Na Hyasinta Kissima,JamhuriMedia

Naibu Waziri Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini, amewatala Makamanda wa mikoa kuwafutia na kuwanyang’anya leseni madereva hatarishi ambao wamekuwa hawafuatia na kuzingatia sheria za usalama barabarani na kusababisha vifo na ulemavu licha ya elimu ya mara kwa mara ambayo imekuwa ikitolewa na Jeshi la Polisi.

Sagini amezungumza hayo wakati alipowajulia hali baadhi ya majeruhi wa ajali iliyotokea Februari 9,2023 ambayo imesababisha vifo vya watu 12 baada ya basi la abiria la Kampuni ya Frester kugongana uso kwa uso na lori lililokuwa limebeba saruji katika Kijiji cha Silwa Pandambili , barabara kuu ya Dodoma-Morogoro.

Akizungumza na majeruhi wa ajali hiyo ambao 25 waliruhusiwa mara baada ya kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Gairo na kuruhusiwa kuendelea na safari Sagini amewataka wnanachi kuhakikisha wanapaza sauti zao kwa kutoa taarifa pindi wanapoona viashiria vya mwendokasi kwa madereva au wanapoona kusimama kwa safari mara kwa mara kutokana na ubovu wa magari wanayosafiria kwa kupiga namba za simu za Makamanda wa Polisi zilizopo ndani ya mabasi wanayosafiria

“Wadau wa usafirishaji wakiwemo madereva na sisi abiria wote inapaswa tuguswe na mwenendo wa madereva wetu tukatae na tupige kelele. Pale unapoona dereva anaendesha kwa mwendo hatarishi kataeni kwa sababu mkinyamaza na baadhi mkishangilia wakati mwingine mnakwenda kushangilia yanayopelekea mwisho wenu wa maisha.

“Uamuzi wa dereva yule haukuwa uamuzi kabisa wa mtu mwenye akili za kawaida kuyapita magari mawili yote marefu na mbele kuna gari inakuja hii si akili za kawaida tupige kele vitendo vya namna hii vinatumaliza”alisema Sagini.

Sagini amewasihi wananchi wanaotumia vyombo vya usafiri kuwa vyombo hivyo vinamasharti yake kuna viwango vya spidi ya kutembea lakini pia kama unataka kupita gari nyingine lazima uwe na tahadhari ya kutosha kwani dereva aiyesababisha ajali hakuwa na tahadhari ya kutosha.

By Jamhuri