Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto imesema kuwa, kupungua kwa asilimia 19.6 bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2018/19 ikilinganishwa na mwana 2017/18 kunatokana na dhamira ya serikali kutekeleza bajeti hiyo kwa kutumia fedha za ndani ya nchi.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akijibu hoja mbalimbali zilizoibuka ameeleza kuwa, wabunge walishauri serikali ipunguze utegemezi kutoka kwa wafadhili katika kutekeleza bajeti ya afya.

Katika mwaka wa fedha 2017/18, bajeti ya wizara hiyo ilikuwa TZS 1.07 trilioni lakini kwa mwaka 2018/19 imepungua na kufikia TZS 898.3 bilioni.

“Kilichotokea, bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka huu fedha za ndani zimeongezeka kutoka TZS 628 bilioni hadi kufikia TZS 681 bilioni,lakini fedha kutoka kwa wafadhili zimepungua,” alisema Waziri.

Waziri Ummy alisema kuwa, dhamira hiyo inaonsha nia ya Rais Dkt Magufuli kupunguza utegemezi wa wadau wa maendeleo katika kupunguza changamoto za Watanzania.

Alisema kuwa, lengo ni kuona kwa namna gani serikali kwa kujitegemea yenyewe inaweza kutekeleza bajeti yake.

Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii ilieleza kuwa, kupungua huko kwa bajeti ya Wizara ya Afya kwa asilimia 19.6 kunaweza kuathiri utaoji huduma za afya.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Peter Serukamba alisema katika mwaka wa fedha 2017/18, fungu la fedha za maendeleo, wizara ya afya ilitengewa TZS 785 bilioni, lakini hadi kufikia Februari TZS 385.77 bilioni sawa na 49% kilipokelewa na kutekeleza miradi.

Alibainisha kuwa, katika fedha hizo za maendeleo, TZS 336.3 bilioni ni kutoka vyanzo vya ndani na 449.5 ni kutoka vyanzo vya nje.

“Kamati imebaini fedha zilizopokewa kutoka vyanzo vya ndani ni TZS 64.7 bilioni sawa na 19% ya fedha zilizoainishwa. Pia, fedha za nje zilizopokewa ni TZS 321 bilioni sawa na asilimia 71,” alisema Serukamba.

Please follow and like us:
Pin Share