• Waziri Mavunde aainisha programu ya MBT
  • Itashirikisha vijana kwa asilimia 100
  • Asilimia 70 ya fedha za migodi ni manunuzi

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Serikali kupitia Wizara ya Madini imeanisha Programu ya Mining for Better Tommorrow ( MBT) itakayo wawezesha vijana kushirikishwa katika sekta ya Madini kwa kujengewa uwezo na kupatiwa mitaji , vifaa na mashine ili wachimbe madini kwa uhakika bila kupoteza mitaji.

Hayo yamebainishwa leo Septemba 28,2023 na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde katika kongamano la Mpango wa Ushirikishwaji Wananchi kwenye Sekta ya Madini (local content) lililofanyika Viwanja vya EPZ Mkoani Geita.

Akielezea kuhusu programu ya MBT , Mhe. Mavunde amesema hivi sasa nguvu kazi kubwa ipo kwa vijana hivyo ni vema vijana wengi wa kitanzania wakishiriki katika sekta ya madini kupitia programu ya MBT ambayo itasimamiwa na Serikali.

Waziri Mavunde amefafanua kuwa MBT itawajengea uwezo vijana kwa kuwapatia mitaji na kuwaunganisha katika Taasisi za fedha , kuwapatia wataalam waliopo katika sekta ili wapate ushauri elekezi katika hatua za Utafutaji , Uchimbaji , Uchenjuaji na Uthaminishaji .

Aidha , Mhe. Mavunde ameongeza kuwa Sheria ya Madini Sura 123 , Kifungu cha 102 kinataka Kampuni za uchimbaji madini kutoa kipaumbele kwa bidhaa na huduma zinazozalishwa na Watanzania.

Amesisitiza kuwa kifungu hicho kinaendana na Matakwa ya Kanuni za Ushirikishwaji ambazo zilitungwa mwaka 2018 na kufanyiwa marekebisho 2019 na 2022.

Akizungumzia kuhusu mpango wa manunuzi kutoka katika migodi mikubwa, Mhe. Mavunde amesema zaidi ya asilimia 70 ya fedha za migodi zinapelekwa katika mpango wa manunuzi, hivyo kuna haja ya kufanya tathmini ni namna gani watanzania watafaidika na fedha hizo.

Kongamano hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Mkuu wa Mkoa wa Geita , Naibu Gavana wa BoT, Mbunge wa Geita Mjini , Mkuu wa Wilaya ya Chunya , Mwenyekiti wa Tume ya Madini , Kamishna wa Madini , Wakuu wa Taasisi za Umma , Viongozi wa Vyama vya Wachimbaji wadogo , Wawakilishi wa Migodi mikubwa na Kati , wadau wa Sekta ya Madini.

Please follow and like us:
Pin Share