Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,Dodoma

Katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano, kwa kuzingatia awamu zote zilizopita na hii inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali inaendelea kutekeleza jitihada za kuzuia na kupambana na rushwa ili wananchi waweze kupata huduma bora.

Akiongea na waandishi wa habari leo Aprili 15,2024 jijini hapa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa umma na Utawala Bora George Simbachawene amesema kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) ziumeunda timu ya uratibu ya kitaifa yenye Wajumbe kutoka Chama cha Skauti Tanzania (CST) ili kuimarisha ushirikiano katika jitihada za kupambana na rushwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema ushirikiano huu ni muhimu kwa ustawi wa Taifa kwa kuwa Skauti wapo katika kundi la vijana na ni Jeshi kubwa Katika kutoa mchango chanya katika matukio mbalimbali ya kijamii na kitaifa na kwamba kupitia ushirikiano huo, wameelimishwa kuhusu madhara na jinsi ya kuzuia na kupambana na rushwa ili wakaelimishe vijana wenzao na jamii kwa jumla katika maeneo yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Wakati huo huo Simbachaweze akizungumzia mafanikio ya mpango wa kunisuru Kaya Masikini( TASAF) kwa miaka 60 kuwa umekuwa na manufaa makubwa hususani kwenye eneo la Uhawilishaji wa Ruzuku kwa Walengwa ambapo kiasi cha Shilingi bilioni 824.4 kililipwa kwa Kaya Maskini 1,321,098 Tanzania Bara na Shilingi bilioni 41.2 ililipwa kwa Kaya Maskini 50,818 Zanzibar ili kuziwezesha kumudu gharama za msingi za maisha na kupeleka watoto wao shule na kliniki.

Amesema TASAF iliandaa Mpango wa Miradi ya kutoa Ajira ya muda kwa Kaya za Walengwa ili kuongeza kipato kwa kushiriki kufanya kazi katika miradi iliyoibuliwa na jamii kwa kulipwa ujira ambapo Tanzania Bara miradi 27,161 ya muda iliibuliwa na kutekelezwa katika Vijiji/Mitaa 9,891 huku Walengwa 626,620 walipata ajira ya muda na kulipwa kiasi cha shilingi bilioni 110.4, wakati Unguja na Pemba katika shehia 244 miradi 702 iliibuliwa na kutekelezwa na Walengwa 35,754 ambao walilipwa ujira wa kiasi cha shilingi bilioni 13.2.

Amesema serikali ya Awamu ya Sita na awamu zilizopita zinazoongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) zote zimekuwa na malengo kabambe ya kupunguza na kuondoa umaskini wa kipato ili nchi iwe na maendeleo tunayoyatarajia.

Waziri huyo amesema Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ulianzishwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2000 kama mojawapo ya mikakati ya Serikali katika kupambana na umaskini kwa kutumia dhana ya ushirikishaji jamii.

Amesema,Madhumuni ya kuanzishwa kwake ilikuwa pia ni kusaidiana na taasisi zingine za Serikali ili kupambana na umaskini wa wananchi wake katika maeneo ya Vijijini na pembezoni mwa Miji ambapo TASAF imetekelezwa katika Awamu Tatu tangu kuanzishwa kwake hadi sasa.

Ameeleza TASAF imekuwa ikitekelezwa kwa awamu tangu kuanzishwa kwake Awamu ya Kwanza ya TASAF ilianza mwaka 2000 2005 na ilijumuisha maeneo ya utekelezaji 42 ambapo 40 ni ya Tanzania Bara na mawili (2) ya Zanzibar (Unguja na Pemba).

“Jumla ya miradi 1,704 ya huduma za jamii yenye thamani ya shilingi bilioni 72 ilitekelezwa kupitia mpango huu wa TASAF I. Awamu hii ilitekelezwa kwa mafanikio makubwa katika kuwapatia wananchi huduma muhimu za kijamii katika sekta mbalimbali zikiwemo za maji, elimu, miundombinu na afya, “.

Na kuongeza”Awamu ya Pili ya TASAF ilianza utekelezaji mwaka 2005 hadi 2013 Ili kuendeleza mafaniko yaliyopatikana katika Awamu ya Kwanza kwenye maeneo mengine ambapo Awamu hii ilitekelezwa katika Halmashauri zote za Tanzania Bara na wilaya zote za Tanzania Zanzibar.

Amesema Jumla ya miradi 12,347 ya huduma za jamii yenye thamani ya shilingi bilioni 430 ilitekelezwa wakati wa Awamu hii ya Pili ya TASAF (TASAF II).

” Katika kipindi cha utekelezaji wa TASAF Awamu ya Kwanza na ya Pili, wananchi walishiriki vyema kutekeleza miradi mbali mbali iliyoboresha upatikanaji wa huduma za jamii ,Mbali na miradi ya kuboresha miundombinu kama vile barabara, maji, masoko, huduma za afya, elimu, ustawi wa jamii na mazingira, wananchi katika makundi mbali mbali walitekeleza miradi ya kuongeza kipato ambayo iliwasaidia kukabiliana na umaskini, ” Amesema

Aidha amesema awamu ya Tatu ilianza kutekelezwa Agosti, 2012. Awamu hii inatekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini kwa lengo la kuziwezesha kaya masikini kuongeza kipato, fursa na uwezo wa kugharamia mahitaji muhimu.

“Utekelezaji wa Mpango huu umegawanyika katika vipindi viwili vya miaka mitano kwa kila kipindi, Kipindi cha Kwanza kilianza Mwaka 2012 na kukamilika Mwaka 2019 Kipindi cha Pili kilianza kutekelezwa Desemba 2019 baada ya kukamilika kwa utekelezaji wa Kipindi cha Kwanza na utekelezaji utakamilika September 2025,”

Hata hivyo amesema Moja kati ya shughuli kuu za Mpango wa TASAF awamu ya tatu kipindi cha kwanza ilikuwa ni utoaji wa Ruzuku kwa Kaya za Walengwa. Katika Kipindi cha Kwanza kiasi cha shilingi billion 968.7 zilikuwa zimehawilishwa kwa kaya za walengwa zipatazo 1,118,752 katika vijiji, mitaa na shehia 9,831.

Hali kadhalika katika Kipindi cha Pili hadi kufikia Juni 2023 kiasi cha shilingi bilioni 696.7 zimehawilishwa kwa kaya za walengwa zipatazo 1,371,916 katika vijiji, mitaa na shehia 17,260.

Aidha, Mpango umekuwa ukitekeleza Miradi ya Ajira ya Muda ambapo unatoa ajira ya muda kwa kaya ya mlengwa ili kuongeza kipato cha kaya na kuiwezesha jamii kupata raslimali itakayochochea maendeleo ya sehemu husika. Jumla ya miradi 17,421 imetekelezwa ambapo kaya zipatazo 676,610 zilishiriki kufanya kazi katika sekta mbalimbali za kutoa huduma kwa jamii kama afya, elimu na maji na kulipwa ujira.