Mashabiki na wapenzi wa Chelsea wanashindwa kumuelewa Kocha wa timu yao, Mtaliano Maurizio Sarri (Garimoshi), kutokana na timu hiyo kushindwa kufanya vizuri katika mechi zake za hivi karibuni.

Chelsea imeanza kusuasua katika mzunguko huu wa pili wa ligi katika mechi dhidi ya Arsenal, Bournemouth na Manchester City, ambapo matokeo ya mechi hizo yamewazindua mashabiki na kukosa imani na Sarri, huku tetesi zikizagaa kuhusu kiungo wa zamani wa Chelsea, Frank Lampard na Zinedine Zidane kurithi mikoba yake.

Kabla ya ujio wa Sarri kwenye Klabu ya Chelsea, watangulizi wake walikuwa wakitumia mfumo wa kujilinda kuliko kushambulia, lakini mmiliki wa klabu hiyo, Roman Abramovich, alikuwa anahitaji kocha atakayekuja na falsafa tofauti.

Kibopa huyo alihitaji kuona Chelsea ikishambulia zaidi na kupata matokeo bora, ndiyo maana baada ya Kocha Muitaliano, Antonio Conte, alifungishwa virago mapema tu baada ya msimu wa 2017/2018 kumalizika. Kabla ya ujio wa Sarri, tetesi zilionyesha kwamba rada za Chelsea zilikuwa zikimwinda aliyekuwa kocha wa Barcelona, Luis Enrique.

Haikuwa bahati ya Enrique kufika London kuifundisha Chelsea, badala yake jina la Maurizio Sarri, ndilo likatajwa kama mrithi wa Antonio Conte. Sarri ambaye alikuwa anaifundisha Napoli ya Italia, bado anahitaji kupambana kuiweka Chelsea kwenye chati ambayo wanaitarajia huku akipambana kubaki ‘top four’ ili acheze Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Magumu anayoyapitia Sarri si mageni kwa makocha wageni katika Ligi Kuu ya Uingereza, hata Pep Guardiola alikaribishwa kwa vipigo vya kutosha katika msimu wake wa kwanza wa 2016/2017, Jurgen Klop naye akaonja shubiri ya Ligi Kuu ya Uingereza.

Lakini hivi sasa timu zao zimejengeka na zina uhakika wa kupata matokeo mazuri katika mechi yoyote dhidi ya wapinzani wao, kwa maana hiyo katika falsafa aliyonayo Sarri bado ataendelea kuwepo ndani ya Klabu ya Chelsea.

Tatizo kubwa ambalo linawakabili Chelsea ni safu ya kiungo, ambapo Joginho anaonekana bado hajazoea mikiki ya ligi ya Uingereza, kwani anaonekana kushindwa kupokonya mipira kutoka kwa viungo wa timu pinzani, hali inayosababisha kushambuliwa wakati wote, huku mashabiki wakimlalamikia kocha kumchezesha kiungo wao, Ngolo Kante, kama kiungo mshambuliaji badala ya kiungo mkabaji.

Kukosekana kwa mshambuliaji mzuri kumekuwa pia tatizo ndani ya Klabu ya Chelsea. Tangu kuondoka kwa Diego Costa timu hiyo bado imekuwa na washambuliaji butu, licha ya uwepo wa Olivier Giroud bado amekuwa si mchezaji anayetumia nafasi vizuri.

Ujio wa mshambuliaji mwenye uzoefu, Gonzalo Higuain, ambaye wamemsajili katika dirisha dogo akitokea Klabu ya AC Milan ya Italia, pengine utaweza kuisaidia Chelsea kupata matokeo mazuri.

Katika hali hiyo, Sarri, bado ataendelea kuinoa Chelsea, maana muda ambao amekaa na timu hiyo ni mfupi. Hata hivyo ikumbukwe kwamba mmiliki wa Chelsea, Roman Abramovich, huwa hana uvumilivu linapokuja suala la timu kutopata matokeo mazuri.

Sarri ameiongoza vema timu yake katika mashindano ya Europa baada ya kufuzu hatua ya makundi bila kupoteza mechi yoyote. Vilevile katika hatua ya mtoano walishinda magoli 2-1 dhidi ya timu ya  Malmo.

Please follow and like us:
Pin Share