KMeruama kuna mambo yatakayobaki kwenye historia nchi baada ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete, ni kuwapa nafasi wanawake katika vyombo vya uamuzi.

Mbali ya kuteua wakuu wengi wa wilaya, mikoa, majaji ni Rais Kikwete aliyeonekana kuwa na kiu akitaka moja ya nguzo za dola kuongozwa na mwanamke.

Kupitia taratibu mwafaka, Anne Makinda-Mbunge wa Njombe Kusini akateuliwa na chama na kuchaguliwa kuwa Spika la Bunge la 10 linalomaliza kabisa muda wake Oktoba, mwaka huu.

Haikuishia hapo, ushawishi wa Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa CCM taifa, ndio ukamfanya mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli kumteua Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea ambata katika safari ya kwenda Ikulu.

Samia, mahiri katika uongozi kwani licha ya kuongoza vema Wizara ya Muungano chini ya Ofisi ya Makamu Rais na kushika wadhifa wa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, ana mengi anataka kufanya katika wadhifa wake mpya, kama Watanzania watamchagua Dk. Magufuli.

Mwandishi wa Gazeti la JAMHURI amekutana ghafla na Samia jijini Dar es Salaam na bila kusita, mama huyo mwenye umri wa miaka 54 anajibu maswali ya mwandishi kama ifuatavyo:-

JAMHURI: Ulipokeaje uteuzi wa wa mgombea ambata (mwenza)?

SAMIA: Binafsi ni kitu ambacho kilinishtua, lakini kwa vile mimi ni kiongozi ninayejiamini sikupata shida maana natambua wajibu wangu katika nchi yangu. Hivyo naweza.

JAMHURI: Wewe ni mwanamke wa kwanza kuteuliwa kuwania nafasi hii, unaichukuliaje?

SAMIA: Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa hilo, lakini nashukuru kupata fursa hii ambayo itanisadia kuionesha jamii kuwa mwanamke ni binadamu kama walivyo wanaume, hivyo hakuna nafasi ya jinsia moja tu.

Namshukuru Dk. Magufuli na chama wameweza kuniamini na kuamini utendaji kazi wangu, nitatekeleza majukumu yangu ipasavyo na kuhakikisha nchi yangu inazidi kusonga mbele bila kutetereka.

JAMHURI: Umekuwa ukizunguka kufanya kampeni katika mikoa mbalimbali nchini, nini umejifunza katika kipindi hiki?.

SAMIA: Jambo kubwa na la kujivunia ambalo ni vigumu kutoka akilini kwangu ni upendo mkubwa walio nao Watanzania, hakika nchi yetu imebarikiwa kitu kikubwa, umoja, upendo na amani yetu. Ni lazima tujivunie hilo maana kila ninapokwenda nimekuwa nikipata mapokezi makubwa ambayo yananipa faraja ikiwa ni pamoja na watu kutaka kusikia nini nakwenda kuwaambia. Sitawaangusha.

JAMHURI: Umejipangaje kushughulikia kero zinazomkabili mwanamke nchini?

SAMIA: Moja kati ya watu nchini wanafanyakazi zaidi ni wanawake, maana majukumu yake yaanzia ndani ya familia. Katika kampeni zangu nimeweza kushuhudia ni kwa kiasi gani mwanamke anapambana kuyaendesha maisha huku akikumbana na changamoto lukuki.

Jambo la kwanza ni kuhakikisha mwanamke anawezeshwa kutimiza ndoto zake, na kumwezesha mwanamke si kiuchumi tu bali zipo njia nyingi za kumuenzi, njia ya kwanza ni kumuwezesha kwa kumpatia mafunzo maalumu ya kujiamini na ujasiliamali ambao kila mmoja wetu anaweza kufanya kupitia mazingira yake aliyopo.

Wapo wanawake wengi wanafanya biashara, lakini wananyonywa kutokana na wao kutopata fursa ya utambuzi wa thamani ya kile kitu anachokiingiza sokoni. Lakini pia nimeweza kuona na kuumizwa na unyanyasaji unaofanywa na baadhi ya watu wanaotoza kodi ambao hawana huruma na wafanyabiashara ndogondogo wanaorundikiwa mzigo wa utitiri wa kodi.

JAMHURI: Unapoongelea utitiri wa kodi unamaanisha nini hasa katika kodi hizo? Ni kodi za aina gani hasa ambazo unadhani si sahihi kutozwa?

