Na Cresensia Kapinga,JamhuriMedia,Songea

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Rabani Thomas amewataka Makandarasi wazawa kuonyesha uzalendo wa ufanisi wa kazi pindi wanapopewa kazi za ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwemo za barabara ili waendelee kuaminiwa kupewa kazi zingine.

Wito huo ameutoa wakati akiongoza zoezi la utiaji saini mikataba ya awamu ya pili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara kati ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini(Tarura)na Makandarasi iliosainiwa katika ukumbi wa Manispaa ya Songea Mkoani humo.

Kanali Thomas amesema kuwa kumekuwepo kwa baadhi ya Makandarasi kuleta visingizio pindi wanapoharibu miradi au kuchelewesha kuimaliza jambo ambalo amesema limekuwa likirudisha nyuma jitihada za maendeleo kwa Wananchi.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kanali Laban Thomas akizindua utiaji wa saini mikataba ya ujenzi wa miundombinu ya barabara kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Aidha katika hatua nyingine mkuu huyo amempongeza Meneja wa TARURA mkoani humo Wahabu Nyamzungu kuwa amekuwa akisimamia vema fedha zinazoletwa na Serikali kwaajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara na kupelekea baadhi ya Vijiji ambavyo vilikuwa havifikiki kwa usafiri wa gari kama barabara ya kutoka Njambe na Ndonga kuwa sasa inapitika.

Kwa upande wake Meneja wa TARURA Mkoani humo Wahabu Nyamzungu amesema kuwa fedha ambazo huletwa kwenye mwaka wa fedha tangu 2021 hadi 2023 zimekuwa zikitumika katika ujenzi wa miundombinu ya barabara,madaraja na Vivuko jambo ambalo limefanya maeneo mengi barabara za Wilaya tano na Halmashauri nane ziweze kupitika.

Nyamzungu amesema kuwa mikataba iliosainiwa ni ya awamu ya pili na kuwa ya awamu ya kwanza Makandarasi wapo kwenye sehemu zao za miradi waliopewa (Site)na kuwa miradi hiyo inaendelea vizuri.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kanali Laban Thomas akionesha moja ya vitabu vya mkataba wa ujenzi wa miundombinu ya barabara kwa mwaka wa fedha 2022/2023 afla hiyo fupi imefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea.

Kwa upande wake mmoja wa Makandarasi ambaye amesaini mkataba huo Valence Urio ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya Ovans Construction Limited yenye makao yake Mjini Mbinga ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini kumpa kazi ya kutekeleza miradi mbalimbali ya miundombinu ikiwemo ya barabara na kuwa ataifanya kwa wakati.

By Jamhuri