Na Bashir Yakub

Nimemsikia Mwenyekiti wa Chama cha Dermokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, akisema kuwa hakutaka kufutiwa mashitaka bali alitaka kesi ifike mpaka mwisho (yaani hukumu).

Yawezekana anasema hivyo kutokana na sababu ya tafsiri halisi ya kufutiwa kwake mashitaka. 

Kisheria ukifutiwa mashitaka kwa ‘Nolle Prosequi’ chini ya Kifungu cha 91(1)CPA kama alivyofutiwa Mbowe, sheria inaruhusu kukamatwa tena hapo hapo au siku za baadaye na kushitakiwa tena upya kwa makosa yale yale.

Hii ni tofauti na pale kesi inaposikilizwa mpaka mwisho na Mahakama ikatoa hukumu ya hatia au ya kuachiwa huru kwa mshitakiwa husika.

Kesi ikifikia hatua hiyo na kumalizika, basi huwezi tena kukamatwa au kushitakiwa tena kwa makosa yale yale (autrefois acquittal & autrefois convict).

Kufutiwa mashitaka kwa staili hii tafsiri yake si kwamba hauna hatia, bali ni kwamba kwa muda huo wanaokushitaki (yaani serikali), wameamua tu kutoendelea na kesi ila wakiamua tena muda wowote, saa yoyote wanarudi kukushitaki.

Pengine hili ndilo limemfanya Mbowe aseme hakutaka afutiwe mashitaka bali alitaka kesi iende mpaka hukumu/mwisho.

Pia kufutwa mashitaka kwa mtindo huu hutumika kisiasa kumnyamazisha mtu (blackmail).  

Kila ukifukuta utatishiwa kurudishiwa mashitaka yako, au tu wewe mwenyewe kila ukitaka kung’aka utakuwa una hofu kuwa unaweza kurudishiwa mashitaka yako, hivyo unajikuta ukiwa mpole. 

Kwa ufupi kufutiwa mashitaka kwa mtindo huu hakuleti raha ya kudumu, amani ya nafsi, na uhuru wa kweli kwa aliyefutiwa kama ambavyo ingekuwa iwapo kesi ingekuwa imefika mwisho na hatima yako ikatangazwa na mahakama.

Hii ndiyo tafsiri halisi ya kufutwa mashitaka ya Freeman Aikael Mbowe.

By Jamhuri