Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Serikali hutenga shilingi milioni 250 kwa ajili ya wahudumia wajasiriamali wadogo nchini bila malipo yoyote kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Hayo yamebainishwa leo Aprii 15,2024 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dk Athumani Ngenya wakati wa kikao kazi na wahariri wakiwemo waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Dk Ngenya amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuwainua kiuchumi wajasiriamali wadogo kwa kuwawezesha bidhaa zao zipate ubora na kuuzika ndani na nje ya nchi.

“Rais Samia amedhamiria kuwaleta pamoja wajasiriamli na kwa sasa mjasiriamali asikuambie lolote kwamba TBS sijui kuna nini, hapana kuna funds ambazo mheshimiwa Rais Samia amezitoa na zipo kila mwaka kwa ajili ya kuwasaidia wajasiriamali wadogo hivyo ni jukumu lao kuwasiliana na nasi.

“Kwa hatua hiyo inaonesha mheshimiwa Rais wetu anaangalia mpaka mjasiriamali mdogo ili aweze kuwezeshwa bidhaa yake ipate ubora na hadi kufikia level (kiwango) cha kupata alama ya ubora,” amesema mkurugenzi huyo.

Ameongeza kuwa kuwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki wana makubaliano kwamba, bidhaa yoyote ikitoka nchi fulani ikiwa na alama ya viwango inaruhusiwa kuingia nchi nyingine bila kufanyiwa vipimo nchi husika.

Amesema, hatua hiyo inampa mjasiriamali husika nafasi ya kupata soko pana katika ukanda wa Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

“Nichukue nafasi hii kwenu wanahabari hizi taarifa ziwafikie wajasiriamali ambao wanatamani bidhaa zao ziwe na alama ya ubora ziweze kuuzika kwa urahisi ndani na nje ya nchi, tuwaeleze waje TBS funds zipo, Mheshimiwa Rais katoa funds sisi tutafuata taratibu zote kuanzia kwenda kuangalia sehemu yake anapozalishia, na kumsaidia kama haijakaa vizuri, tunamsaidia kumwelekeza.

“Haitoshi, baada ya kuzalisha tutakwenda kuchukua sampuli yake bila malipo, tutakuja nayo maabara, itafanyiwa uchunguzi bila malipo, itapewa alama ya ubora bila malipo na baadaye ana miaka mitatu, bure kabisa kuweza kupata huduma za TBS.

“Na baada ya kupata alama ya ubora tunakuja mara mbili kwenye eneo lako la uzalishaji kuweza kuchukua sampuli kuhakikisha kwamba unaendelea na taratibu zile tulizokubaliana mwanzo wakati tunakupa ile lama ya ubora,”amefafanua Dkt. Ngenya.

Dk Ngenya amesema kuwa mafanikio ya shirika hilo ndani ya miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ni mengi mojawapo ni kusogeza huduma karibu na wananchi.

“Kama mnavyofahamu huko nyuma miaka kama mitano, TBS ilikuwa iko tu makao makuu Dar es Salaam pale Ubungo, lakini taratibu sasa tumeweza kusogeza maana Tanzania ni kubwa, kuweka TBS hapa wakati inahitajika kule Kigoma haikuwa sahihi.

“Lakini, kadri muda unavyokwenda tunaweza kuona namna ya kuweza kujirekebisha, kwa hiyo kati ya mafanikio katika kutekeleza hayo majukumu ni hili.

“Tunajenga maabara katika mikoa ya kimkakati, katika hili shirika linatekeleza mradi wa makao makuu ya shirika wa maabara Viwango House pale Dodoma. Dodoma ni makao makuu ya nchi na ni mkoa wa kimkakati. Tumeamua kusogeza huduma, lakini kutakuwa na maabara katika jengo Viwango House kama jina la taasisi lenye lilivyo” ameongeza.

Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema, maabara hiyo itahudumia mikoa mitatu kwa maana ya Dodoma, Singida na Tabora.”Itahudumia pamoja na mikoa mingine ya jirani pale kwa mfano Iringa.”

Pia, amesema shirika hilo linatarajia kujenga maabara nyingine Kanda ya Ziwa ambayo itajengwa jijini Mwanza na nyingine jijini Arusha kwa Kanda ya Kaskazini.

“Maabara ya Kanda ya Ziwa inatarajiwa kuhudumia mikoa sita, Mkoa wa Mwanza wenyewe, Kagera, Mara, Geita, Shinyanga na Simiyu.

“Mnafahamu mikoa ya kule ina mazao mengi sana, lakini pia ina biashara kubwa sana, kwa hiyo baada ya kujenga kwa mkoa wa kimkakati Dodoma makao makuu ambao umefikia asilimia 60 tunaendelea na ujenzi Mwanza ili kuweza kuhudumia Kanda ya Ziwa.”

Amesema, kwa kufanya hivyo si tu kwamba watakuwa wamesogeza huduma karibu kwa wananchi bali kuwapunguzia wananchi wenye bidhaa zao gharama za kufika Dar es Salaam kuhudumiwa.

Kwa upande wa maabara ambayo inatarajiwa kujengwa hivi karibuni Arusha amesema, itahudumia Arusha yenyewe, Manyara, Kilimanjaro na Tanga.”Na kiwanja pale tayari tumeshapata, bado ujenzi upo kwenye karatasi.”

Shirika limefanikiwa kusogeza huduma karibu na wananchi kupitia ofisi zake saba za kanda ikiwemo ya Kaskazini ambapo makao makuu yapo Arusha.Kanda ya Kusini makao makuu Mtwara, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini makao makuu Mbeya, Kanda ya Magharibi makao makuu Kigoma.

”Kanda ya Ziwa makao makuu Mwanza, Kanda ya Kati makao makuu Dodoma, Kanda ya Mashariki kwa maana ya mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro” amesema.

Amesema, TBS ilianzishwa mwaka 1975 kwa juhudi za Serikali kama jitihada za kuimarisha miundombinu ya sekta ya viwanda na biashara ili kukuza uchumi wa Taifa.Kwa hiyo, shirika liliundwa kama miundombinu ya sekta ya viwanda na biashara ili kukuza uchumi wa Taifa hili.

Jukumu kuu la TBS wakati inaundwa ilikuwa ni kuratibu uandaaji wa viwango,lakini baadaye waliongezewa jukumu la kusimamia utekelezaji wa hivyo viwango.

Hivyo wanawajibika kutoa mafunzo kwa wenye viwanda na wazalishaji na utoaji wa huduma bora kwa kuzingatia viwango na kuvifanyia ugenzi vifaa vya vipimo.

Please follow and like us:
Pin Share