‘Royal Tour’ kukuza utalii, uwekezaji kimataifa

DAR ES SALAAM

Na Mwalimu Samson Sombi

Desemba 9, mwaka jana Tanzania iliadhimisha miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika ikijivunia mafanikio lukuki baada ya kutawaliwa na wakoloni kwa takriban miaka 75.

Baada ya kupata uhuru mwaka 1961, Tanganyika, kwa sasa Tanzania, imeendelea kutambuliwa na kuheshimika katika mataifa ya Afrika na dunia kwa ujumla kutokana na historia yake nzuri ya kudumisha Amani na umoja huku ikiwa na vivutio vingi vya utalii na mambo mengine ya kitamaduni.

Mmoja wa watu muhimu walioitambulisha nchi yetu kimataifa ni Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kutokana na  juhudi na uzalendo wake katika harakati za kutetea haki na kudai uhuru wa Afrika wakati wote wa ukoloni.

Mwalimu Nyerere, Rais wa Kwanza wa Tanzania, ni miongoni mwa viongozi wa Kiafrika waliowahi kuhudhuria Mkutano wa Umoja wa Mataifa (UN) enzi za utawala wa kibeberu na kudai uhuru wa Tanganyika.

Tanzania pia inatambulishwa duniani na Mlima Kilimanjaro ambao ni mrefu kuliko yote Afrika. Madini ya tanzanite yanayopatikana Tanzania pekee duniani ni alama nyingine inayoiweka nchi katika ramani ya dunia.

Pamoja na mambo mengine, Tanzania inatambulika na kuheshimika duniani kuwa nchi pekee inayotumia Kiswahili kama lugha ya taifa, tofauti na mataifa mengine ambayo hutumia lugha za wakoloni kama lugha za mataifa yao.

Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani zilizojaliwa vivutio vya utalii, ambavyo huipatia nchi fedha za kigeni, kuburudisha na kuendeleza mila, desturi na historia nzuri ya nchi yetu.

Jumanne ya Juni 16, 2020, aliyekuwa Rais, Dk. John Magufuli, alieleza mafanikio katika sekta mbalimbali ikiwamo utalii katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake.

Alisema wamechukua hatua mbalimbali za kukuza sekta ya utalii ikiwamo kuanza utekelezaji wa mpango wa uendelezaji utalii nyanda za kusini, kuanzisha hifadhi mpya tano na kuongeza jitihada za kuvitangaza vivutio tulivyonavyo kimataifa, ikiwamo kuanzisha chaneli maalumu ya utalii ya TBC Taifa.

Aliongeza kwamba serikali imezidisha mapambano dhidi ya ujangili kwa kuanzisha Jeshi Usu, hivyo kusaidia kuongezeka kwa idadi ya wanyama waliokuwa kwenye hatari ya kutoweka kama faru na tembo na kwamba sasa idadi ya faru imeongezeka kutoka 162 mwaka 2015 hadi 190 mwaka 2019 na tembo wameongezeka kutoka 43,330 mwaka 2014 hadi 51,299 mwaka 2019.

Kufuatia hatua hiyo, idadi ya watalii na mapato yameongezeka kwa mfano mwaka 2019 tulipokea watalii 1,510,151 kutoka watalii 1,137,182 mwaka 2015 aidha mapato yaliongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 1.9 mwaka 2015 hadi kufikia dola za Marekani bilioni 2.6 mwaka 2019.

Sekta nyingine inayoonekana kuwa na mchango mkubwa kwenye uchumi wa nchi ni sanaa na utamaduni, kwa mujibu wa taarifa ya hali ya uchumi ya mwaka 2018, shughuli za sanaa na burudani ziliongoza kwa ukuaji mwaka 2018 ambapo ilikua kwa asilimia 13.7 na mwaka 2019 ilishika nafasi ya tatu kwa ukuaji wa asilimia 11.2.

Mbali na vivutio na kazi nzuri za wasanii wetu, kivutio kingine kikubwa ambacho hufanya wageni wengi kuja kutembelea nchi yetu na kujionea maajabu ni amani na utulivu wa nchi yetu.

Tanzania imetajwa kuwa nchi salama duniani kutokana na idadi kubwa ya watalii kutoka nje ya nchi wanavyoongezeka mwaka hadi mwaka. Baraza la Dunia la Utalii limeitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi salama zaidi duniani.

Agosti 2020, aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla, alibainisha hayo wakati wa kuzindua rasmi matumizi ya stempu iliyowekwa nembo ya baraza hilo. Stempu ambayo itabandikwa katika kila tangazo linalohusu utalii wa Tanzania.

Dk. Kigwangalla alibainisha kuwa watalii wengi kabla ya kufanya uamuzi wa kutembelea nchi yoyote huwa wanataka kujihakikishia usalama wa nchi husika kuanzia ulinzi, huduma za chakula, malazi na usafiri.

Nchi yetu imefanikiwa katika hayo ndiyo maana tumepewa stempu hiyo.

