieleza makosa yanayowagharimu watu wa mataifa ya Ulaya na Marekani yaliyotokana na dhambi ya kuwaua wanyamapori na kuharibu misitu katika mataifa yao.

Mwalimu alisema: “Ni vizuri kujifunza kwa wenzetu waliotangulia. Na wakati mwingine ni kujifunza kutokana na makosa yao. Wenzetu waliotangulia tunaowasema zaidi ni wale wa nchi zilizoendelea sana hasa za Ulaya na Amerika Kaskazini.

Wamefanya makosa mawili makubwa – wao wanajua, sisi hatujui. Wao wanajua kwa sababu wameyafanya makosa hayo, sisi kwa sababu hatuyafanya hatujui kwamba ni makosa. Moja, mtashangaa nikilitamka. Wameharibu sana nchi zao kwa kitu wanachokiita maendeleo. Wameua vi-nyama vingi sana vilivyoumbwa na Mwenyezi Mungu – vingi. Wameua vyote. Hawana tena makundi makubwa makubwa ya wanyama kama tuliyonayo katika Afrika na hasa katika Tanzania. Hawana kabisa. Sasa wao wanajua kwamba wamefanya makosa, na wanakuja huku wanatwambia: ‘Sisi tumefanya makosa, tumeua wanyama wetu wote tumemaliza, tafadhalini msiue wanyama wenu.’ Sisi tunawaona kama wajiinga wanapotuambia hivyo. Lakini wao wanajua kosa kubwa la kufuta wanyama na kuwamaliza; na kukatakata misitu yao na kuimaliza. Wanajua kosa walilolifanya na wanatuomba tusilifanye kosa hilo. Sasa wanakuja kwa wingi, ndio hao mnawaita watalii. Wanakuja kwa wingi kuja kuona wanyama. Wewe unamshangaa huyu mtu mzima anatoka kwao mbaaaaali kuja…anatoka kwao mbaaaali, analipa hela kuja kuona tembo, kwanini. Ana akili, hana akili! Ni kwa sababu ana akili ndiyo maana anatoka kwao mbaaali sana, analipa fedha anakuja kuona tembo. Angekuwa hana akili asingekuja. Anajua faida ya kuwa na ma-tembo, na ma-simba, na ma-nyati, na ma-chui, na ma-pundamilia katika nchi hii, lakini kwao wameshafuta. Sasa wanaanza kutuomba, wengine wanaanza kutuomba tuwauzieuzie angalau wafufuefufue, lakini kufufua si jambo jepesi. Ukishaifuta misitu, kuifufua na kuweka wanyama waishi kama walivyokuwa zamani ni vigumu sana, kwanza hali yake ile ni tofauti. Huwezi kuifufua, vigumu sana. Wala hawajui ilikuwaje hata waweze kuifufua. Sasa nasema wanatushawishi – Wazungu wanatushawishi katika jambo hilo ambalo hatujafanya kosa, tusifanye kosa.

Serikali ya Tanzania imekubali, nadhani wananchi wanaanza kukubali kutofanya kosa hilo lililofanywa na wenzetu. Tuhifadhi wanyama wetu na tuhifadhi misitu yetu. Tusivuruge vuruge mazingira ambayo tumeyarithi, na kwa kweli hatujui yamechukua muda gani hata yakawa hivyo; halafu tunafika sisi tunaita maendeleo tunavuruga vuruga, tunaharibu; tunaua wanyama, tunakata miti. Matokeo yake hatuwezi kuyajua.”  Mwisho wa kunukuu. Nakuomba Ndugu Rais uyatafakari maneno haya ya Mwalimu na uone lipi la kuondoa katika hayo [kama kweli lipo].

Please follow and like us:
Pin Share