RC Ruvuma aagiza kukamatwa wazazi ambao watoto wao hawajaripoti shuleni

Na Albano Midelo,JamhuriMedia, Ruvuma

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amewaagiza wakuu wa Wilaya,wakurugenzi na viongozi ngazi ya kata na vijiji kuwakamata wazazi wote ambao hadi Jumatatu ijayo watakuwa hawajawapeleka watoto wao shule.

Ametoa agizo hilo baada ya kukagua na kubaini mahudhurio hafifu ya wanafunzi katika shule za sekondari Ruhuwiko Wilaya ya Mbinga na sekondari ya Limbu Wilaya ya Nyasa.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Janali Laban Thomas akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari Limbu Halmashauri ya wilaya ya Nyasa ambapo alibaini mahudhurio kwa wanafunzi wanaoanza kidato cha kwanza ni hafifu

Kanali Thomas amesikitishwa na taarifa ya isiyoridhisha ya mahudhurio hasa kwa wanafunzi wanaoanza kidato cha kwanza katika Wilaya hizo.

“Nawaagiza wakuu wa Wilaya zote tano hadi Jumatatu ijayo kama kuna mwanafunzi hajaripoti shuleni,acha kuangaika na mwanafunzi kamata wazazi sukuma ndani tutakwenda kuwachambulia selo”,alisisitiza RC Thomas.

Amesema serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imetekeleza wajibu wake katika Mkoa wa Ruvuma kwa kununua samani na kujenga vyumba 500 vya madarasa kwa gharama ya shilingi bilioni kumi,mwaka 2021.

Amesema Rais Dkt Samia Suluhu Hassan pia mwaka 2022 ametoa shilingi bilioni 3.1  katika Mkoa wa Ruvuma kwa ajili ya kujenga vyumba vya madarasa 156 na kununua samani zake hivyo hakuna kisingizio chochote kwa mzazi kushindwa kumpeleka mtoto wake shule.

wanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Ruhuwiko wilayani Mbinga  ambapo  hadi kufikia Janauri 10 mwaka huu walitakiwa  kuripoti wanafunzi 346 lakini walioripoti ni 65 tu

Awali akitoa taarifa ya mahudhurio ya wanafunzi katika Wilaya za Mbinga na Nyasa Mkuu wa Wilaya ya Mbinga ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Mheshimiwa Aziza Mangosongo amesema kwa ujumla mahudhurio ya wanafunzi wanaoanza kidato cha kwanza sio mazuri.

Ametolea mfano katika Halmashauri ya Mji Mbinga katika shule za sekondari wanafunzi waliopangiwa kuripoti kidato cha kwanza ni 2,722 lakini walioripoti hadi Januari 10,2023 ni  wanafunzi 376 sawa na asilimia 14. 

Kulingana na Mkuu huyo wa Wilaya katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga walipangiwa kuripoti wanafunzi wa kidato cha kwanza 5,171 na walioripoti hadi Januari 10 ni wanafunzi 675 tu sawa na asilimia 14.

Mkuu wa Wilaya ya Mbinga mheshimiwa Aziza Mangosongo akitoa taarifa ya mahudhurio kwa wanafunzi katika wilaya hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas  baada ya kuanza muhula wa masomo

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Mheshimiwa Desderius Haule amesema wamepokea maagizo ya Mkuu wa Mkoa wamejipanga kufanya operesheni ya kuwasaka wanafunzi wote waliochaguliwa kidato cha kwanza kuhakikisha wote wanakwenda kuripoti.

Amesema kwa kushirikiana na madiwani wenzake na viongozi wa serikali katika ngazi ya Halmashauri watahakikisha ndani ya siku saba watoto wote wanaripoti katika shule walizopangiwa.