Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, aDodoma
Wiki iliyopita ilikuwa na mambo mengi. Nimepata fursa ya kuwa katika Ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati Rais Samia Suluhu Hassan anatoa hotuba ya kuvunja Bunge la 12, lililoanza mwaka 2020 na sasa limehitimishwa mwaka 2025. Si kawaida yake, lakini zamu hii Rais Samia amehutubia kwa saa 2:47. Hotuba za Rais Samia tumezoea zinachukua nusu saa au chini ya muda huo, ila zamu hii aliamua.
Aliamua kutaja maeneo mengi ya msingi ambayo Serikali ya Awamu ya Sita imeyatekeleza. Amegusa afya – ujenzi wa vituo vya afya, hospitali, zahanati na kuviwekea vifaa na mitambo ya kisasa ya tiba.
Ameelezea eneo la elimu jinsi ambavyo serikali imejenga madarasa na shule nyingi za sayansi. Shule mpya 26 za wasichana za sayansi na saba za wavulana, kurejesha mafunzo ya ufundi kwa wanafunzi wa sekondari na kubadili mchepuo, ambapo sasa wanafunzi wanafundishwa biashara na historia ya Tanzania, ni moja kati ya mageuzi makubwa.
Mwanadamu asipoifahamu historia yake, ni rahisi kupotea njia. Biashara ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Kwamba watoto wetu kama hawana ujuzi wa biashara, tunahatarisha ustawi wao. Wakiwa na ujuzi wa biashara, wakafundishwa kulipa kodi katika umri mdogo, wakafundishwa kukataa rushwa, tunakuwa tunajenga nchi yenye misingi imara.
Sitanii, silengi kuirudufisha hotuba aliyoitoa Rais Samia katika makala hii. Itoshe tu kusema kuwa hii ilikuwa hotuba nzito kupata kusikika kutoka kwa Rais Samia. Hotuba hii imegusa kila sekta kwa utuo. Hata na yeye alifahamu uzito wa hotuba hii ndiyo maana akasema amezungumza kwa takwimu. Hapana shaka alikuwa akiwasema wanaobeza maendeleo yaliyofikiwa na nchi yetu.

Rais amegusa umeme. Kwamba wakati anaingia madarakani, nchi yetu ilikuwa na wastani wa megawati 1,600 hivi. Leo ina megawati zaidi ya 4,000. Niseme umeme ni maendeleo. Baada ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kusambaza umeme hadi kwenye vitongoji, Tanzania inameremeta. Kuna sehemu ukipita usiku kwa sasa unajiuliza ni mji upi? Kumbe ni kijiji.
Umeme ni nguzo ya maendeleo kwa taifa lolote. Mataifa yaliyoendelea yanatumia umeme mwingi. China kwa sasa inatajwa kutumia umeme megawati 900,000. Nchi nyingi zenye uchumi wa kati wa juu, lengo ambalo Rais Samia ameliweka kuwa Tanzania italifikia ifikapo mwaka 2030 zinatumia umeme kati ya megawati 15,000 na 30,000. Tujipongeze kiasi kwani katika Afrika Mashariki, Tanzania sasa ndiyo nchi inayozalisha umeme mwingi kuliko yoyote.
Rais Samia alipotaja kwenye hotuba yake juu ya ukombozi uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kupitia kilimo, amewagusa wananchi. Wiki iliyopita nilipata fursa ya kuwa Iringa. Nimeushuhudia mradi mkubwa wa umwagiliaji wa Mkombozi uliopo Tarafa ya Pawaga, Iringa. Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa, mradi huu unakwenda kumwagilia ekari 15,000.
Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inajenga mabwawa 29 makubwa na madogo 200 kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Serikali inakwenda kujenga gridi ya taifa ya maji kutoka Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika, kwa kuweka mtandao wa maji ya kilimo cha umwagiliaji nchi nzima.
Hadi sasa katika kipindi cha miaka minne serikali imewekeza zaidi ya Sh trilioni 1.2 katika umwagiliaji pekee. Hii ni ishara ya umakini wa hali ya juu katika kuendeleza kilimo.
Sitanii, inawezekana bila tafsiri sahihi ya mpango huu wa kilimo cha umwagiliaji msomaji usielewe. Nchi yetu asilimia 70 ya watu wake wanategemea kilimo. Sehemu kubwa ya nchi yetu inapata mvua kwa wastani wa msimu mmoja, sawa na miezi minne. Kuna maeneo mengi mpunga wanalima na kuvuna mara moja kwa mwaka.
Mahindi, kahawa, pamba, karanga, ndizi na mazao mengine mengi, kwa kiasi kikubwa yanalimwa mara moja kwa mwaka. Hii ina maana kuwa wakulima wa Tanzania, ambao ni asilimia 70 ya wakaazi wa Tanzania, wanafanya kazi kwa miezi minne tu, miezi iliyosalia inakuwa ya ukame, hawawezi kupanda kitu chochote. Mpango huu wa kilimo cha umwagiliaji, sasa utamwezesha mkulima kulima mara mbili au tatu kwa mwaka, kulingana na zao analolima.

