Katika enzi hizi,miongoni mwa viongozi wanaoendela kushangaza dunia kwa uamuzi na matamshi yake ni pamoja na Rais Donald Trump wa Marekani. Na siyo kwa masuala hasi pekee.

Trump amekuwa rais wa kwanza wa Marekani kukaa meza moja ya majadiliano na kiongozi wa Korea ya Kaskazini, baada ya kukutana na kiongozi wa Korea Kim Jong-un jijini Singapore Juni, mwaka huu.

Hata kama mazungumzo yao hayatabadilisha uhasama uliyodumu kwa muda mrefu kati ya nchi hizo, ni suala la kihistoria na limetokea kwa uamuzi wa Kim na Trump.

Lakini yuko yule Trump mwingine, ambaye hutushangaza kila kukicha kwa matamshi na uamuzi wake hasi. Hivi karibuni tumesikia taarifa kuwa ametumia mabavu ya serikali yake kuandama nchi zinazoegemea kutetea matumizi ya maziwa ya mama badala ya vyakula mbadala kama maziwa ya unga.

Trump mwenyewe amekanusha ukweli wa taarifa hii, ingawa taarifa nyingine zinaelekea kuunga mkono ukweli wa taarifa za awali.

Taarifa za awali zimetoka kwenye kikao cha wawakilishi wa serikali mbalimbali pamoja na wadau wa afya kinachoandaliwa kila mwaka na Shirika la Afya Duniani (WHO) la Umoja wa Mataifa (UN) kilichofanyika Geneva mwezi Mei, mwaka huu kujadili masuala kadhaa juu ya sera za afya.

Kwenye kikao hicho, Ecuador ilijiandaa kuwasilisha pendekezo la kuendeleza sera zilizopo, zinazosisitiza matumizi ya maziwa ya mama kwa watoto wachanga. Kwenye pendekezo lake, Ecuador ilitaka kusisitiza kuongezeka kwa udhibiti wa matumizi ya bidhaa mbadala. Ilichokuwa ikijaribu kufanya hakikuwa jambo jipya ila kukumbushana tu yale ambayo jumuiya ya kimataifa kupitia WHO imekuwa ikifanya kwa miongo kadhaa katika kulinda maslahi ya mama na mtoto.

Kilichojitokeza ni kushuhudia nguvu ya Marekani kutetea maslahi ya wazalishaji wa bidhaa mbadala. Wajumbe wa kikao cha Geneva walishangazwa na uamuzi wa wawakilishi wa Ecuador kusitisha mchakato wa kuwasilisha pendekezo bila kutoa sababu. Ni baadaye tu mwakilishi mmoja alidokeza kuwa serikali ya Marekani ilitishia nchi hiyo kuondoa misaada ya kijeshi na hatua ambazo zingeathiri biashara kati ya Ecuador na Marekani.

Jitihada za jumuiya ya kimataifa kulinda maslahi ya mama na mtoto hazikuanza leo. Mwaka 1981, kwa kutambua kushuka kwa matumizi ya maziwa ya mama na kupanda kwa matumizi ya bidhaa mbadala, WHO liliandaa kanuni za kimataifa kusimamia jinsi kampuni zinazozalisha maziwa ya unga zinavyoshawishi, kupitia matangazo ya biashara, kununuliwa kwa bidhaa zao.

Kanuni zilisisitiza kuwa matangazo ya kampuni hizi yasitumike kushawishi kina mama kuacha kuwanyonyesha watoto kwa sababu ya kutambua kuwa maziwa ya mama kwa mtoto yana manufaa mengi na makubwa kwa mtoto na hayana mbadala.

Wanaotetea kutumika vyakula mbadala kwa mtoto wanadai kutetea kina mama ambao wangependa kutumia njia hizo mbadala. Lakini inaeleweka wazi kuwa wanaotetewa hapa si kina mama na uhuru wao wa kuchagua walishe nini watoto wao, ila ni watengenezaji wa hizo bidhaa mbadala. Ni suala la maslahi ya kiuchumi na nguvu ya serikali ya Marekani kushinda kuzingatia busara.

Itikadi inayoshinikiza kwamba wafanyabiashara, pamoja na masoko wanayotawala, wana uwezo mkubwa na wa ajabu wa kupanga matumizi ya rasilimali kuliko serikali na kuliko watu wengine ndani ya jamii ambao siyo wafanyabiashara ndiyo sababu inayojitokeza kuelezea shinikizo hili la Marekani.

Ni itikadi ambayo haitaki kabisa mamlaka ya aina yoyote kudhibiti mienendo ya masoko kwa madhumuni ya kulinda na kutetea maslahi ya wale wanaoweza kuathiriwa na mienendo hiyo mibovu. Waumini wa itikadi hii wanasisitiza kuwa haihitaji kusimamia na kudhibiti masoko kwa sababu ya uwezo mkubwa wa masoko kujisimamia yenyewe na kurekebisha kasoro zinazoweza kujitokeza.

Ni itikadi inayoamini kuwa waliofanikiwa kwenye biashara wamefanikiwa kwa sababu ya uwezo wao mkubwa wa ubunifu, akili, na kupanga mikakati inayoleta mafanikio. Kama ambavyo kwenye mbuga ya Serengeti simba atabakia kuwa simba, na nyumbu atabaki kuwa nyumbu; basi hali kadhalika waumini wa itikadi hii wanasisitiza kuwa jamii inapaswa kuyakubali na kuupokea bila kuuingilia huo uhusiano wa hayo makundi mawili ndani ya jamii ya wafanyabiashara na wasio wafanyabiashara.

Wajibu wa kundi la wafanyabiashara, kwa mujibu wa itikadi hii, ni kuhakikisha wanatumia nafasi yao muhimu ndani ya jamii kuchukua uamuzi sahihi ili shughuli zao zisiathiri maslahi ya wanajamii wengine.

Hiyo ni nadharia, lakini tunashuhudia kuwa hali halisi iko tofauti. Pamoja na kwamba dhana ya kuacha masoko yajiendeshe yenyewe ni hali inayomlemea mnyonge, bado tunashuhudia wazalishaji wenye nguvu tayari ya kutawala masoko wanapata utetezi wa ziada wa serikali ya Marekani kufuta jitihada zozote za kuathiri maslahi yao na badala yake kutishia kuathiri maslahi ya mama na mtoto.

Wakati wa kampeni za kugombea urais, Trump alijinadi kama mfanyabiashara ambaye mafanikio yake kwenye biashara yanampa uwezo na uzoefu mkubwa wa kuongoza nchi yake. Haishangazi kuwa anatumia nafasi na nguvu yake ya kisiasa kutetea maslahi ya wafanyabiashara.

Kwa hali ilivyo ni sahihi zaidi kusema kuwa mfumo wa masoko una watetezi wenye nguvu kubwa ya kisiasa na kiuchumi kuliko ilivyo kwa wale wanaoathirika na uendeshaji mbovu wa mfumo huo.

Kundi dogo la watu na serikali zilizokuwa na nguvu kubwa ya kushawishi zimetwaa jukumu la kusimamia kuchukua uamuzi kwa ajili ya wote na kuna kila dalili kuwa wanachukua uamuzi ambao unanufaisha wachache na kuwaumiza na kuwaangamiza wengi.

 

.tamatiā€¦

Please follow and like us:
Pin Share