Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi atatoa hotuba ya ufunguzi wa maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu Sabasaba kwa kutumia lugha ya Kiswahili.

Ameyasema hayo leo Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumkaribisha Rais Nyusi ambaye yupo nchini kwa ziara ya kiserikali ya siku tatu.

Kesho Jumatano Julai 3, 2024 Rais Nyusi atakuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa maonyesho hayo ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu Sabasaba na atasindikizwa na mwenyeji wake Rais Samia.

Rais Samia amesema kuwa hayo yanafanyika ni kutokana kwamba watu wa nchi hizo mbili wanaongea lugha zinazoelewana.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mazungumzo Rasmi na Mgeni wake Rais wa Msumbiji Mhe. Filipe Jacinto Nyusi aliyeambatana na ujumbe wake Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 02 Julai, 2024.

“Rais Nyusi akizungumza kimakonde, Wamakonde waliopo Mtwara pale watamuelewa na kujua nini amesema, Tamaduni zetu pia zimetuunganisha na hayo ndio yametufanya tuwe wamoja katika kufanya biashara, uwekezaji, kuona, na kufanya Msumbiji kuwa siyo tu nchi jirani kwa Tanzania bali ni ndugu na rafiki wa siku zote,” amesema .

Amesema urafiki wa nchi hizo mbili uliwekwa vizuri na wababa wa mataifa hayo mawili ambao ni marehemu Edward na Mwalimu Julius Nyerere wakati ule nchi hizo zikitafuta uhuru kutoka kwa wakoloni.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na mgeni wake Rais wa Msumbiji Mhe. Filipe Jacinto Nyusi wakati wakishuhudia utiaji saini Hati ya Makubaliano ya kushirikiana katika masuala ya Afya baina ya Tanzania na Msumbiji Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 02 Julai, 2024. Kulia ni Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akionesha Hati ya Mkataba huo pamoja na Naibu wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Msumbiji Mhe. Manuel José Gonçalves
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na mgeni wake Rais wa Msumbiji Mhe. Filipe Jacinto Nyusi wakati wakishuhudia utiaji saini Hati ya Makubaliano baina ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania na Taasisi ya Msumbiji ya Uwekezaji na Uwezeshaji Usafirishaji Nje ya Nchi, Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 02 Julai, 2024. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC Bw. Gilead Teri akitia saini Hati hiyo pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa AIPEX Bw. Gil Da Conceçao Bires kwa upande wa Msumbiji.