Rais Samia awakumbuka watoto kituo cha Madina Pwani

Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia,Pwani

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa zawadi ya Sikukuu za mwisho wa mwaka ikiwa ni pamoja na vitoweo ,mchele , maharage,mafuta ya kupikia ,vinywaji na viungo vingine mbalimbali vya kupikia.

Akimwakilisha rais kukabidhi bidhaa hizo katika kituo Cha kulelea watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu ,Makao ya malezi Madina kilichopo Mtaa wa Vikawe kata ya Pangani,Kibaha Mjini, Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge amesema , kituo hicho kinawakilisha vituo 37 vilivyopo mkoa mzima.

Ameeleza ,Rais kwa kutambua makundi maalum ametoa zawadi hizo ili watoto hao washeherekee kama watakavyosheherekea wengine ambao wanaishi kwa furaha .

“Nimekuja hapa leo kumwakilisha Rais wetu, amewaletea zawadi pamoja na salamu za sikukuu za mwisho wa mwaka, ambapo amewaletea mbuzi wawili,mchele kilo 60,maharage kilo 40, mafuta lita 20 ,juise na viungo vingine mbalimbali”amesema Kunenge.

Aidha Kunenge ameeleza ,mkoa una Jumla ya makao ya malezi 37 vyenye Jumla ya watoto 1,301, na kituo hicho kina watoto 30.

Mkuu huyo wa mkoa aliwaasa wadau wa Maendeleo na wenye uwezo kujenga tabia ya kujitolea kwa vituo vya watoto wenye mahitaji.

Kwa upande wao, watoto wa Makao ya Madina Zainab Athuman na Jumanne Manzi amemshukuru Mungu kwa kumwezesha Rais kupata na kuweza kuwapa zawadi hizo.

Nae Mlezi wa watoto Makao Makuu ya Madina Fatma Abdilai alieleza, wananchi waendelee kumuombea Rais Samia kwa mengi anayofanya nchini na kutekeleza ilani kwa kutambua makundi maalum.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Kibaha Mjini, Mwajuma Nyamka alimshukuru Mwenyekiti wa CCM Taifa Dkt.Samia kwa kuitendea haki ilani ya Chama na kujali.