CCM si Shwari

Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Dodoma

Kwa muda mrefu sasa vita ya mamlaka bado inaendelea kuathiri mwenendo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) huku ikizidi kuchagizwa na vitendo vya fitina, uongo na uzushi.

Licha ya kukemewa na hatua mbalimbali za kinidhamu na kimaadili kuchukuliwa kwa baadhi ya wanachama, lakini vitendo hivyo bado vimekuwa kama saratani isiyotibika, kwa sababu vinazidi kumea kadiri siku zinavyosonga mbele.

Vitendo hivyo bado vinaendelea kufukuta chini chini. Kwa nini vinaendelea kushamiri? Je, pengine ni kwa sababu ya vita ya madaraka kati ya makada na wakereketwa hasa kabla, wakati na baada ya uchaguzi wa ndani wa chama hicho?

Hatua hiyo imesababisha hata baadhi ya viongozi wa chama hicho kunukuliwa mara kadhaa siku za nyuma kupitia vyombo vya habari wakivilalamikia.

Kama viongozi hao wakizungumzia hadharani maana yake tafsiri ya hatua ya vitendo hivyo kuzidi kuendelea haina tofauti na donda ndugu huku wale wanachama wapya au waliohamia kutoka vyama vya siasa au walipokuwa watumishi katika taasisi za serikali wakinyoshewa kidole.

Kuthibitisha hilo ni kauli zilizotolewa Desemba 8, 2022 katika Mkutano Mkuu wa 10 wa CCM uliofanyika jijini Dodoma na kuashiria kwamba mambo ndani ya CCM bado yanazidi kuendelea kuwa si shwari na kuibua mjadala kwa baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa.

Katika mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan, amewataka wanachama wa chama hicho kutokubali mikikimikiki ya uchaguzi kuwa chanzo cha wao kufarakana na kuanzisha nyufa.

Amesema wakati wa uchaguzi ndani ya CCM kuna makundi mengi, wagombea nao ni wengi na wanatofautiana, lakini wakimaliza waendelee kuwa pamoja.

“Nyufa ndani ya chama chetu, wamesema wakubwa zangu hapa na mimi nataka niseme kuna vijinongwa nongwa ndani ya chama chetu vinaendelezwa, lakini nataka niseme kwa mwana CCM ambaye anakijua chama.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi

“Anayejua mwelekeo wa sera za chama chetu au kwa wana CCM waliotokana na chama chetu, hawawezi kufanya nongwa wakaharibu chama chao, lakini kuna wana CCM walioshika nyadhifa tofauti wakapitia kwa CCM, hawa wanaweza kutuharibia chama.

“Hivyo natoa wito kwa viongozi wote wa CCM na jumuiya zake kuzingatia ukweli huo na sote kwa pamoja kupanga na kutekeleza ibara ya 5 ya kwanza ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977, toleo la mwaka 2002,” amesema.

Pamoja na mambo mengine, Rais Samia, amekazia kwa kutoa kauli hiyo baada ya Rais wa Awamu ya Nne na Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Jakaya Kikwete na Rais wa Awamu ya Saba wa Zanzibar na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Dk. Ali Mohamed Shein, kuvikemea vitendo hivyo.
Kikwete amemtaka Rais Samia kutosikiliza porojo za watu wanaodai ana mgombea wa urais katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2025.

Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo akishauriana jambo na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana.

“Kwamba sijui nina kijana gani atagombea, sijui nina mzee gani atagombea, ni upuuzi mtupu. Si kwamba nasema nawazuia, lakini simuoni mwana CCM mwaka 2025 atakayechukua fomu kukupinga, labda mambo yaharibike sana kati ya sasa na wakati huo, lakini siamini hivyo.

“Si mila yetu, lakini niseme ukweli tu, hapa Tanzania leo kuna mwanasiasa maarufu kumshinda Samia? Hayupo ndani ya chama hiki, hayupo nje ya chama hiki, usibabaishwe na maneno hayo, na wengine wanaosema sijui waziri gani kaenda wapi, sijui kukusanya fedha,” amesema.

Pia amesema hao ni waganga njaa na waliyapata maneno hayo kutoka kwa aliyemuita bwana Fulani, aliyekuwa anajiita mwanaharakati huru.

“Uongo mtupu, na mimi ninachowaombeni ndugu zangu acheni uongo, yaani katika kipindi cha kuelekea uchaguzi ukisoma mitandao kuna maneno ya ovyo ovyo, yote ni ya kutunga tu. Fulani sijui yuko hivi, fulani sijui anaungwa mkono na mzee huyu, fulani anaungwa mkono na mzee huyu, upuuzi mtupu, tuache hii tabia, tabia hii inakigawa chama chetu bila ya sababu,” amesema.

Vilevile amesema watu hao wanawatengenezea viongozi wao stress isiyokuwa na msingi badala ya kukusanya nguvu zao kujenga chama na kutimiza majukumu yao ya kikatiba ya kuongoza nchi.
“Viongozi wanaanza kuhangaika na upuuzi wenu, this is not fair, na kwa mwana CCM anayefanya hivyo, wengine mkiwasikia wanasema hivyo waiteni katika kamati ya maadili.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Samia Suluhu Hassan akifafanua jambo wakati akiongoza Kikao Maalum cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, katika Ukumbi wa NEC (White House), Makao Makuu ya CCM jijini Dodoma. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Rais Mstaafu wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein.

