Na Mwandishi wetu JAMHURI MEDIA,Dar es Salaam.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata watuhumiwa 7 akiwemo raia wa Canada kwa tuhuma za kupanga njama, kumtishia kwa silaha, na baadae kumteka mwanamke aliyefahamika kwa jina la Hani Nooh Hussein (29) Mkazi wa Masaki, Dar es Salaam.

Hiyo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu Mkoa wa Dar es Salaam SACP Muliro Jumanne Murilo Oktoba 30, 2023 Dar Es Salaam.

Amesema, tukio hilo limetokea Oktoba 16, 2023 saa nne asubuhi wakati  Hani Nooh Hussein akiwa anaendesha gari lake namba T.333 CNH Toyota Rav4, ghafla akiwa eneo la Msasani Village ambapo alisimamishwa na sehemu ya kundi la watuhumiwa hao na kuingia ndani ya gari, kumtishia kwa silaha, kumteka na kuelekea maeneo ya Mbezi beach mtaa wa Ujirani ambako Siku  walimshikilia kwa nguvu kwa nne huku wakidai pesa kwa vitisho kwa baba wa mhanga kuwa asipotoa kiasi cha dola za kimarekani milioni 3.5 mtoto wake atapotezewa maisha.

“Jeshi la Polisi mara baada ya kupata taarifa ya tukio hilo lilifanya kazi ya ziada ya ufuatiliaji wa kisayansi na Oktoba 19, 2023 Jeshi hilo lilifanikiwa kumuokoa mhanga kuwakamata watekaji wote wakiwa na gari walilomteka nalo pamoja na silaha iliyotumika Pistol Glock 19 yenye namba za usajili LZB 614 iliyotengenezwa Austria ikiwa na risasi nne”Amesema SACP Muliro

Gari la watuhumiwa

Watuhumiwa waliokamatwa ni Hassan AbusherNur (39) Raia wa Canada mwenye asili ya Somalia, Mkazi wa Msasani, Nathan Lungumisa (27),  Fredick Chahonza (49), Assad Abdurasur (43),Fahad Mussa (32),  Ilfan Saleh (41),  Nicolas Nilay (39).

Jeshi la Polisi limekamilisha upelelezi na leo tarehe 30 Oktoba 2023 watuhumiwa wote watafikishwa mahakama ya Kisutu kwa hatua zaidi za kisheria.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limetoa onyo na kuwa halitosita kuchukua hatua za haraka kwa mtu au kundi lolote linalopanga au kujihusisha na vitendo va kihalifu.

Aidha Jeshi hilo limewaomba wananchi kuendelea kuchukia uhalifu na kutoa taarifa za wahalifu kwa Jeshi la Polisi ili ziweze kufanyiwa kazi haraka kabla ya matukio.