Nahodha wa zamani wa Klabu ya Arsenal na mchezaji wa klabu za Juventus, Barcelona, Red Bulls ya New York pamoja na timu ya taifa ya Ufaransa, Thierry Henry, ameteuliwa kuwa kocha mkuu wa Klabu ya AS Monaco inayoshiriki Ligi Kuu ya Ufaransa.

Henry ameajiriwa kwa mkataba wa miaka mitatu utakaokwisha mwaka 2021 na anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Leonardo Jardim aliyefukuzwa kazi baada ya AS Monaco kufanya vibaya katika Ligi Kuu ya Ufaransa, maarufu kama Ligue1.

Wakati timu inakabidhiwa kwa Henry, ilikuwa katika nafasi ya tatu kutoka mkiani mwa ligi, mpaka wikiendi iliyopita AS Monaco ilikuwa inashika mkia, yaani nafasi ya 20 kati ya timu 20 zinazoshiriki Ligue 1, ikiwa na alama saba tu.

Henry ambaye amekuwa mshindi wa Kombe la Dunia 1998 akiwa na timu ya taifa ya Ufaransa na mshindi wa UEFA Champions League akiwa na Barcelona, amekabidhiwa kibarua kigumu kuhakikisha timu yake ya utotoni haishuki daraja.

Mshambuliaji huyo wa kihistoria wa ‘Washika Bunduki’ wa Jiji la London, kabla ya kujiunga na AS Monaco alikuwa msaidizi wa Kocha Roberto Martinez katika kikosi cha timu ya taifa ya Ubelgiji.

Kocha Jardim atakumbukwa na AS Monaco kwa kuwapatia ubingwa wa Ligue 1 katika msimu wa 2016/2017 na kuwaduwaza wababe wa ligi hiyo, matajiri kutoka jijini Paris, Paris Saint Germain (PSG).

Klabu hiyo ilitangaza kwamba Henry mwenye umri wa miaka 41 atakuwa meneja mpya wa timu hiyo kwa vipindi vitatu hadi mwezi Juni 2021.

“Kwanza kabisa ningependa kuishukuru Monaco kwa kunipa nafasi ya kuifundisha timu ya mpira ya klabu hii ambayo kwangu mimi ni muhimu sana,” alisema Henry kupitia mtandao wa klabu hiyo.

“Nina furaha kubwa sana kurudi Monaco na nipo tayari kukabiliana na chochote kitakachokuja mbele yangu, nina hamasa kubwa ya kukutana na wachezaji ili tuanze kufanya kazi pamoja,” aliongeza Henry.

“Ujuzi alionao kuhusu mpira wa miguu, mapenzi yake kwa mchezo, viwango vyake vya hali ya juu na ahadi zake kwa timu yetu vimetufanya tuweze kumteua,” alisema Makamu wa Rais na Mkurugenzi wa AS Monaco, Vadim Vasilyev.

Vasilyev alisema anatambua kwamba Thierry Henry anafahamu ugumu wa kazi ya ukocha, lakini amekiri kwamba Henry ana shauku na kazi hiyo.

Henry ametikisa nyavu mara 356 katika michezo 771 aliyoingia uwanjani. Mchezeji huyu wa kimataifa wa Ufaransa alikuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa la Ubelgiji mwaka 2016.

Kocha wa timu ya Nice inayoshiriki Ligi Kuu ya Ufaransa, Patrick Vieira, ameipongeza Klabu ya AS Monaco kwa kumteua Henry kuwa kocha wake mpya.

Vieira alisema anamfahamu vema Henry, amecheza naye katika timu ya taifa na Klabu ya Arsenal, ni mtu makini, mwenye malengo na msimamo na asiyekubali kushindwa.

“Ninawapongeza AS Monaco kwa kumuamini na kumpa jukumu la ukocha Henry, naamini atawafanyia mazuri na kuirejesha timu hiyo kwenye ushindani,” alisema.

Vieira alimsifia Henry akisema amepata uzoefu wa kutosha baada ya kufanya kazi akiwa kocha wa kikosi cha vijana cha Arsenal na baadaye kuwa Kocha Msaidizi wa timu ya taifa ya Ubelgiji kwa miaka miwili akimsaidia Martinez.

Vieira alisema Henry aliyecheza soka kwa kiwango cha juu anaweza kuhamishia mafanikio hayo pia katika ukocha kama alivyofanya kiungo mwingine nyota wa zamani wa Ufaransa, Zinedine Zidane.

Akiwa kocha wa Klabu ya AS Monaco, Henry ameiongoza klabu hiyo katika michezo mitatu, ambapo wamepoteza michezo miwili ya ligi na kutoka sare mchezo mmoja. Michezo hiyo ni Strabourg 2 -Monaco 1; Monaco 2 – Dijon 2 pamoja na Reims 1 – Monaco 0. Mechi ijayo ya Novemba 11, Monaco itacheza na vinara wa ligi hiyo PSG.

Please follow and like us:
Pin Share