SAMIA: Hakuna Serikali isiyotaka raia wake kulipa kodi, ni wajibu wa kila mmoja wetu kulipa kodi, lakini zipo kodi ambazo zinamuumiza mwananchi wa kipato cha chini. Mimi binafsi naziona kama kodi za kukomoana kutokana na mazingira. Binafsi nikiwa katika kampeni mkoani Kilimanjaro nilipita Rombo, wakati nikiwa kwenye msafara niliwakuta akinamama wamejipanga barabarani wakiwa wamejitwisha mikungu ya ndizi.

Binafsi nilidhani walikuwa wakitoka shamba, lakini nashukuru niliokuwa nao waliweza kusimama na kuzungumza nao na kugundua kuwa kumbe walikuwa pale sokoni wakiningoja waweze kunifikishia kilio chao. Pale ni sokoni, hivyo siku zote wanakwenda kuuza ndizi hapo, na kila wanapokwenda kuuza ndizi wanalazimika kuuza zikiwa kichwani kwao maana wakishusha chini tu, wanatozwa ushuru hivyo wanateseka kwa kubaki na mzigo wa ndizi kichwani mpaka watakapopata wateja. Huu ni unyanyasaji. 

Hizo ndizo kodi zisizofaa, kodi zinazomuumiza Mtanzania. Pia, Halmashauri nyingi nchini zimekuwa zikitoza kodi nyingi zisizofaa hivyo ni lazima kuziondoa zote hizo ili kumpunguzia mwananchi mzigo usiokuwa wa lazima.

Tatizo la namna hiyo nililikuta pia mikoa ya Kusini ambako wanakatwa kodi kutokana na mazao yao, vyama vya ushirika vinawakata wananchi kodi kiasi kwamba mkulima hapati faida kutokana na mazao yake, ni lazima kukomesha tabia hiyo ila kila mmoja afaidike na jasho lake.

JAMHURI: Kumekuwa na tatizo la huduma katika vituo vya afya, zahanati na hata hospitali zetu. Kina mama wanalazwa zaidi ya mmoja kitandani huku wengine wakijikuta wakijifungulia chini. Unazungumziaje suala hilo?.

SAMIA: Suala la huduma bora za matibabu ni muhimu kwa kila binadamu, kila mmoja wetu anahitaji kupatiwa matibabu ya uhakika ili kuokoa maisha yake. Jambo la muhimu kwanza ni kuhakikisha kila hospitali na zahanati kunakuwa na dawa za kutosha hilo linawezekana na litafanyika.

Kuhusiana na wahudumu wa afya na vitendea kazi ikiwa ni pamoja na vitanda, hayo ni mambo muhimu ya kuboresha, tunaweza kuboresha kwa kutumia fedha zetu ambazo zimekuwa zikitumika ndivyo sivyo. Zipo fedha ambazo zimekuwa zikitumika katika matumizi yasiyokuwa ya lazima katika halmashauri zetu, hizo ni kuhakikisha zinaelekezwa huko na changamoto hizo zite zitakuwa zimepatiwa ufumbuzi.

Wote ni mashuhuda, kumekuwa na malipo hewa yanayofanywa, tukitumia fedha hizo ambazo tayari zimeanza kuokolewa. Tutaondokana na kero hizi na utatuzi utakuwa wa kudumu.

Pamoja na kutumia fedha hizo ila ni pamoja na kuhakikisha tunahamasishana kila mmoja wetu kuwa mzalendo na kuthamini kilicho chetu kwa kukitunza na kukilinda kwa maslahi ya wengi.

JAMHURI: Unaridhishwa na shule zetu kukosa madawati na wanafunzi kusoma wakikalia mawe huku wengine wakikaa chini.

SAMIA: Moja kati ya vitu vinavyoniumiza ni hali ya watoto wetu kusoma katika mazingira hayo, si jambo la kujivunia hata, lakini nakuhakikishia ya kuwa miezi 12 ya kwanza ni kuondokana na aibu hii kwa kuhakikisha kila mwanafunzi anakali dawati kama ilivyokuwa hapo awali.

Tunazo raslimali za kutuwezesha kupata madawati ya kutosha, hivyo basi tutazitumia na kuondokana na aibu hii. Mimi kama mama natambua jukumu hili naliweza maana natambua zaidi mwanangu anaposoma katika mazingira magumu nini matokeo yake. Naahidi kulinda mazingira ya kusomea na kuyaboresha kwa kizazi hiki na kijacho.

JAMHURI: Umeoneka  katika kampeni zako ukitoa ahadi nyingi kuhusiana na kupeleka kiasi kikubwa cha fedha vijijini kila mwaka, fedha hizo utazipata wapi?

