Hofu yatanda Z’bar

*Walio Tanganyika kugeuka wawekezaji

*Wasiwasi watanda, wanunua ardhi Bara

*Wahoji Tume ya Warioba kufuta Takukuru

Mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya ya kuondoa suala la ardhi katika mambo ya Muungano, yamezaa hofu kwa Wazanzibari wanaoishi Tanzania Bara na ndugu zao walioko Zanzibar.

Hali hii imewafanya wawe na vikao vya dharura na kuanza kufikiria njia bora ya kuhakikisha wanaendelea kuishi Tanganyika bila kuondolewa, baada ya Katiba mpya kupitishwa.

 

Idadi ya Wazanzibari wanaotafuta ardhi upande wa Tanzania Bara (Tanganyika), imeongezeka.

 

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI kwa siku kadhaa tangu rasimu hii itangazwe June 3, 2013, umebaini wakazi wengi wa Visiwa vya Unguja na Pemba wanakwenda katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Mtwara na Lindi kwa ajili ya kununua ardhi.

 

Hali hiyo imeelezwa kuwa inatokana na hofu iliyowaingia ya kukosa ardhi endapo kutaundwa Serikali ya Tanzania Bara na hivyo kuwafanya wananchi wa Zanzibar kukosa haki waliyokuwa nayo tangu mwaka 1964 ya kumiliki ardhi upande wa Tanzania Bara.

 

Kwenye rasimu ya Katiba mpya iliyozinduliwa wiki iliyopita, mambo ya Muungano yamepunguzwa kutoka 22 hadi saba. Mambo hayo ni Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Uraia na Uhamiaji, Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje, Usajili wa Vyama vya Siasa; na Ushuru wa biadhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya Muungano.

 

Baadhi ya watendaji wa mitaa mkoani Dar es Salaam waliozungumza na JAMHURI wamesema siku mbili tangu kutangazwa kwa rasimu, wameshangaa kupata idadi kubwa ya wananchi wenye asili ya Unguja na Pemba wanaotafuta mashamba ya kununua. Viongozi wa Msakuzi na Mpigi Magohe ni miongoni mwa waliokiri kuwapo ongezeko la mahitaji ya mashamba.

 

Kwa miaka zaidi ya 50, Watanzania kutoka Unguja na Pemba wamekuwa wakimiliki ardhi upande wa Bara, lakini wenzao wa Tanzania Bara hawakuruhusiwa kufanya hivyo Visiwani kwa hoja kwamba ardhi ya Zanzibar ni ndogo mno.

 

Endapo yaliyopendekezwa kwenye rasimu yatakubaliwa na baadaye kupitishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hiyo ina maana kwamba Wazanzibari watapaswa kupata haki ya kukodi ardhi upande wa Tanzania Bara kwa sheria zinazotumika sasa kwa wewekezaji wageni kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC).

 

Hatua hiyo inaweza kuwa pigo kwa Wazanzibari wengi ambao wamekuwa na kasi ya kuwekeza upande wa Tanzania Bara, kutokana na urahisi wa kupata ardhi na pia kuendesha biashara mbalimbali.

 

SERIKALI TATU ZACHANGANYA WENGI

Muundo wa Serikali Tatu za Tanzania Bara, Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndiyo uliochukua nafasi kubwa zaidi ya kujadiliwa na wananchi kupitia vyombo vya habari na mitaani.

 

Wakati wananchi wakionesha kufurahishwa na mengi yaliyo kwenye rasimu na kuimwagia sifa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, muundo wa Serikali hizo umeibua sintofahamu miongoni mwa wengi. Wanahoji gharama za uendeshaji Serikali hizo, hasa kwa nchi yenye uchumi usio imara sana kama Tanzania.

 

Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye, ni miongoni mwa waliokosoa utaratibu wa Serikali tatu, akisema unaongeza gharama kwa walipa kodi.

 

Kwenye mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) akiwa nchini Afrika Kusini, Sumaye, pamoja na kupongeza rasimu, alisema muundo wa Serikali tatu utakuwa mzigo mkubwa kwa Watanzania.

