Wananchi wa Kata ya Njoro Wilayani Kiteto, wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti akizungumza nao,  juu ya kuwachukulia hatua kali wanasiasa wanaosababisha migogoro ya ardhi. 
 Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti akizungumza kwenye Kata ya Njoro Wilayani Kiteto juu ya kuwachukulia hatua kali wanasiasa wanaosababisha migogoro ya ardhi, kushoto ni mbunge wa jimbo hilo Emmanuel Papian na Mkuu wa wilaya hiyo mhandisi Tumaini Magessa.
Wananchi wa Kata ya Njoro Wilayani Kiteto, wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti akizungumza nao,  juu ya kuwachukulia hatua kali wanasiasa wanaosababisha migogoro ya ardhi. 
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti ametoa onyo kali kwa viongozi wa kisiasa wa Wilaya ya Kiteto kuwa atawachukulia hatua kali wote watakaosababisha migogoro ya ardhi kwa wananchi.
Akizungumza kwenye kata ya Njoro, Mnyeti alisema atawachukulia hatua kali wanasiasa hao kwani yeye siyo mkuu wa mkoa wa maboksi anayeogopa kulowanishwa na mvua. Alisema alipata taarifa ya baadhi ya wanasiasa wanaotumia migogoro ya ardhi kwa ajili ya kujinufaisha kisiasa, ila hatawafumbia macho wanasiasa wa aina hiyo waliopo wilayani Kiteto.
“Tumekuwa na migogoro isiyokwisha, wewe una shamba lako kwenye kijiji cha Bwawani kuna mtu anakuzuia kulima hapa Njoro? au ukiishi hapa Njoro kuna mtu amekunyima kununua nyumba kule Kibaya makao makuu ya wilaya?” alihoji Mnyeti. Alisema atawashughulikia wanasiasa hao wanachochea migogoro ya ardhi baina ya watu na watu na kijiji na kijiji ili iwe funzo kwao na hawatasahau kitendo hicho.
“Wanasiasa hao wababaishaji, wanaojaribu kuishika serikali sharubu nitakula nao sahani moja, kwani hatuwezi kukubali hali hiyo ijitokeze na kuacha kuchukua hatua kwao bila kuangalia vyeo vyao,” alisema Mnyeti. Hata hivyo, alimuagiza mkuu wa wilaya ya Kiteto, mhandisi Tumaini Magessa kuhakikisha vijiji vyote vinawekewa alama za mipaka ili kuondokana na migogoro ya ardhi.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto, Lairumbe Mollel ambaye ni diwani wa kata ya Chapakazi ni mmoja kati ya viongozi wanaotajwa kusababisha migogoro hiyo wilayani Kiteto alikana kujihusisha nayo. “Mheshimiwa mkuu wa mkoa afanye uchunguzi wake na atabaini kuwa mimi sihusiki na uchochezi wa migogoro hiyo ya ardhi zaidi ya kuongoza halmashauri yangu ya wilaya kupitia nafasi hii,” alisema Mollel.
Pia, mbunge wa jimbo la Kiteto, Emmanuel Papian ambaye naye anatajwa kuhusika na uchochezi wa migogoro alisema wapinzani wake wa kisiasa ndiyo wanasambaza habari hizo potofu kwani yeye hausiki. Awali, mmoja kati ya wakazi wa Njoro Amina Omary alisema wanasiasa hao wamekuwa mwiba mkali kwao kwani wamekuwa wachonganishi kwa wakulima na wafugaji kwa lengo la kujipatia kura pindi kipindi cha uchaguzi kitakapofika.
Omary alisema wanasiasa hao wamekuwa wanawaunga mkono wafugaji wanaoingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima badala ya kuwakataza ili kuepusha migogoro isiyo kuwa na tija.
Ramadhan Juma alimuomba mkuu huyo wa mkoa kuwachukulia hatua kali wanasiasa hao wababaishaji ili kuepuka kutokea kwa mapigano kama ya miaka iliyopita ambayo ilichochewa nao na kusababisha mauaji.
Please follow and like us:
Pin Share