Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Rufiji

Serikali imetenga eneo la ukubwa wa hekta 60,000 kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji wa zao la mpunga katika wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa kauli hiyo, Septemba 20, 2023, akiwasalimia wananchi wa Kata ya Ikwiriri wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.

Alisema kwa mwaka huu wamekusudia kulima hekta 30,000 za mpunga kupitia skimu ya umwagiliaji ambayo serikali imetenga kwa ajili ya shughuli za kilimo na kwamba mwaka ujao wanatalima nyingine 30, 000.

“Tumeamua kugawa eneo la bonde la Rufiji kwa ajili ya shughuli za kuzalisha umeme na nusu yake skimu za umwagiliaji na mwaka huu tunaanza kulima hekta 30,000, zitakuwa mahsususi kwa ajili ya kulima mpunga ambao utalisha mataifa mbalimbali kutokea hapa Rufiji “anasema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Hata hivyo aliwahamasisha vijana kuchangamkia fursa hiyo ya kilimo cha umwagiliaji kupitia mradi ya Jenga Kesho iliyobora (BBT) kwa kuzalisha mpunga kwa wingi ambao utauzwa ndani na nje ya nchi kutokana na kuwepo kwa soko la uhakika.

Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, alimshukuru Rais wa Tanzania kwa kutoa bure pembejeo za kilimo ikiwamo mbolea ya ruzuku katika zao la korosho ambalo amedai kutokana na hatua hiyo ubora na uzalishaji umeongezeka.

Alisema kwa sasa wanapata bure ruzuku ya sulphur na ya unga ambayo hapo awali walikuwa wanapata changamoto ya kudumu gharama za pembejeo za kilimo.

Please follow and like us:
Pin Share