DAR ES SALAAM

Na Christopher Msekena

Mwishoni mwa wiki jijini Dodoma lilifanyika tamasha kubwa la Serengeti, lililofanikiwa kukata kiu ya mashabiki na wapenzi wa Bongo Fleva kwa siku mbili mfululizo (Jumamosi na Jumapili).

Tamasha hilo limefanyika katika msimu wa pili baada ya mwaka jana kufanyika kwa mafanikio makubwa jijini Dar es Salaam na kushuhudia wasanii zaidi ya 100 kwenye jukwaa moja.

Safari hii Serengeti Festival limefanyika kwenye viwanja vya Chinangali huku mashabiki wakishuhudia burudani ya wasanii zaidi ya 200 kwenye jukwaa moja kuanzia Jumamosi mpaka Jumapili.

Huu ni mwendelezo wa serikali chini ya Wizara ya Sanaa na Michezo kuhakikisha tasnia ya burudani inaendelea kuwa hai kwa uwepo wa matamasha makubwa ili kutoa fursa za ajira kwa wasanii huku ikiwapa burudani na raha mashabiki.

Ukiangalia mwaka uliopita ambapo Serengeti Festival lilifanyika kwa mara ya kwanza, wengi walidhani ni nguvu ya soda lakini kadri muda unavyokwenda unaweza kuona uthubutu wa Serikali katika kuandaa tamasha hili linaloonyesha kukua kila msimu unapofika.

Miaka michache nyuma kabla ya uwepo wa Serengeti Festival kulikuwa na taasisi mbalimbali binafsi zinazoandaa matamasha ya muziki na yalikuwa yanashindana kwa ukubwa wake.

Matamasha kama Fiesta, Muziki Mnene, Wasafi Festival ni miongoni mwa majukwaa yaliyosifika zaidi kwa kuwatengenezea wasanii ujira pamoja na kuwapa fursa mashabiki kushuhudia burudani.

Ushindani wa matamasha hayo ulionyesha wazi jinsi tasnia ya burudani inavyokua huku ukionyesha kuwapo kwa ombwe la wawekezaji wengine kwenye tasnia ili tuwe na matamasha mengi zaidi.

Na macho yalikuwa yanalitazama Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kufanya jambo litakaloleta mchango wa moja kwa moja kwenye tasnia na hapo ndipo mawazo ya Serengeti Festival yalipoanzia, hatimaye sasa linafanyika kwa mafanikio.

Kutokana na ukuaji wa kasi wa tasnia ya muziki, tumekuwa tukihitaji uwepo wa matamasha mengi ambayo yatatoa fursa kwa wasanii mbalimbali kushiriki, mashabiki kupata burudani na kupitia majukwaa hayo kutangaza vivutio vyetu vya utalii na mambo mengine yanayopatikana Tanzania.

Kwa hiyo ujio wa Serengeti Festival umeleta taswira mpya ya muziki wa Bongo Fleva. Tamasha hilo limevunja mipaka ambayo matamasha mengine yamekuwa nayo.

Mfano ni kawaida kuona wasanii fulani wakipata nafasi ya kutumbuiza kwenye tamasha fulani lakini hawapati nafasi ya kutumbuiza kwenye matamasha mengine yaliyoandaliwa na taasisi binafsi kwa sababu tu za kibiashara.

Ila sasa ukifuatilia Serengeti Festival utabaini hakuna matabaka. Wasanii wote wanapata nafasi ya kutumbuiza kwenye jukwaa hilo bila kujali ukubwa au udogo wa msanii mhusika.

Hali kadhalika unaweza kuona mashabiki wakipata nafasi ya kushuhudia wasanii wengi kwenye jukwaa moja kwa siku mbili mfululizo, tofauti na matamasha mengi ambayo yamekuwa yakifanyika siku moja na kunakuwa na wasanii wachache.

Huku jambo jingine zuri likiwa ni kuwaona washereheshaji wa tamasha hilo ni watangazaji nyota kwenye tasnia ya burudani kutoka vyombo vya habari vyenye ushindani wa kibiashara.

Lakini Serengeti Festival imeweza kuwakutanisha pamoja na wamefanya kazi nzuri kwa kushirikiana, jambo ambalo hauwezi kuliona kwenye matamasha yanayoandaliwa na taasisi binafsi.

Bila shaka Serengeti Festival licha ya uchanga wake, imeonyesha sura na mwelekeo mpya wa tasnia ya muziki nchini tofauti na ilivyozoelekea kwenye matamasha mengi.

Hivyo niipongeze serikali kwa kuweka nguvu zake katika tamasha la Serengeti ambalo linatarajiwa kuwa tegemeo kwa wasanii, ukizingatia taasisi nyingi miaka ya hivi karibuni zimekuwa zikiahirisha matamasha yake.

Ndiyo maana unaona wasanii wenye uwezo wamekuwa mstari wa mbele kuandaa matamasha yao binafsi. Wasanii kama Nandy na Mandy Festival au Harmonize na Afro East Carnival ni mfano tu wa mastaa walioamua kuandaa matamasha yao na kuacha kutegemea matamasha ya taasisi.

Serengeti Festival ni jukwaa lililokuja muda mwafaka na sasa ni kazi ya wasanii kuchangamkia fursa pamoja na mashabiki kujitokeza kushuhudia burudani za wasanii ili kuunga mkono jitihada za serikali katika kuinua tasnia ya muziki nchini.

By Jamhuri