Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Mkoa wa Dodoma una zaidi ya mizinga 18,000 ya nyuki yenye uwezo wa kuzalisha zaidi ya kilo 135,000 za asali kiwango ambacho kinatajwa kuwa bado ni kidogo ikilinganishwa na fursa za ufugaji nyuki zilizopo mbapo zaidi ya hekta milioni 1,038,193 za misitu imehifadhiwa na zinaweza kutumika kwenye shughuli za ufugaji nyuki.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule ameeleza hayo leo Mei 18,2025 Jijini Dodoma kwenye ufunguzi wa maadhimisho ya kitaifa ya siku ya Nyuki duniani ambapo ameeleza kuwa shughuli za ufugaji nyuki zinaweza kufanyika katika maeneo ya kilimo na kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo kupitia huduma ya uchavushaji.

Amesema,rasilimali zilizopo kwenye mkoa endapo zikitumika vizuri zitawezesha kuzalisha zaidi ya kilo milioni 7,000,000 za asali na kuongeza kipato cha kaya pamoja na taifa na kuwataka wananchi wa mkoa wa Dodoma kuchangamkia fursa hiyo na kufanya shughuli za ufugaji nyuki ili kujiongezea kipato.

“Dunia nzima huadhimisha Siku ya Nyuki, lengo ni kutambua mchango wa Sekta ya Nyuki katika maisha ya mwananchi mmoja mmoja, Taifa na Dunia kwa ujumla,siku hii ni sehemu ya kuenzi jitihada za mwanzilishi wa ufugaji Nyuki Bwana Anton Jana raia katika nchi ya Slovenia ambapo nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ziliidhinisha na kutangaza rasmi tarehe 20 Mei ya kila mwaka kuwa siku ya Nyuki Duniani itakayoadhimishwa na kila nchi mwanachama wa Umoja huo, “ameeleza

Ameeleza kuwa maadhimisho hayo yanatoa fursa kwa wafugaji nyuki, wajasiriamali na wafanyabiashara wa mazao ya nyuki na wadau wengine wa sekta ya Ufugaji Nyuki kukutana kwa lengo la kujengeana uwezo wa namna bora ya kuendeleza Sekta ya Nyuki katika Mkoa wa Dodoma na nchi kwa ujumla.

Sambamba na hayo ameeleza kuwa Sekta ya nyuki bado inakabiliwa na changamoto zinazotishia uendelevu wake na hivyo kuhatarisha upatikanaji wa mazao ya nyuki kwa siku zijazo.

Amezitaja Changamoto hizo kuwa ni pamoja na matumizi ya dawa za kuua wadudu kwenye kilimo, uchomaji moto misitu, kubadilisha maeneo ya ardhi ya misitu kwa matumizi mengine, kuongezeka kwa kasi ya mabadiliko ya tabia nchi ambayo yanaambatana na mabadiliko ya hewa na mazingira rafiki kwa nyuki kuzalisha mazao yao.

“Ni wazi kuwa Mkoa wa Dodoma na Mikoa mingine bado tuna nafasi ya kuhifadhi misitu katika ardhi za Vijiji, misitu ya Halmashauri, misitu ya Serikali kuu na hifadhi za wanyamapori. Hatuna njia ya mkato ambayo itawezesha uendelevu wa mazao ya nyuki sambamba na huduma za mdudu nyuki kwenye mimea zaidi ya kumlinda na kuhifadhi mazingira yake, “amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki Deusdedit Bwayo amengumzia sekta hiyo kuwa ni fursa hususani Nyuki wasiodunga na kwamba wananchi wanapaswa kujivunia maendeleo ya sekta hiyo kwa kutafakari kuhusu uendelevu wake.

” Hii ni fursa kwa wananchi wote, wafugaji nyuki, wauzaji na wachavushaji wa mazao kwa kutumia makundi ya nyuki,kaulimbiu ya maadhimisho haya kitaifa ni Nyuki kwa Afya na Maendeleo#APIMONDIA 2027 Tanzania ipo Tayari,inatukumbusha mchango wa mdudu nyuki katika afya zetu kutokana na matumizi ya mazao mengi anayozalisha pamoja na kujipatia kipato kupitia mazao hayo, “amesema.

Maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani hiashimishwa kila mwaka fikapo Mei 17 na kuhitimishwa Mei 20 ambapo hutoa nafasi kwa wadau kubadilishana mawazo juu ya uboreshaji wa Sekta ya Nyuki na kupata nafasi ya kujenga uelewa wa pamoja..

By Jamhuri