Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka amewataka wana CCM kutopoteza muda kwa malumbano na majibizano kwa kuwa kuna kazi muhimu mbele yao ya kujenga Chama na nchi.
 
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi wameanza vizuri uongozi katika kuwatumikia wananchi, hivyo ni jukumu la wana CCM na Watanzania kwa jumla kuwaunga mkono.
 
Aidha, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah amewataka wale wenye tamaa ya kutaka vyeo kujitafakari na kuchapa kazi kwa kuwa kazi kubwa Sasa ni kuijenga nchi.
 
Shaka ameyasema hayo jana katika mapokezi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM (Zanzibar) Dk. Hussein Ali Mwinyi yaliyofanyika katika viwanja vya Afisi Kuu ya CCM Zanzibar (Kisiwandui) na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali.
 
“Niwaombe wana CCM wenzangu tusipoteze muda wa marumbano, tuna kazi ya kukijenga Chama tuna kazi ya kuijenga nchi, tuna kazi ya kuijenga Zanzibar hii. Dk. Mwinyi ameanza vizuri jasiri mwongoza njia lazima wafuasi tufuate…bega kwa bega,” amesema.
 
Shaka alisema Chama Cha Mapinduzi Zanzibar kipo katika mikono salama chini ya uongozi wa Dk. Mwinyi kwa kuwa ameonyesha uwezo mkubwa wa uongozi na kusimamia maendeleo ya wananchi. 
 
“Makamu Mwenyekiti umekabidhiwa jahazi hili hatuna wasiwasi na wewe, umekabidhiwa jahazi hili likiwa salama ‘inshallah’ (Mungu akipenda) utatuvusha…wewe ni nahodha jabari, wewe ni nahodha makini utatuvusha. Wasiojua waanze kupata salamu tunakuja na Dk. Mwinyi,” alisema.
 
Katibu Mwenezi Shaka alisema moja ya mambo ambayo CCM haijawahi kukosea ni katika kuwapata viongozi makini wa kuivusha nchi.
 
Shaka alisema kasi ya Rais Dk. Mwinyi imeanza kuwatisha baadhi ya watu waliokuwa na tamaa ya madaraka ambao sasa wameanza kutapatapa.
 
“Nimesikia kwamba wanafikiria sijui watasusa, msuse msisuse shughuli ipo,” amesema.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi, akiwapungia mkono wananchi wakati wa mapokezi yake baada ya kuchaguliwa kuwa mkmu Mwenyekiti wa CCM. Hafla ya mapokezi ilifanyika jana kuanzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Amani Abeid Karume, hadi Afisi Kuu ya Makao Makuu ya CCM Zanzibar (Kisiwandui). (Picha zote na Fahad Siraj wa CCM).
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka akizungumza wakati wa mapokezi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi baada ya kuchaguliwa kushika wadhifa huo wiki iliyopita jijini Dodoma, hafla ya mapokezi hayo ilifanyika jana Afisi Kuu ya Makao Makuu ya CCM Zanzibar (Kisiwandui). (Picha na Fahad Siraj wa CCM).

By Jamhuri