MANCHESTER, ENGLAND - FEBRUARY 25: Romelu Lukaku of Manchester United celebrates scoring their first goal during the Premier League match between Manchester United and Chelsea at Old Trafford on February 25, 2018 in Manchester, England. (Photo by John Peters/Man Utd via Getty Images)

Mshambuliaji wa Klabu ya Manchester United ya Uingereza raia wa Chile, Alexis Sanchez, mwenye umri wa miaka 29, anatajwa kutaka kuachana na klabu hiyo ikiwa ni chini ya mwaka mmoja tu tangu ajiunge nayo akitokea Klabu ya Arsenal.

Septemba mwaka huu Man United ilieleza nia ya kumuuza mshambuliaji huyo iwapo kiwango chake hakitaimarika. Tangu ajiunge na Mashetani Wekundu, Sanchez amekuwa hana kiwango bora ikilinganishwa na alipokuwa chini ya Kocha Arsene Wenger.

Mshambuliaji wa zamani wa Arsenal, Ian Wringt, alinukuliwa akisema kuwa kiwango cha Sanchez hakilingani na malipo yake hapo Manchester United.

Sanchez analipwa kiasi cha Pauni 391,000 kwa wiki, lakini hajaonyesha kiwango cha mchezo wake kama alivyokuwa Arsenal kabla ya kujiunga na United Januari mwaka huu.

Wright, ambaye amewahi kung’ara akiwa na Klabu ya Arsenal amenukuliwa akisema kwamba kama angekuwa mfanyabiashara angetazama hali ilivyo halafu aanze kupanga ni wachezaji gani atawauza.

Kauli hii ilitolewa kutokana na mshahara anaolipwa Sanchez ikilinganishwa na mchango wake kwenye timu.

Sanchez alionyesha mchezo mzuri alipoingia kuichezea United katika mechi ya FA Cup dhidi ya Yeovil mwezi Januari mwaka huu, lakini hadi kufikia sasa amekuwa na mchanganyiko wa viwango vya mchezo wake akifunga mabao matatu pekee katika mechi 23.

Wright amebainisha kuwa iwapo United imemlipa fedha hizo, kitu cha kwanza kufikiria ingekuwa ni vipi wanaweza kuzirudisha fedha hizo.

“Sanchez atalazimika kupunguza kiwango chake cha mshahara wa kila wiki iwapo atahamia klabu nyingine. Hakuna mtu anayeweza kumlipa fedha anazopata kutokana na kiwango chake kuwa chini,” amesema Wright.

Wright hakubaliani kabisa na kiwango cha Sanchez ambapo amesema kwamba hafai kuchezeshwa katika timu wakati unapokuwa na Martial na Marcus Rashford.

“Unapomtazama akiichezea Man United, ana uhuru wote na kiwango chake cha mchezo kilitakiwa kuimarika ili kuwa na haki ya kuchezeshwa,” ameongeza Wright.

Mshambuliaji wa zamani wa Blackburn na mshambuliaji wa zamani wa Chelsea, Chris Sutton, amesema kuwa Sanchez amepotea na hana motisha tena.

Sutton amesema: “Sanchez ni kana kwamba anabeba uzani wa dunia nzima katika mabega yake, wakati anacheza Arsenal alicheza na uhuru mwingi na furaha, kwa sasa sioni kiwango kama hicho.”

Mwaka jana Man United walijinasibu kuwa katika nafasi nzuri ya kumnunua Sanchez kutoka Klabu yake ya Arsenal, dhamira ambayo hata hivyo waliitimiza Januari mwaka huu.

Hii ni baada ya kuibuka kwamba wako tayari kulipa Pauni milion 35 ambazo Arsenal walikuwa wakitaka kulipwa ili kumruhusu aondoke London.

Hii ilikuwa baada ya kumwacha nje ya kikosi ambacho kilicheza mechi ambayo Arsenal walilazwa 2-1 na Bournemouth katika ligi ya kuu ya nchini humo (EPL).

Kabla ya kwenda Man United, Sanchez alitaka sana kwenda kwa majirani zao Manchester City lakini alitatizwa na dau lililotolewa na United.

Mwaka jana Klabu ya Arsenal ilikataa Pauni milioni 50 kutoka kwa Manchester City ili kumuuza Sanchez.

Raia huyo wa Chile aliongezewa mkataba wa kuendelea kuichezea klabu hiyo baada ya kuiwakilisha nchi yake katika michuano ya dunia ya Shirikisho nchini Urusi.

Sanchez akiwa na miaka 28, aliifungia Arsenal mabao 24 na alibainisha kuwa angependa kwenda kuichezea Klabu ya Manchester City inayofunzwa na Pep Guardiola.

Sanchez aliwakasirisha mashabiki wa Arsenal baada ya kuonekana akitabasamu wakati klabu yake ikifungwa.

By Jamhuri