Kama ni mahindi kwa miezi mitatu atalima angalau mara tatu kwa mwaka. Hii maana yake ni kwamba unampa mkulima nafasi ya kupata kipato mara tatu ya kipato chake cha sasa. Lakini pia unampa kazi ya kufanya kwa mwaka mzima na kupunguza mawazo ya kucheza ngoma na kuoa kwa misimu kadiri inavyokwisha. Mpango huu unaokwenda sambamba na maghala ya kuhifadhia mazao, ni mpango mzuri unaolikomboa taifa letu. Nawiwa kuipongeza serikali ya Rais Samia kwa kufanya uamuzi huu wa kijasiri.
Sitanii, najua mawazo na upepo kwa sasa uko kwenye siasa. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimefungua dirisha la wagombea kuchukua fomu. Tayari nimeshuhudia mbio za wagombea. Namshukuru Mungu nimeshuhudia mbio za uchaguzi tangu mwaka 1980. Naweza kusema nazifahamu kiasi siasa za nchi yetu. Yameongezeka majimbo ya uchaguzi mwaka huu.
Wakati nikiwatakia kila la heri, naomba kusema jambo mahsusi kwa Jimbo jipya la Kivule, la jijini Dar es Salaam. Jimbo hili mwanzoni lilifahamika kama Jimbo la Ukonga. Ikawa lina wapigakura wengi, likagawanywa na kuwa majimbo mawili; Ukonga na Segerea. Baadaye bado Ukonga limeonekana ni kubwa kwa wingi wa watu, limegawanywa na kuzaa Ukonga na Kivule.
Sitanii, nimeanza kushuhudia maajabu. Jimbo hili limefanyiwa kuwa la mazoezi. Nadhani katika Jiji la Dar es Salaam ndilo jimbo pekee lenye barabara mbovu kuliko jimbo lolote. Ni jimbo pekee ambalo kwa upana wake, halina mtandao wa lami unaofikia kilomita 15. Lipo jijini Dar es Salaam. Barabara ya Banana – Kitunda – Kivule inatia huruma. Miaka yote tunamkumbuka angalau marehemu Dk. Makongoro Mahanga.
Mbunge huyu, Mungu amlaze mahala pema peponi. Baadaye alikuja Mama Eugen Mwaiposa, alipopata ubunge akahamia Mikocheni.
Mama huyu alifariki dunia Juni 2, 2015. Hakuzigusa barabara, wala hakushughulika na matatizo ya wakaazi wa Ukonga. Baada yake akaja Mwita Mwikwabe Waitara. Huyu alichaguliwa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mwaka 2015. Jumamosi, Julai 14, 2018 alitangaza kukihama (CHADEMA) akaunga mkono juhudi na kuhamia CCM.
Baada ya hapo akaja Jerry Silaa. Mbunge huyu kama watangulizi wake, Jimbo jipya la Kivule aliliacha yatima. Ndiyo maana hata hakuwaza kugombea kupitia jimbo hili. Barabara pamoja na kumwambia mara kadhaa, hakupata kuzishughulikia.
Kila kukicha anatangaza miradi ya ujenzi wa barabara usiotekelezeka. Ipo barabara ya Kitunda – Relini – Machimbo – Moshi Baa – Kanyigo – Mwembeni. Hii ni barabara ya msaada mkubwa kwa wakaazi wa jimbo hili, ila kwake haikuwa na umuhimu.
Sitanii, sasa Jimbo hili jipya la Kivule nimeambiwa watangaza nia wanafikia 12. Hadi naandika makala hii, waliochukua fomu ni sita tu. Yameanza kujitokeza makosa yaleyale yaliyotangulia. Unakuta mtu si mkaazi wa jimbo hili, lakini siku tatu zilizopita amenunua kiwanja, anajenga nyumba mchana na usiku apate ubunge, baada ya hapo arejee kwao Mikocheni. Hawa ma-TX wajue Kivule si pa kufanyia mazoezi.
Wajumbe nao waelewe dhamana waliyonayo kwa wakaazi wa jimbo hili. Kwamba wakipenyezewa vijisenti kama 50,000 au hata 300,000 wakauza maendeleo ya jimbo, laana wataichuma duniani na mbinguni. Jimbo la Kivule tunataka tupate mbunge ambaye kila atakayemsikia ajue kweli jimbo lina mbunge, si hawa yeboyebo.

Najua tatizo hili lipo sehemu nyingi nchini. Vikao vya chama vinavyochuja wagombea naamini viongeze na kigezo cha ukaazi katika jimbo husika.
Wapo watu wana zaidi ya miaka 10 hawajafika kwenye majimbo waliyokwenda kuchukua fomu. Ni wazi hawa wanakuwa hawayafahamu matatizo ya wananchi na kuna kila dalili wakipewa ubunge, kwa kuwa wamekwenda majimboni kama kwereakwerea, baada ya mavuno watarejea makwao.
Bunge lililomaliza muda lilikuwa Bunge la aina yake. Zaidi ya asilimia 60 hawakuingia bungeni kwa mapenzi ya wapigakura. Kwa kufahamu aliyewaingiza bungeni wakawa na jeuri kwa wapigakura. Sasa wakati umefika. Wananchi tuamue wenyewe kusuka au kunyoa.
Mpira uko uwanjani, tuna jezi na njumu. Refarii pia ni mwanakijiji au kitaa mwenzetu. Tuwashikishe adabu hawa waliotukoga hadi wakaanza kudai wapewe namba maalumu za magari. Mungu ibariki Tanzania.
0784 404 827