Na Andrew Chale, JamhuriMedia, Zanzibar

MKUU wa mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud amewaomba wananchi wa Shehia za Pwanimchangani na Kandwi wanaojihusisha na kilimo cha Mwani kuendelea kuwa na imani na Serikali yao kwani inalifanyia kazi suala lao la mwani kuungua na kukosa soko la uhakika.

RC Ayoub amesema hayo, katika mwendelezo wa ziara yake ya Shehia kwa Shehia inayoendelea ndani ya Mkoa huo, ambapo akiwa Shehia ya Pwanimchangani, amepokea kero mbalimbali ikiwemo kero kubwa ya wakulima wa zao la mwani ambao wamelalamikia kwa mahoteli kutiririsha maji machafu hali inayopelekea mwani wao kuungua huku pia wakikosa soko la uhakika.

Ambapo akijibu kero ya Mwatima Musa Silima wa mkulima wa Mwani la bei za mwani na umwagaji maji machafu kwenye mwani wao, RC Ayoub amesema kuwa umwagaji wa maji unatokana na mahoteli kudhibitiwa na watu wa mazingira wa kutomwaga maji baharini.

“Hoteli zinadhibitiwa umwagaji maji mengi baharini, kuna utafiti uliofanyika umetazama haya yote ya maji na bei ya mwani.

Kwa hiyo tunataraji kuja na utaratibu mkakati wa namna gani bei ya mwani itaongezeka, Serikali upande wake imeunda kamapuni maalum ya kushughulikia mwani ili upande bei hivyo hili linafanyiwa kazi.” Amesema RC Ayoub.

Pia suala la mwani kutoota vizuri baharini linatokana na suala la mabadiliko ya tabia nchi kwa kuwa kikwazo cha wakulima kutopata mwani wa kutosha.

“Tunalo tatizo jingine la Mabadiliko ya tabia nchi, yamekuwa ni kikwazo kwa wakulima kutokupata mwani wa kutosha.

Nini kifanyike, mapendekezo mbalimbali yametolewa ikiwemo baadala ya kuwa maji madogo pekee, wakulima wasogee kwenye maji mengi kidogo ili yasiunguze sana ule mwani, ili mfike huko mnahitaji vifaa ikiwemo mahitaji ya boti ya kufikia huko, Serikali haya yote inafanyia kazi.” amesema RC Ayoub.

Aidha, amemwagiza Sheha wa Pwanimchangani kuitisha kikao cha Wananchi kutatua kero zilizopo chini yake ikiwemo ujenzi holela wa mahoteli kwa kufunga njia pamoja na masuala mengine ikiwemo ukosefu wa ajira kwa vijana katika miradi ya maeneo yao ikiwemo hoteli na shughuli za Kitalii.

By Jamhuri