Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan amewahakikishia Watanzania hakutakuwa na maandamano Oktoba 29 na kuwataka wajitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura bila wasiwasi.
Rais Samia ametoa kauli hiyo, wakati akihutubia maelfu ya wakazi wa Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, wakati wa mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani kwenye viwanja vya Leaders leo Oktoba 21, 2025.
Ndugu zangu niwahakikishie Oktoba 29, tokeni mwende mkapige kura, ninayeongea hapa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa nchi hii, nataka niwaambie maandamano yatakayokuwapo ni ya watu kwenda vituoni kupiga kura.
Hakuna maandamano mengine yatakayokuwapo, hakuna tishio la kiusalama litakalokuwapo anayesema ni Amiri Jeshi Mkuu wa nchi hii, niwaombe ndugu zangu twendeni mkapige kura, twendeni mkapige kura, baba ukitoka hakikisha umetoka na familia, kila aliyeandikishwa afanye hivi,amesema.

Amewataka mabalozi wa chama hicho kuhakikisha wanatoka na watu wao kwenda kupiga kura.
Twendeni tukaheshimishe CCM, twendeni tuhaiheshimshe Tanzania tukapige kura kwa usalama turudi kwa usalama.
Ndugu zangu mingine niachieni mimi, matusi niachieni mimi nayebeba kwa niaba yetu, manabii wetu wanajua Bwana Yesu alisulubiwa kwa kukomboa watu kwa amri ya Mungu, alikuwa anafanya kazi ya watu, Nabii Mohamed alipigwa mpaka akatolewa meno kwa kufanya kazi ya kukomboa watu kwa amri ya Mwenyezi Mungu.
Samia Suluhu aliapa kuitumikia Tanzania na ndicho ninachokifanya, niliapa kulinda nchi, niliapa kujenga utu wa Mtanzania na kuheshimisha utu wa Mtanzania na ndicho nachokifanya, napohakikisha watu wanapata maji safi, watoto wetu wanapata elimu, afya ipo karibu na kila mtu, umeme upo, usalama wa nchi upo ni kuheshimisha utu wa Mtanzania.
Kwa hiyo sina uchungu ndugu zangu wa kubeba matusi yote yanayotolewa kwa sababu nafanya kazi hii sina uchungu wala sijutii, nawaomba sana ndufu zangu wa Ubungo na Kinondoni tunawaomba kura zenu,amesema.
