Albano Midelo,JamhuriMedia, Songea

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas ameyataja mahitaji ya chakula mkoani Ruvuma kwa msimu wa mwaka 2022/2023 ni tani 469,172 na kuufanya Mkoa kuwa na ziada ya chakula tani 787,190.

Mkuu wa Mkoa Ruvuma Kanali Laban Thomas

Hata hivyo amesema chakula ambacho kilizalishwa katika msimu wa mwaka 2021/2022 kinatumika katika msimu huu wa mwaka 2022/2023 ambapo katika mazao ya chakula zilizalishwa tani 1,256,362.

“Mkoa wa Ruvuma ni mzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula na biashara, kwa miaka minne mfululizo mkoa umeendelea kuongoza kitaifa katika uzalishaji wa chakula nchini’’,amesema RC Thomas.

Akizungumzia mazao ya biashara,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ameyataja mazao ya kimkakati yanayowaingizia wakulima kipato kuwa ni zao la kahawa ambapo katika msimu wa mwaka 2021/2022 jumla ya kilo milioni 13.7 ziliuzwa na kuingiza jumla ya shilingi bilioni 97.

mazao ya mahindi ambayo yanazalishwa mkoani Ruvuma na kuufanya Mkoa kuendelea kuwa kapu la Taifa katika uzalishaji wa mazao ya chakula nchini

Mazao mengine ya kimkakati ameyataja kuwa ni zao la ufuta ambalo katika msimu uliopita limewaingizia wakulima shilingi bilioni 23.4,zao la soya limeingiza bilioni sita na zao la mbaazi limeingiza shilingi bilioni 1.3.

Amesema katika msimu ujao wa kilimo Mkoa wa Ruvuma unahitaji mbolea tani 50,280 ambapo hivi sasa usajili wa wakulima kwa ajili ya mbolea ya ruzuku unaendelea na hadi sasa wakulima 216,366 wamejasiliwa kwenye vitabu.

zao la ufuta ambalo limenunuliwa na kuhifadhiwa katika ghala ya Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru TAMCU ambapo katika msimu uliopita zilinunuliwa kilo milioni 7.9 zenye thamani ya shilingi bilioni 23.4
Mbaazi zilizohifadhi wa katika Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru TAMCU ambapo hadi kufikia Agosti 30, mwaka huu ,zimenunuliwa kilo milioni 1.5 zenye thamani ya shilingi bilioni 1.3

By Jamhuri