Doyo Hassan Doyo ambaye ni katibu Mkuu wa Chama cha ‘Alliance For the Democratic Change’ (ADC), amesema kitendo cha Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuitisha mkutano na vyama vya siasa kinapaswa kupongezwa kwa kuwa kinaimarisha afya katika siasa za hapa nchini.

Akizungumza katika mahojiano na JAMHURI DIGITAL Dar es Salaam leo Januari 3, 2023,Doyo amesema hatua hiyo ya Rais Samia, ni wazi imeonyesha dhamira yake ya kweli kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika siasa hususani kwa vyama vya upinzani na kwamba kwa kuliona hivyo ameona ni vyema kukaa nao pamoja na kuzungumza.

Doyo amesema kuwa hatua ya rais kuruhusu kwa mikutano ya hadhara ni jambo la kupongeza sana kwani sasa wadau wa masuala ya siasa nchini wameona ushirikiano ulipo kati ya Serikali na vyama vya siasa.

“Ukweli binafsi nimefarijika na hatua ya Rais Samia kuitisha mkutano huu mapema kabisa kwa mwaka, na kutoa maamuzi ya kuruhusu kwa mikutanoi ya hadhara sasa Tanzania itakuwa na mipango ya pamoja katika kuleta maendeleo” amesema Doyo.

Amesema wao kama ADC watahakikisha wanatimiza wajibu wao na kwenda kutoa mchango wa mawazo yao pale watakapopewa nafasi, lengo ni kuona hali ya kisiasa nchini inahimarika kama ambavyo imeanza kujionesha hivi karibuni tangu Rais Samia Suluhu Hassan ashike madaraka ya kuongoza nchi.

By Jamhuri