“Hakika hii ni hatua kubwa sana na yenye mafanikio kwa nchi yetu. Hii stempu inatuweka katika mazingira shindani zaidi ya utalii na nchi nyingine, tunachotakiwa ni kuendelea kuitunza heshima hii kwa kuhakikisha kuwa zile sababu za kupatiwa stempu hii zinazidi kuimarika,” alisema Dk. Kigwangalla.

Katika hatua nyingine, Agosti 29, mwaka jana, Rais Samia Suluhu Hassan alianza harakati za kutangaza vivutio vya utalii kimataifa, hatua ambayo inaelezwa kuwa kichocheo kikubwa katika sekta hiyo muhimu katika kukuza uchumi na uwekezaji nchini.

Septemba 2, 2021, akizungumza na wananchi wa Tegeta jijini Dar es Salaam, Rais Samia alisema ameamua kurekodi kipindi maarufu cha Royal Tour kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii, uwekezaji, utamaduni na sanaa vilivyopo pembe zote za Bara na Visiwani.

Rais Samia alisema filamu hiyo itakapoonyeshwa huko nje ya nchi mbali na kuitangaza nchi kiutalii, vilevile itawafanya watu wa mataifa kadhaa duniani kutambua Watanzania ni wa aina gani na wanaendeshaje siasa.

Akiambatana na mpiga picha wa Kimarekani na mshindi wa tuzo ya Emmy, Peter Greenberg, Rais Samia amezungukia maeneo yenye vivutio ikiwamo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Mamlaka ya Uhifadhi ya Ngorongoro na mbuga zenye wanyama maarufu nchini.

Rais Samia pia alitembelea machimbo ya madini ya tanzanite huko Mererani, Mlima Kilimanjaro na baadhi ya maeneo maarufu ya vivutio huko Zanzibar. 

Aprili 18 mwaka huu, tasnia ya filamu nchini ilifungua ukurasa mpya baada ya Rais Samia kushiriki uzinduzi wa filamu ya Royal Tour huko Los Angeles Marekani na kutangaza duniani vivutio vya utalii vinavyopatikana nchini na fursa za uwekezaji kwa ujumla.

Baada ya filamu hiyo kuonyeshwa katika ukumbi wa Jumba la Makumbusho la Guggenheimim jijini New York, anaanza kuwakutanisha waigizaji wa Tanzania na kampuni kubwa zilizofanikiwa kwenye masuala ya filamu duniani ikiwamo, Paramount Pictures na AMC ambazo tayari amekutana na wawakilishi wao katika moja ya vikao vyake kwenye Jiji la New York Marekani.

“Naanza kuwa connect (kuwaunganisha) na dunia waigizaji wa dunia. Nilikuwa na kikao kizuri sana na kampuni kubwa tano za utalii hapa Marekani na kwingineko, yalikuwa mazungumzo mazuri na nilikutana na mtu anayefanya kazi na Paramount na AMC, tulikuwa na mazungumzo mazuri ya kuunganisha utamaduni na sanaa ya Tanzania kwao, nipeni muda,” alisema Rais Samia.

Filamu hiyo yenye urefu wa saa moja na dakika 58 inauzwa kwa dola 19.99 za Marekani (sawa na Sh 46,476) na inakodishwa kwa dola 5.99 za Marekani (sawa na Sh 13,925) katika mtandao huo.

Mbali na kukuza uwekezaji, utalii na uchumi wa nchi, filamu hiyo inaendelea kuimarisha uhusiano wa Tanzania na mataifa mengine ikiwamo Marekani.

Ijumaa ya Aprili 15, Rais Samia alikutana na Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Haris, katika Ikulu ya Washington DC na viongozi hao wawili waliahidi kuendelea kuimarisha uhusiano mkubwa kati ya Marekani na Tanzania.

Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala, alisema mazugumzo yao yalihusu zaidi ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

“Utawala wetu una nia ya dhati ya kuimarisha uhusiano na Tanzania na nchi za Afrika kwa ujumla,” alisisitiza Kamala.

Mbali na hiyo Tanzania imesaini mikataba saba ya biashara na kampuni za Kimarekani yenye thamani ya Sh trilioni 11.7 inayotarajiwa kuzalisha ajira 301,110 katika sekta ya kilimo, utalii na biashara.

Rais Samia pia alishuhudia utiaji saini wa hati za makubaliano kwa ajili ya kuanza mazungumzo ya uwekezaji na biashara kati ya kampuni za Marekani na Tanzania.

Mdau wa mazingira wa taasisi ya usimamizi na uendelezaji wa misitu (TaLro) Wilaya ya Kisarawe, Nasra Rashid, amesema hatua ya Rais Samia kutangaza vivutio vya utalii kimataifa kunaiweka nchi katika soko la utalii duniani.

“Rais Samia anaitangaza sekta ya utalii kimataifa, Watanzania tunapaswa kumuunga mkono kwa kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vyetu ili kukuza pato la taifa,” anaeleza Rashid.

Mzee Leonard Mbata wa Songea amesema Rais Samia ameonyesha ubunifu wa hali ya juu, huu ni mfano mzuri wa kuigwa na viongozi wengi serikalini katika kutimiza majukumu yao ya kujenga taifa.                                              

 0755-985966