KMeruiongozi wa Kamati ya Wafugaji kutoka Kijiji cha Lumbe, Kata ya Ukumbisiganga, Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora, amepiga kambi jijini Dar es Salaam akililia fidia ya ng’ombe 2,537 waliopotea kwenye ‘Operesheni Tokomeza Ujangili’ iliyofanyika Oktoba 2013.

Wakati wenzake wakirudi nyumbani, kiongozi huyo, Mashili Shija, anasema anapambana kutaka kuonana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ili kupata majibu ya hatima ya mali wakiamini kwamba zimeuzwa na watendaji wa Serikali.

“Tunataka jibu moja tu, nayo ni haki. Je, haki ya kulipwa ng’ombe zetu ipo au hapana,” anasema Shija, ambaye huzungumza kwa upole na unyonge huku akiwaza ng’ombe 285 – mali yake, waliopotea katika Operesheni hiyo.

Kadhalika, Shija anasema Operesheni ilisababisha madhara mengi kwa wananchi ikiwa ni pamoja na watu kuuawa, kujeruhiwa na kuporwa mali mbalimbali kama vile ng’ombe na fedha za wananchi.

Kwa mujibu wa Shija, ambaye yuko Dar es Salaam tangu Julai 11, mwaka huu, kuuzwa kwa ng’ombe 2,537 ‘ndiyo mali inayotugusa’ wananchi wengi kutokana na kushindwa kufanya maisha tangu Oktoba, mwaka juzi.

Shija amepeleka barua kwa Waziri Mkuu Pinda kwa jina lake, lakini majibu aliyopata yanamvunja nguvu, kwani hujibiwa kwamba avute subira na kwamba Serikali inafanyia kazi.

Katika barua hiyo, Shija anasema kuwa kwa sasa wanakutana na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kushindwa kulipa ada kwa watoto wao na kukosa huduma za afya kutokana na kufilisika.

Katika barua hiyo ambayo mwandishi wa habari hizi ameiona, Shija anasema shughuli ya Operesheni Tokomeza ilitokomeza utajiri walioumiliki baada ya kufanyiwa ukatili na udhalilishaji, kutokana na uteswaji ambao ni kinyume cha haki za binadamu uliosababishwa na askari waliohusika.

“Kuna watu walipoteza maisha katika zoezi (shughuli) hili…wengine walipata ulemavu wa viungo pamoja na kupoteza mali. Tumekumbwa na umaskini usiopimika kwa sasa na Serikali ipo,” anasema.

Shija anashangazwa na taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyojiridhisha kwamba wananchi wa eneo hilo walifanyiwa unyama unaowatesa kisaikolojia.

Anasema kwamba hata uchunguzi uliofanywa na Tume ya Majaji watatu iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete chini ya Jaji Ihema, ilijiridhisha kwamba walifanyiwa ushenzi na askari waliotumika katika Operesheni hiyo.

“Tunahoji, nini mwafaka wa jambo letu kwa kuwa wahanga tumejitahidi kufuatilia Ofisi ya Waziri wa Maliasili na Utalii bila mafanikio,” inasema sehemu ya barua hiyo.

“Pia tumefuatilia Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Utawala Bora kumuona Waziri George Mkuchika, naye hana majibu. Pia Wizara ya Mifugo ya Mheshimiwa Titus Kamani, naye hana majibu ya kutoka kwenye Tume ya Rais.

“Bado wananchi tumerudi Ofisi ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, nipo hapa tangu tarehe 10/7/2015 kuomba jitihada za kuonana naye, tukaambiwa yupo mapumzikoni Nkasi, tumesubiri hadi amerudi tukaambiwa ameenda Mbeya, mara Dodoma, mambo yanakuwa magumu,” anasema.

Shija anaamini kwamba Pinda ndiye anayeweza kuwasaidia kwa kuwa ndiyo msimamizi mkuu wa Serikali pamoja na msimamizi wa raia na mali zao.

“Kutokana na kukaa zaidi ya miezi miwili, imelazimika wenzangu kurudi nyumbani. Mimi nimebaki hapa na hali yangu ya maisha ni ngumu kabisa. Ninaumia kimawazo juu ya familia yangu na kupoteza ng’ombe zangu 285,” anasema.

Walioondoka na idadi ya ng’ombe walizopoteza kwenye mabano ni Mjanandege Dotto (320); Midero John (242); Emmanuel Lukalalila (620) wakati Redio Nhumai anadai kupoteza ng’ombe 520.