SAMIA: Wapo watu wananishangaa kwa kutoa ahadi hizo, haya mambo nakuhakikishia kuwa yanawezekana. Haiwezekani nchi za wenzetu waweze siye tushindwe. Ahadi hizo nimezitoa kwa vile natambua kuwa zinatekelezeka, nitasimamia fedha hizo kupelekwa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa ikiwa ni pamoja na kuwafikia walengwa.

Tunaweza kupambana na changamoto ya kupunguza umasikini wetu kwa kuinua wananchi walio vijijini, nchi yetu asilimia kubwa ni ya wakulima ambao wakiwezeshwa vizuri watafikia malengo yao.

JAMHURI: Ni changamoto zipi umekua ukikumbana nazo katika kipindi cha kampeni?

SAMIA: Naweza  kusema kuwa sijakutana na changamoto zaidi ni kuzidi kuifahamu nchi yangu na watu wake. Mimi kama mama nimeweza kuona ni kwa jinsi gani tunaweza kuifanya nchi yetu ikawa zaidi ya hivi ilivyo.

Nimeweza kuona changamoto wanazokumbana nazo wanawake walio wengi wa Mkoa wa Ruvuma, Songea na Tunduru nimeweza kushuhudia kuwa wao ndio wanaotakiwa kujenga nyumba ambazo hata kivyo si imara.

Upande mmoja wapo wanakijiji ambao mwanamke ndiye anayehusika na kujenga nyumba ambayo ni ya tope na juu anaezeka nyasi. Nyasi hizo mwanamke ni lazima akazitafute na kuzileta kuezeka nyumba ambayo hudumu kwa miaka miwili tu, baada ya hapo inaanza kuvuja, hivyo ni kazi ya mwanamke kuhakikisha nyumba haivuji.

Upande mwingine wanawake wamejiunga vikundi vidogo vidogo ambavyo huchanga fedha na kumpati mmoja wao ambaye hutumia fedha hizo kununulia bati za kuezekea, kazi ya kununua bati ni ya mama, baba kazi yake ni kutafuta miti kwa ajili ya kuezekea bati hizo. Hivyo basi mama analo jukumu kubwa mno kuliko baba katika familia nyingi nchini. Unahitaji uwezeshwaji mkubwa ili kukabiliana na majukumu yanayomkabili katika familia na nchi kwa ujumla.

JAMHURI: Unauchukuliaje uchaguzi wa mwaka huu na nafasi ya mwanamke?

SAMIA: Uchaguzi wa mwaka huu una changamoto zake kutokana na kukua kwa demokrasia, lakini natambua ya kuwa wapo wanawake wengi wamejitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, hawana haja ya kuogopa maana wanaweza kuwa viongozi wazuri tu. Jambo la muhimu ni kujiamini na kuamini katika kutenda. Pia inaeleweka wazi kuwa wanawake wengi ndio wapigakura, hivyo nataraji kuona wanawake nchini wakijitokeza kupiga kura na kukichagua Chama Cha Mapinduzi ambacho katu hakiwezi kuwaangusha katika utekelezaji wa ahadi zake.

JAMHURI: Nini kauli yako kwa Watanzania katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi Mkuu?. 

SAMIA: Nawaomba Watanzania watuamini na kutuunga mkono kwa kukichagua Chama Cha Mapinduzi Oktoba 25, 2015. Tunawaomba watupe kazi, tutafanyakazi kama mchwa, tutawatumikia ipasavyo na katu hatutowaangusha.

Natambua ya kuwa watanzania wanahitaji mabadiliko, mabadiliko wanayoyahitaji watayapata kupitia Dk. John Magufuli na Samia Suluhu Hassan. 

Tunatambua kero za Watanzania wote, tutatekeleza ipasavyo majukumu yetu bila kuacha doa. Tutahakikisha tunapambana na urasimu na rushwa ambazo zimekuwa zikipigiwa kelele. Tanzania ni nchi yetu sote kila mmoja wetu anapashwa kunufaika na raslimali zake hivyo ni jukumu letu kuona zikitumika vyema kwa faida yetu sote.

Watanzania watutume nasi tutawatumikia, tupo tayari kuwatumikia kwa moyo mmoja maana tuna dhamira ya kweli ya kuwatumiakia na kuitumikia nchi yetu kwa manufaa ya wote.

Tanzania ni nchi yetu sote hivyo tukipewa ridhaa hiyo tutashirikiana kuhakikisha inazidi kusonga mbele kwa kasi kwa kutumia raslimali zetu tulizobarikiwa nazo.

Nafahamu ni kwa kiasi gani Watanzania wanachukizwa na ubadhirifu wa mali za umma, hilo halina ubishi, tutapambana nalo kufa na kupona. Hatutokuwa na mchezo katika kulinda mali ya umma.

1638 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!