Makampuni ya Japan yameonesha kuvutiwa na kahawa ya Tanzania katika maonesho ya Kimataifa ya Kahawa Japan yajulikanayo kama 2022 Japan Specialty Coffee Conference & Exhibition yaliyofanyika jijini Tokyo tarehe 12 – 14 Oktoba, 2022.

Maonesho hayo ambayo yalishirikisha taasisi zipatazo 235 zinazoshughulika na kahawa kutoka kote duniani, yaliandaliwa na kusimamiwa na Taasisi ya Kahawa ya Japan (Specialty Coffee Association of Japan – SCAJ).

Kutokana na mapokeo mazuri ya kahawa ya Tanzania miongoni watumiaji na makampuni ya Japan katika maonesho hayo, soko la kahawa ya Tanzania nchini humo linatarajiwa kuongezeka kutoka asilimia 32 ya sasa, ambayo ni sawa na wastani wa kilogramu 15,000,000 zinazounzwa nchini humo kwa mwaka. Kiwango hiki kimeelezwa kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi tatu duniani zinazouza kahawa kwa wingi nchini Japan.

Maonesho hayo imekuwa ni fursa adhimu katika kukuza wigo wa soko na kujihakikishia soko la kudumu la kahawa ya Tanzania nchini Japan, ikiwa ni miongoni mwa kahawa pendwa nchini humo iliyopewa jina maarufu la kibiashara “Tanzania Kilimanjaro Coffee”.

Ujumbe wa Tanzania katika maonesho hayo uliongozwa na Bodi ya Kahawa Tanzania ikiwa imeambatana na wawakilishi wa vyama viwili vya ushirika na makampuni matatu ya Kitanzania yanayohusika na uzalishaji na uuzaji wa kahawa ikiwemo; Kagera Cooperative Union (KCU), Karagwe District Cooperative Union (KDCU), Kampuni ya Kaderes Peasants Development (KPD),Kampuni ya Acacia na Kampuni ya Touton Tanzania Ltd.

By Jamhuri