Wafugaji hao wanadai kuwa wahasibu hao, waliwapiga faini ya Sh. 180,000 kwa ng’ombe mmoja na baada ya kushindwa kulipa mifugo hiyo ilinadiwa kwa bei kati ya Sh 400,000 hadi 700,000 na wao kuachwa na ufukara.

“Kinachouma zaidi ni kwamba wahusika waliouza ng’ombe zetu wapo, tunawaona wanaishi maisha ya kifahari na kiasi cha pesa walizoingiza Benki katika Akaunti Na. 20101000154 tawi la NMB Tabora kwa ng’ombe 2,537. Tunaamini pesa hizo si sahihi, kwani ni kidogo,” anadai.

Wanawataja waliouza ng’ombe hizo kuwa ni Nelson Mujwahuzi ambaye ni Mhasibu wa Mbuga ya Kuhifadhi Wanyamapori – Kijiji cha Lumbe na msaidizi wake, Cleti Nayda, pamoja na dalali Vincent Bulba.

Wakati nayda na Bulba hawakupatikana kuzungumzia sakata hilo, Mujwahuzi ambaye ni maarufu kwa jina la Mombeki, anasema; “Suala hilo nalijua, lakini kwa siku ya leo Jumamosi siwezi kuzungumza chochote kwa sababu siko ofisini.

“Naomba unipigie Jumatatu (jana) nikueleze kwa kina kuhusu suala hili. Leo Jumamosi niko mtaani tu, tafadhali nipigie Jumatatu bwana,” anasema Mujwahuzi.

“Sisi tunaamini Tume ya Rais, iliyohusisha majaji watatu, iliundwa kupitia usimamizi mkuu wa Serikali ambako Pinda ndiye mtendaji mkuu na hivyo tunaamini majibu na mapendekezo yake,” anasema.

“Kwa hiyo, Waziri Mkuu anayo na anajua hatua zote za uamuzi au mapendekezo kuhusu sisi tuliodhulumiwa. Usumbufu tunaoupata katika ufuatiliaji katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Katiba na Sheria, na Wizara ya Mifugo bila majibu hivyo tunategemea msaada wa Pinda,” anasema.

Katika mahojiano hayo, Shija anasema: “Kamwe sitakata tamaa. Lakini tunataka jibu moja tu kutoka kwa Pinda kwamba lini tutalipwa. Sitaondoka Dar es Salaam mpaka nipate jibu.”

Shija anarejea wafugaji wa Monduli, Arusha ambako ng’ombe walikufa kwa ukame na Serikali ikajenga hoja ya kuwalipa, hivyo anahoji: “Inakuwaje kuhusu sisi ambao ng’ombe zetu zimeuzwa kweupe na waliouza wanajulikana?”

Anasema kwamba bajeti yake kwa siku ni Sh. 20,000 ikiwa ni malazi na chakula hivyo kwa kuishi wake kwenye nyumba ya wageni na kujinunulia chakula, hadi sasa ametumia si chini ya Sh. 1,200,000.

Anasema kwamba salamu alizotumiwa na wenzake kutoka Tabora ni kwamba huenda mwaka huu, wakabadili uongozi mara baada ya kuona kwamba Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inashindwa kuwajali.

“Mimi nimepigiwa simu, wakaniuliza umefikia wapi? Nikajibu kwamba nimepewa tena barua wakisema nisubiri. Wakasema aah, dawa yao iwe ni Oktoba 25, mwaka huu, eti wanataka kuchagua upinzani, mimi sikujibu tena, nina imani tutasikilizwa tu,” anasema.

Katibu wa Waziri Mkuu, Haonga alipoulizwa na gazeti hili kuhusu ofisi hiyo kulalamikiwa kuwasumbua wananchi hao, akajibu kwamba, “Kama ulivyowasikia, ni kwamba suala hili linashughulikiwa. Majibu watapata.”

Hata hivyo hakuwa tayari kuelezea kwa nini wanazungushwa kwa kipindi chote wakidai fidia hiyo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Meru alipoulizwa na JAMHURI, kuhusu wizara yake kutofuatilia suala hilo, akajibu haraka “Nimechoka kusikia taarifa za wananchi hao.”

Anasema wamefikisha malalamiko yao kila ofisi hadi kwa Waziri Mkuu, na kuhoji kwamba wanataka, “Suala lao lipo kwa waziri mkuu sasa unataka mimi niwasaidie kitu gani? 

“Hebu zungumza nao, wanaelewa nilichowaambia, na wanafahamu nini cha kufanya kwa mujibu wa barua niliyowaandikia, wafuate maelekezo hayo,” anasema Dk. Meru.

1565 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!