 

Alisema ni kwa sababu za gharama za kuendesha Serikali hiyo, waasisi wa Muungano waliona umuhimu wa kuwa na Serikali mbili.

 

Kuwapo kwa Serikali tatu kunamaanisha kuwa Tanzania Bara itapaswa kuwa na kiongozi wake kama ilivyo kwa Zanzibar, kwa jina lolote – Rais au Waziri Mkuu – inapaswa kuwa na Baraza la Mawaziri na muundo wote wa Serikali kwa mambo ambayo si ya Muungano.

 

WANASIASA Z’BAR WAKOMALIA MADARAKA KAMILI

Kauli zinazotolewa na wanasiasa kadhaa wa Zanzibar baada ya kutolewa kwa rasimu ya Katiba Mpya, zinaibua hofu kama Muungano utaendelea kudumu.

 

Viongozi waandamizi wa Chama cha Wananchi (CUF), wamenukuliwa wakisema baada ya kupendekezwa kuwapo kwa Serikali ya Tanzania Bara, sasa ni wakati wa kuhakikisha Zanzibar inapata madaraka kamili.

 

Mjumbe wa Baraza Kuu la CUF na Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu, alitangaza kujiuzulu nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho kwa kile alichokieleza kwamba ni kuongeza nguvu katika kuhakikisha Zanzibar inapata mamlaka kamili.

 

Kauli za Jussa pamoja na Wazanzibari wengine wakiwamo wa kikundi cha Uamsho, zinalenga kuiona Zanzibar ikiwa na mamlaka kamili. Katibu Mkuu wa CUF, ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Maalim Seif Shariff Hamad, ni miongoni mwa wanaoongoza mapambano ya kuiona Zanzibar ikipata kiti katika Umoja wa Mataifa (UN).

 

Pamoja nao, wanatajwa wanachama maarufu na viongozi waandamizi wa SMZ wanaounga mkono msimamo wa CUF na Uamsho. Hata hivyo, inaelezwa kwamba kada ya wananchi wa kawaida wanauona Muungano kama chombo muhimu kwa ajili ya maisha yao na hivyo wanapenda kuona ukiendelea kuimarika.

 

Washangaa Takukuru kufutwa

Hatua ya Tume ya Jaji Warioba kutupilia mbali mapendekezo ya wadau ya kutaka Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) kupewa meno kutupwa, imewaacha wengi wakiwa vinywa wazi.

 

Maafisa wanaofanya kazi katika sekta mbalimbali Serikalini, wamezungumza na JAMHURI kwa sharti la kutotajwa wakilaumu hatua ya Rasimu ya Katiba kuifuta Takukuru na kuiweka chini ya Jeshi la Polisi.

 

“Mhariri wala usishangae. Mpango wa kuifuta Takukuru ni wa siku nyingi. Ilipeleka Ikulu Awamu ya Nne ya Mpango wa Mapambano dhidi ya Rushwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi miezi minane iliyopita, mpango huo umekaliwa.

 

“Wapo wakubwa wamefanya madudu mengi, hivyo wanaona Takukuru ni tishio kwa maslahi yao. Ndiyo maana imewekwa chini ya Jeshi la Polisi. Polisi wamekula kiapo cha kupokea amri, hivyo hawawezi kuwa huru sawa na Takukuru,” alisema Afisa Mwandamizi wa Serikali.

 

Henry Rwekaza Batamuzi, mfanyabiashara na mkazi wa Mlandizi, mkoani Pwani, alisema yeye alipendekeza Takukuru ipewe meno, na sasa anashangaa kuona imewekwa chini ya ibara ya 228 (d) chini ya polisi. “Tukiua Takukuru, tunaipeleka nchi hii katika bwawa la rushwa,” alisema.

 

Chini ya Ofisi ya Rais, Takukuru ilikuwa na uwanda mpana wa kufanya kazi. Hata hivyo, inaelezwa kuwa bado fursa ya Takukuru kuwa ofisi inayojitegemea ipo, kulingana na jinsi Mabaraza na Bunge la Katiba vitakavyofanya kazi kwa ufanisi kudai uwepo wa Takukuru kwenye Katiba Mpya kama chombo huru.

By Jamhuri