* Watendaji wadaiwa kutumia jina lake kula rushwa kwa walima bangi

* RPC Tarime/Rorya awaruka, DC asema dawa yao inachemka

Maofisa watendaji wa Kijiji cha Kwisarara na Kata ya Bumera wanatuhumiwa kutumia jina la Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) wa Kipolisi Tarime/Rorya kuchukua rushwa ya fedha kutoka kwa wakulima wa zao haramu la bangi.

Habari zilizopatikana kutoka kwa wakulima wa bangi katika maeneo hayo, zinasema maofisa watendaji hao wamekuwa wakichangisha rushwa hiyo kwa maelezo kwamba wanampelekea RPC ili asitishe mpango wa kwenda kufyeka na kuteketeza mashamba yao.

 

Wakizungumza na JAMHURI wiki iliyopita, wakulima hao ambao wameomba kutotajwa majina kwa sababu za kiusalama, wamesema mtindo huo ndiyo unaotumika kubariki kilimo cha bangi katika maeneo hayo kwa miaka mingi sasa.

 

JAMHURI ilikwenda maeneo hayo kuchunguza ukubwa wa tatizo la wananchi kukodisha ardhi kwa wafanyabiashara raia wa Kenya kwa ajili ya kulima zao la bangi linalosemekana kuwa na soko kubwa nchini humo.

 

Hata hivyo, watendaji hao – Sospeter Malimi wa Kata ya Bumera na Matiko Nyaisurya wa Kijiji cha Kwisarara – walipoulizwa na JAMHURI kuhusu tuhuma za kutumia jina la RPC kuchangisha rushwa ya fedha ili kunusuru mashamba yao kuteketezwa na polisi walikataa kuzungumzia suala hilo kwa maelezo kwamba mwandishi alipaswa kuonana nao kabla ya kuwenda kukutana na wakulima husika.

 

Kwa upande wake, Kamanda Kamugisha alipoulizwa na JAMHURI kuhusu tuhuma za kuwatuma maofisa watendaji hao kuchangisha rushwa hiyo, amekana kupokea fedha yoyote kutoka kwa viongozi hao, huku akiahidi kufuatilia kwa kina suala hilo na kuchukua hatua stahiki.

 

“Hiyo inaweza kuwa ni mbinu tu iliyobuniwa na watendaji hao kwa lengo la kujipatia fedha kutoka kwa wakulima hao, wakiwadanganya kwamba mashamba yao ya bangi hayataharibiwa na Jeshi la Polisi,” amesema RPC Kamugisha.

 

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewele, amesema dawa ya maofisa watendaji hao inachemka, kwani ameshapokea malalamiko dhidi yao yanayowahusisha na vitendo vya rushwa na kubariki kilimo cha bangi katika maeneo yao ya uongozi.

 

“Nitahakikisha suala hilo linafika kwa mwajiri wao [Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime] kwa hatua za kinidhamu na kisheria,” amesema Henjewele.

Please follow and like us:
Pin Share