Dar es Salaam

Na Joe Beda Rupia

Simba ni mmoja wa wanyama wakali sana. Si sahihi hata kidogo na ni hatari sana kumchezea au kumfanyia masihara mnyama huyu mla nyama.

‘Kuchezea sharubu za simba’ ni hatari. Au tuseme haiwezekani kabisa! Lakini wapo watu wanajaribu kuchezea sharubu za Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Nyakoro Sirro.

Sirro ndiye ‘polisi namba moja’ nchini. Kwa nini kuchezea sharubu zake?

Kwa miaka kadhaa sasa, Jeshi la Polisi nchini kupitia Kitengo cha Usalama Barabarani chini ya usimamizi wa ‘polisi namba moja’, kimefanikiwa sana kupunguza ajali za barabarani.

Naam! Awali ilikuwa ukimsindikiza ndugu yako anayeondoka Stendi ya Ubungo kwenda mkoani, unakosa amani kabisa.

Kila ukiona simu yake, unajiuliza; ‘kuna usalama huko?’

Ajali zilikuwa nyingi, tena zinazoua nusu ya basi na hata basi zima. Sisi tuliokuwa tukiripoti taarifa hizi na kuzifuatilia, tunafahamu kwamba mbali na watu wanaokufa kwenye eneo la tukio, wapo wengine wanaokufa miaka hata mitatu baadaye kutokana na madhara ya ajali waliyopata.

Familia zinauguza hadi wanandugu wanakosana! Kuuguza ni kazi eti. Kuuguza, hasa kwa muda mrefu kunahitaji upendo wa dhati. Si kila mtu mwenye uwezo wa kuuguza ndugu yake kwa miezi minne, mitano hadi sita mfululizo! Miaka miwili je?

Unakwenda Muhimbili kila siku hadi walinzi wanakuwa marafiki zako; wapishi wa migahawa yote unafahamiana nao, achilia mbali madaktari na manesi!

Kuuguza kunahitaji ‘commitment’ (majitoleo) ya ajabu ambayo ni wachache sana wanayo. 

IGP Sirro analifahamu hili na ndiyo maana Jeshi la Polisi likaamua kuweka mikakati kabambe kuhakisha Watanzania hawapotezi rasilimali zao kwa ujinga na uzembe wa watu wachache barabarani. Polisi wamedhibiti ajali na lazima tuwapongeze.

Ni bahati mbaya kwamba wapo madereva watano au sita hivi wa kampuni za mabasi za Sauli na New Force wanaodharau na kupuuza jitihada hizo.

Mabasi ya kampuni hizi mbili yanayofanya safari zake kati ya Tunduma, Mbeya na Dar es Salaam kwa sasa ndiyo pekee ambayo hayajali kabisa ‘mwendokasi elekezi’ barabarani.

Madereva hao wamekuwa wakishindana ni nani atakayewahi kufika kituo fulani! Wanakimbizana kuanzia Tunduma hadi Dar es Salaam! 

Imefika hatua hadi wapigadebe kwenye vituo vya mabasi ‘wanabeti’ ni nani kati ya Sauli na New Force atakayewahi kufika! 

Siku moja askari wa Iringa walimkamata dereva wa Sauli kwa maelekezo ya askari mmoja (nadhani ni mkubwa) aliyekuwamo kwenye basi hilo lililokuwa likitokea Tunduma; kwamba mwendo aliokuwa akienda nao (kilomita 100 na zaidi kwa saa) ulikuwa ni wa hatari kubwa.

Wakamshusha na basi likaendelea na safari baada ya kupatikana dereva mwingine pale Iringa. Dereva huyo ‘mpya’ akaendesha kwa mwendo elekezi (kilomita 80 kwa saa) vizuri kabisa.

Lakini baada ya kupokea simu kadhaa (nadhani ni kutoka kwa dereva aliyeshushwa Iringa), akabadilika. Kuanzia Kitonga akaanza kuendesha kwa kilomita 40 kwa saa! Eti anatukomoa abiria.

Basi likaingia Ubungo saa 4:30 usiku badala ya walau saa mbili! Watu tupo hoi. Bahati nzuri yule jamaa ambaye nina uhakika ni askari, hakumuacha. Akamkamata na kwenda naye kituoni.

Hii maana yake nini? Kiburi. Madereva wa Sauli na New Force (si wote) wana kiburi na sijui ni nani anayewalinda!

Hofu yangu ni kwamba, ikitokea siku moja (Mungu apishe mbali) moja kati ya mabasi haya likapata ajali, yale majanga ambayo tumeanza kuyasahau, yatarejea kwa kishindo.

Kwa nini hili litokee? Kwa nini vijana hawa waruhusiwe au waachiwe kuchezea sharubu za Afande Sirro?

Hapana. Usipoziba ufa utajenga ukuta. Ni lazima wamiliki wa Sauli na New Force waelezwe wazi kuwa mwendo wa baadhi ya madereva wao unaashiria misiba kwa Watanzania.

Jukumu hili ni la Kitengo cha Usalama Barabarani. Afande Mossy Ndozero asikubali sharubu za bosi wake IGP Sirro zichezewe hivi hivi. Aende kuwatembelea na baada ya kuwapa elimu ya umuhimu wa kuzingatia maelekezo ya usalama barabarani; awaonye, kisha kuanza kufuatilia mienendo yao barabarani.

0679 336 491

By Jamhuri