Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
SERIKALI mkoani Pwani imewahakikishia wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha pamoja na wawekezaji katika Kongani ya Viwanda ya Kwala kuwa Kituo cha Kupoza Umeme cha Mlandizi, chenye njia 21 za umeme, kinatarajiwa kusaidia kutatua changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara ifikapo Novemba 30, mwaka huu.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, ametoa kauli hiyo Oktoba 21, 2026, wakati wa ziara yake ya kikazi katika Halmashauri ya Kibaha, ambapo pia amewataka wamiliki binafsi wa maeneo ya uwekezaji kupunguza gharama za ardhi ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi na kuongeza kasi ya ujenzi wa viwanda.
Nyongo amesema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kuimarisha miundombinu muhimu, ikiwemo umeme, maji na barabara, ili kurahisisha shughuli za uzalishaji na biashara na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi.
Akiwa katika Kongani ya Viwanda ya Kwala, Nyongo amesema atawasilisha kwa mamlaka husika ombi la kujengwa kwa kituo cha reli ya kisasa ya SGR katika eneo hilo ili kuangalia uwezekano wa kutekeleza mradi huo na kurahisisha usafirishaji wa mizigo.
Amesema atazungumza na waziri mwenye dhamana pamoja na mamlaka zinazohusika kuhusu ombi hilo, akieleza kuwa uwepo wa kituo hicho utasaidia kuwezesha makontena kushushwa Kwala na kusafirishwa kwenda maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi, badala ya kutegemea Bandari ya Dar es Salaam pekee.
Kwa mujibu wa Nyongo, hatua hiyo inatarajiwa kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo, kupunguza msongamano wa magari katika barabara kuu ya Chalinze–Morogoro na kuchochea shughuli za kibiashara katika eneo la Kwala.
” Kongani ya Viwanda ya Kwala ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayotarajiwa kuchochea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi imara, jumuishi na wenye ushindani”alifafanua Nyongo.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi wa umeme wa Mlandizi, Mhandisi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Issack Kwina, amesema kituo hicho kimejengwa kwa gharama ya zaidi ya Sh bilioni 16, chini ya mkandarasi TBEA Ltd, kupitia msaada kutoka nchini Ufaransa.
Kwina amesema kituo hicho kimeanza kufanya kazi kwa asilimia 100 tangu Septemba 30, 2026, kikilenga kuimarisha upatikanaji wa umeme katika maeneo ya Kibaha Vijijini, Bagamoyo na Chalinze, hususan maeneo ya viwanda ya Zegereni na Zogowale.
Amesema TANESCO inaendelea kuboresha miundombinu ya umeme kwa tahadhari ya mvua za El Niño, ikiwemo kubadilisha nguzo za zamani na kuweka nguzo za zege ili kuongeza uimara wa miundombinu na kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Kongani ya Viwanda ya Kwala, Barry Chale, amesema eneo hilo linatarajiwa kuchangia mapato ya Sh trilioni 1.2, kutoa fursa za kukuza ujuzi kwa vijana 10,000, kuzalisha ajira za moja kwa moja 50,000 na ajira za mikataba 250,000.
Chale amesema kongani hiyo yenye ukubwa wa ekari 2,500 imepangwa kuwa na uwezo wa kupokea viwanda takribani 200 vya aina mbalimbali, huku uwekezaji huo ukitarajiwa kuchangia Sh trilioni 5 katika Pato la Taifa (GDP).








