Rais Samia awashika mkono akina mama waliojifungia njiti

Rais Samia ametoa msaada wa mahitaji muhimu kwa mama waliojifungua watoto njiti katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni, Kigoma.

Mahitaji hayo yamekabidhiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Angellah Kairuki kwa niaba ya Rais Samia, mara baada ya kuweka jiwe la Msingi Jengo la kutolea Huduma za Wagonjwa wa Dharura (EMD) na Wagonjwa wa uangalizi Maalum (ICU) katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni Kigoma. Leo tarehe 18 Oktoba, 2022.

“Rais Samia amewashika mkono mama waliojifungua watoto njiti kwa kutoa mashuka, blanket,vitenge,sabuni, pampasi, mafuta ya nywele na mahaitaji mengine ikiwa ni pamoja ba vyakula kama Mchele na Sukari” amesema Waziri Kairuki.

Kwa upende wake,Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema Serikali italeta Vifaa tiba kwa ajili ya kuhudumia Watoto njiti ikiwa ni pamoja na Mashine za Kufua hewa ya Oksijeni, Mashine za Kuzalisha hewa joto na Mashine za kutunza Watoto njiti.

Naye, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni, Dkt. Stanley Binagi amesema vifaa tiba na Mahitaji hayo yatasaidia utoaji wa huduma bora kwa Watoto Njiti waliopo na wanaoendelea kuzaliwa katika Hospitali hiyo.

Akitoa shukrani zake, Mama wa Mtoto Njiti, Bi. Halima Matayo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha huduma za Afya nchini hasa wa Wakina Mama, na kwa kutoa zawadi ambazo zitawasaidia katika kuwahudumia na kuwalea Watoto wao.