Tumekusikia ukisema kuna mawaziri wamekwenda huko, sasa wamepewa cheo na sasa wanatafuta cheo cha urais, ni nani huyo,” amesema na kuongeza:

“Kama hamjui aambiwe acha uongo, ukome, hiyo ndiyo njia pekee itakayoondoa uchimvi wa kuchimba watu na kuchonganisha watu. Chama chetu ni kikubwa, hakistahili kuvumilia upuuzi kama huo. Mkiuvumilia, chama hiki kitagawanyika kwa masilahi ya watu wapuuzi. Kwa masilahi ya watu waongo, wenye kazi ya kukaa mitandaoni kuandika lipi jipya.

“Lakini yale yote yataleta mifarakano katika chama chetu, hayana kichwa wala miguu, ninachowaombeni kuweni wakali, mkimjua mwanachama mwenzetu anaendesha upuuzi huu mwiteni, bwana umetupa taarifa nzuri kumbe unawajua, tuambie. Akiwa na ushahidi wa kutosha mnawaita na wanaotajwa mnawapa ukweli. Muongo mnamwambia acha uongo wako na shika adabu yako.”

Amesema wakifanya hivyo watajenga mshikamano na utulivu katika chama hicho huku akikazia hoja yake kwamba maneno hayo yatakuwa mengi kuanzia sasa hivi hadi kuelekea mwaka 2025.
“Wako watakaokuja kusema haki ya Mungu wanakutana, kumbe kakutana yeye na mjinga mwenzake. Tutawatia jaka moyo viongozi wetu bila sababu na dawa yake ni hiyo tu kukomesha uongo,” amesema.

Katika hatua nyingine, amesema hataki kutoa mifano ya yaliyowasibu kwenye maisha yao au waliyoyapitia kuhusu mazingira kama hayo, lakini wakati wa kipindi cha uongozi wake hakutoa nafasi ya upuuzi huo.

Amesema wao wanapaswa kuwasaidia viongozi wa chama hicho kupata utulivu na katika kufanikisha hilo wanatakiwa wasizue uongo.

“Tukijiepusha na hayo chama hiki kitakuwa shwari hadi tunakwenda mwaka 2025 na tutakuwa na kazi moja tu, kujiandaa na mapambano dhidi ya wenzetu,” amesema.

Naye Dk. Shein amesema inabidi wakaze kamba kuyasimamia na hakuna budi wanachama wanaokiuka wafukuzwe kwa kuwa siku za nyuma wameshafukuzwa watu wazito katika CCM kwa ukosefu wa maadili.

“Sasa mtu anaitwa anasemwa, anaonywa, anapewa karipio, kama hasikii anafanywa mengine ya ziada. Kwa hiyo nidhamu na maadili ya chama, na bahati nzuri yote yameandikwa ndani ya chama chetu.

“Niliwahi kusema siku ya maziko ya Magufuli kwamba Samia namfahamu vizuri. Watu wakainua macho wakanishangaa. Ana uwezo mkubwa sana, nafasi hii kapewa si kwa kubahatisha, ule Umakamu wa Rais aliopewa anastahili kuwa nao na Mungu kamuweka leo kawa Rais wetu,” amesema.

Aidha, amesema wao wakubwa zake hawafanyi nongwa, hawajahamaki na wanamsaidia, kisha akahoji: “Hajui makada wadogo?” Amesema lazima wamheshimu Rais Samia na wamsaidie.

Pia amesema anamjua Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi na hata katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 aliwaambia Wazanzibari kwamba anamjua hadi uwezo wake. Hata hivyo, ameshangaa kwamba sasa hivi baada ya ushindi mambo yamekwenda shaghalabaghala.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka

“Tunagombania nini? Tunazozana kitu gani? Sote wamoja. Dk. Hussein kaza kamba, fanya kazi. Tuna taratibu zetu, tusiwatwishe viongozi wetu mizigo isiyokuwa ya lazima kwa tamaa zetu na ushawishi wa watu wengine. Tufanyeni kazi na tuwasaidie Samia na Dk. Mwinyi wakiongoze chama chetu,” amesema.

CCM yanyonyoa mbawa

Licha ya wajumbe wa mkutano huo kumchagua Rais Samia kuendelea kuwa mwenyekiti wao kwa kumpigia kura 1,914 za ndiyo huku moja ikimkataa, Dk. Mwinyi naye kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho (Zanzibar) baada ya kupata kura 1,912 za ndiyo na moja ya hapana na Abdulrahman Kinana kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho (Bara) baada ya kupata kura 1,913 za ndiyo na mbili za hapana, pia kimefanya mabadiliko ya kimfumo.

Mabadiliko ya chama hicho yamepitishwa katika mkutano huo baada ya idadi ya wajumbe katika vikao vya uamuzi, ikiwamo wajumbe wa NEC kuongezeka kutoka 30 hadi 40.
Zamani kulikuwa na nafasi 15 za wajumbe wa NEC kutoka Bara na 15 kutoka Zanzibar na mabadiliko hayo yameongeza nafasi tano kila upande.

Huku katibu wa itikadi, siasa na uenezi sasa ni nafasi ya kuajiriwa badala ya kuchaguliwa na hatua hiyo inatajwa kuwa itakisaidia chama hicho. Pia nafasi za uteuzi kwa NEC zimeongezeka hadi 10 kutoka saba ilivyokuwa hapo awali.

Katika u-NEC mchuano mkali ulikuwa kwa mawaziri, viongozi wa zamani serikalini, waandishi wa habari na wanamichezo, huku jumla ya wagombea kutoka Bara na Zanzibar walikuwa 374 wakigombea nafasi 40.