Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Pwani

Serikali imezitaka halmashauri nchini kuendelea kuboresha miundombinu sanjari na kutenga maeneo rafiki kwa uwekezaji na wawekezaji ili kuifikia azma ya serikali kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uwekezaji.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe amesema hayo wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani wakati akizindua kiwanda cha Fortune ambacho ni chakwanza kwa ukanda wa Nchi za Kusini Mwa Jangwa la Sahara, kinachozalisha saruji nyeupe kwa ajili ya ujenzi chenye uwezo wa kuzalisha tani 200 Kwa siku.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe akizindua kiwanda cha Fortune

“Kuwekeza nchini Tanzania ni sehemu salama na yenye mazingira yaliyoboreshwa ambayo kila mwekezani ataweza kunufaika na wananchi nao kunufaika,” amesema Kigahe na kuongeza kuwa uwekezaji huo ni sehemu ya kupunguzwa umaskini na kukuza uchumi wa nchi.

Amesema serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji hususani kupitia sekta ya viwanda Ili viweze kuchangia katika kuongeza fursa mbalimbali nchini, ikiwemo ajira, fedha za kigeni ili kuchangia kukuza uchumi wa nchi.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe

Amesema serikali itashirikiana kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa katika kiwanda hicho zinavuka mipaka ya nchi na kufika hata katika soko huru la Afrika.

“Kiwanda hicho mbali ya kuongeza thamani ya uzalishaji lakini pia ni sehemu ya kuitangaza Tanzania,” amesisitiza Kigahe.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho, Prem Ahuja amesema kiwanda hicho cha saruji nyeupe kinasimama kama ushuhuda wa dhamira ya ubunifu wa ubora na uendelevu ni ahadi ya fursa kubwa kutokana na kuboresha utoaji wa bidhaa zetu za ujenzi.
Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha Fortune, Prem Ahuja akielezea kazi zinazofanywa na kiwanda hicho ikiwemo uzalishaji wa saruji nyeupe

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Khadija Nasri amesema uwekezaji huo ni heshima na imetokana na kuwepo Kwa mazingira mazuri ya uwekezaji.

Amesema Wilaya ya Mkuranga ina viwanda 123 na inajivunia kwa kuwa na mazingira wezeshi kwa wawekezaji.