Na Albano Midelo,JamhuriMedia,Ruvuma

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas ametoa maagizo 20 kwa Halmashauri mbili zilizopata hati zenye mashaka ili ziweze kubadilika na kurejea kwenye hati safi.

Kanali Thomas ametoa maagizo hayo kwa nyakati tofauti katika Halmashauri za Mbinga Mji na Nyasa ambazo zimepata hati zenye mashaka wakati anazungumza kwenye kikao maalum cha Baraza la madiwani cha kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akizungumza kwenye mkutano wa Baraza maalum la kujadili utekelezaji wa hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali CAG kuishia Juni 2022 kwenye ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Nyasa Kilosa Mbambabay.

Maagizo yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ni Pamoja na kufunga hoja zote zilizosalia,kuzuia kujirudia kwa hoja,wakuu wa Idara kushiriki kuandaa kikamilifu majibu ya hoja na Halmashauri kuchukua hatua za kinidhamu mapema kwa watumishi wanaozalisha hoja.

“Hakikisheni taarifa za hesabu za mwisho za mwaka zinaandaliwa kwa kuzingatia matakwa ya viwango vya kihasibu vya kimataifa katika sekta ya umma na Afisa Masuuli uhakikishe unashiriki mwenyewe katika vikao vya wakaguzi’’ amesisitiza.

Maagizo mengine ni kudhibiti upotevu wa mapato katika Halmashauri,marufuku kutumia fedha mbichi,fedha zote zinazokusanywa lazima ziingizwe kwenye mfumo wa mapato na kuwasilishwa benki,kuzingatia sheria za manunuzi na Halmashauri kuendelea kulipa madeni mbalimbali ya wazabuni.

Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa wakiwa kwenye mkutano wa Baraza maalum la kujadili utekelezaji wa hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali CAG

Mkuu wa Mkoa pia ameagiza kufanyika mara kwa mara vikao vya Kamati ya ukaguzi wa Hesabu katika Halmashauri,kufuatilia wadaiwa sugu wa mapato ya Halmashauri,kusimamia kikamilifu mfuko wa Bima ya Afya CHF iliyoboreshwa,kutoa elimu kwa wanufaika wa asilimia kumi na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Mkuu wa Mkoa amesikitishwa na Halmashauri hizo kupata hati zenye mashaka katika matokeo ya ukaguzi ambao ulifanywa na CAG katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30,2022.

Hata hivyo amesema licha ya kupata hati zenye mashaka,mwenendo wa kushughulikia Hoja na Mapendekezo ya CAG katika Halmashauri hizo bado hauridhishi.

Ameuagiza Uongozi wa Halmashauri hizo kuhakikisha kuwa wanakamilisha utekelezaji wa kujibu hoja na mapendekezo yote ya CAG kabla ya Septemba 30,2023.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakurugenzi wa Halmashauri za Mji wa Mbinga na Halmashauri ya Nyasa wameahidi kutekeleza kikamlifu maagizo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa ili kuhakikisha Halmashauri hizo katika ukaguzi ujao wa CAG wanarejea kupata hati safi.

Mkoa wa Ruvuma una Halmashauri nane kati ya hizo Halmashauri sita zimepata hati safi na halmashauri mbili zimepata hati zenye mashaka katika matokeo ya ukaguzi wa CAG uliofanywa katika mwaka wa fedha unaoishia Juni 30,2022.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma Komred Oddo Mwisho akizungumza kwenye mkutano wa Baraza maalumla kujadili utekelezaji wa hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali
baadhi ya madiwani wa Hlmashauri ya Wilaya ya Mbinga Mji wakiwa kwenye mkutano wa Baraza maalum la kujadili utekelezaji wa hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali CAG kwenye ukumbi wa Oddo Mwisho mjini Mbinga

By Jamhuri