Wiki iliyopita timu ya Simba imeendelea kula viporo vyake vema katika mechi zake baada ya kuilaza timu ya Azam kwa magoli 3-1 katika Uwanja wa Taifa.

Simba ilipata magoli hayo kupitia kwa Meddie Kagere aliyefunga magoli mawili huku jingine likifungwa na John Bocco, na lile la kufutia machozi la Azam likifungwa na Frank Domayo, hivyo kujiongezea nafasi ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ushindi huo wa Simba umekuwa wa tatu mfululizo katika ligi kuu, baada ya hivi karibuni kuzifunga timu kadhaa katika mwendelezo wa ‘kula’ viporo vyake. Licha ya kuwafunga Azam, Simba alimfunga mtani wake wa jadi Yanga na baadaye African Lyon.

Wiki iliyopita mashabiki wa Yanga walijawa furaha baada ya timu yao kuifunga timu ya Mbao magoli 2-1 katika Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza. Ushindi huo umeiwezesha Yanga kuvunja mwiko wa kutowafunga Mbao katika Uwanja wa CCM Kirumba kwa miaka mitatu mfululizo.

Timu ya Azam nayo inazidi kujipunguzia nafasi ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kutofanya vizuri katika mechi zake nne mfululizo, ambapo katika mechi hizo haijashinda mechi yoyote zaidi ya kufungwa mechi mbili na kutoka suluhu mechi mbili.

Hali hiyo inaifanya Azam kusalia na alama 50 katika mechi 25 ilizocheza, huku ikiwa inashika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo.

Nafasi ya kwanza katika ligi hiyo inashikiliwa na timu ya Yanga ambayo imecheza mechi 25, huku ikiwa na alama 61, nafasi ya tatu ipo timu ya Simba, ikiwa na alama 45, ikiwa imecheza mechi 18, huku ikiwa na michezo saba mkononi.

Ukiachana na Yanga, Azam na Simba kushika nafasi tatu za juu, timu za Singida United, Biashara United na African Lyon zinashika mkia katika ligi hiyo.

Ligi Kuu Bara msimu huu imekuwa na ushindani mkubwa kutokana na idadi ya timu kuongezeka, ambapo ligi hiyo msimu huu inajumuisha timu 20, tofauti na ilivyokuwa misimu iliyopita zilikuwa timu 18.

Vilevile timu zilizokuwa zinafanya vizuri kama Mtibwa Sugar na Kagera Sugar zimekuwa hazina ushindani mkubwa msimu huu.

Katika ligi kuu msimu huu, timu kama KMC, Alliance na Lipuli zimerudi kwa kasi katika mzunguko wa pili wa ligi hiyo kutokana na kuwa na mfululizo wa ushindi kwa siku za hivi karibuni.

Kimsingi ligi kuu msimu huu imekuwa ngumu sana ukilinganisha na misimu mingine, kwa sababu wakati ligi inakaribia kuanza wadau wengi wa soka waliamini ligi ya msimu huu ingekosa ushindani kutokana na kukosa mdhamini kutokana na aliyekuwa mdhamini wa ligi hiyo Kampuni ya Vodacom kujitoa.

Aliyekuwa mchezaji wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni, akizungumzia hali ya Simba anasema kuwa timu hiyo usajili wake ni tofauti na wapinzani wake, na hadhani kama kuna timu inayoweza kuisimamisha Simba  hasa katika safu ya ushambuliaji kwa kuwa ina uchu wa magoli.

Kibadeni amebainisha kuwa Simba ikicheza viporo vyake vizuri ina nafasi kubwa ya kutetea ubingwa wake.

Kuhusu mwendelezo wa ligi hiyo, Simba leo itachuana na timu ya Lipuli katika Uwanja wa Samora, mkoani Iringa, mtanange unaotazamiwa kuwa wa kukata na shoka kutokana na timu hizo kuwa na upinzani mkali pindi zinapokutana, ambapo katika mechi ya mwisho zilitoka sare ya goli 1-1 katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam mwaka jana.

Please follow and like us:
Pin Share