Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,Dodoma

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali kwa mwaka 2022/2023 imeonesha mashirika ya umma 34 yaliripoti
hasara au nakisi kwa miaka miwili mfululizo ambapo mashirika haya yalijumuisha mashirika yanayojiendesha kibiashara 11 na mashirika yasiyo ya kibiashara 23.

Akiwasilisha ripoti hiyo leo Aprili 15,2024 mbele ya Waandishi wa habari,Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu (CAG)Charles Kichele amesema mashirika yasiyo ya kibiashara yaliripoti nakisi kutokana na upungufu wa fedha kutoka Serikalini na vyanzo mbadala vya mapato.

Ripoti hiyo iliwasilishwa Machi 28,2024 kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan Ikulu Chamwino na Mapema leo imewasilishwa Bungeni na Naibu Waziri wa Fedha Hamad Hassan Chande kisha baadaye CAG kuzungumza na Vyombo vya habari jijini Dodoma.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo imeonesha mashirika ya umma 24 yaliyopata faida au ziada katika mwaka wa fedha 2021/22, yamepata hasara au nakisi katika mwaka wa ukaguzi wa 2022/23 huku Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) imeendelea kupata hasara kwa miaka sita mfululizo.

CAG amesema mwaka wa fedha wa 2022/23 Kampuni ilipata hasara ya shilingi bilioni 56.64, hasara hii imeongezeka ikilinganishwa
na hasara ya shilingi bilioni 35.23 mwaka wa 2021/22, ATCL imeendelea kupata hasara licha ya kuwa inapokea ruzuku kutoka Serikalini.

Ripoti hiyo imeeleza ,”Kwa mfano, mwaka wa fedha 2022/23, ATCL ilipokea ruzuku ya shilingi bilioni 31.55 kwa ajili ya kugharamia mishahara ya wafanyakazi, mafunzo ya majaribio, na ruzuku ya shilingi bilioni 7.45 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, “imeeleza ripoti hiyo

Pamoja na mambo mengine Sababu zinazopelekea hasara zinajumuisha kuwapo kwa gharama kubwa za uendeshaji wa shughuli za ATCL, pamoja na gharama zisizoepukika kama vile gharama za ukodishaji na bima kwa ndege ya Airbus A220 –
300 isiyofanya kazi kutokana na matatizo ya kiufundi kama vile kutu na kasoro za injini.

Matatizo haya yamegunduliwa na mtengenezaji wa ndege hiyo na yameathiri idadi ya ndege za aina hi kote ulimwenguni.
Kuharibika kwa ndege ya Airbus A220 – 300 kuliathiri mwenendo wa safari za ndege, hivyo kusababisha ATCL kukosa mapato na kushindwa kufidia gharama za kudumu za ndege iliyoharibika.

Aidha, Serikali imechukua hatua mbalimbali ili kuboresha uendeshaji wa kampuni hii
ikiwemo, kuundwa kwa timu ya wataalamu inayofanya tathmini ya masuala ya kiufundi ya ndege, kifedha na utendaji wa ATCL katika
biashara ya usafiri wa anga.

Kampuni ya Mawasiliano ya Tanzania (TTCL) imepata hasara kwa miaka miwili mfululizo. Katika mwaka wa fedha wa 2022/23, kampuni
ilipata hasara ya shilingi milioni 894 ikilinganishwa na hasara ya shilingi bilioni 19.23 katika mwaka wa fedha 2021/22 huku sababu ya kupungua kwa hasara hiyo ikitajwa kuwa ni ongezeko la mapato mengineyo kwa shilingi bilioni 8.05. Kwa upande mwingine, kuna kupungua kwa gharama kama vile gharama za mauzo kwa shilingi bilioni 12.58 na gharama za uendeshaji wa mtandao kwa shilingi bilioni 6.22.

“Haya ni matokeo ya mkakati wa kudhibiti gharama uliotumiwa na TTCL katika
mwaka wa fedha wa 2022/23. Aidha, tarehe 30 Oktoba 2022, Serikali ilitangaza nia ya kuhamisha umiliki wa Mkongo wa Taifa (NICTBB) kwenda Kampuni ya TTCL. Uamuzi huu unatarajiwa kuongeza mali za kampuni katika mwaka wa fedha 2023/24, kwa ongezeko la zaidi ya shilingi bilioni 400 kutokana na NICTBB,”inaeleza ripoti

Vilevile ripoti hiyo inaeleza kuwa mapato ya jumla ya kampuni yanatarajiwa kuongezeka kwa zaidi ya shilingi bilioni 20 kutokana na NICTBB na kwamba Shirika la Masoko la Kariakoo limepata hasara mfululizo kwa miaka miwili iliyopita.

Ripoti inafafanua kuwa Katika mwaka wa fedha wa 2022/23, shirika limepata
hasara ya shilingi bilioni 41.57, ambayo ni kubwa kuliko hasara ya shilingi milioni 517.97 iliyopatikana katika mwaka wa fedha uliopita2021/22 sababu kuu ya hasara ni kusitishwa kwa ukusanyaji wa mapato katika eneo la soko la Kariakoo.

” Hii ni baada ya tukio la moto mwaka 2020 ulioteketeza jengo la soko la Kariakoo ambapo kwa matokeo hayo, shirika lilishindwa kukusanya mapato katika soko
kwa ukamilifu kuanzia mwaka wa fedha 2020 hadi Juni 2023 kutokana na kusitishwa kwa shughuli za soko ili kupisha ujenzi wa majengo,.

Aidha, shirika lilirekodi hasara ya shilingi bilioni 41.25 kutokana na kupoteza thamani kwa jengo lililoungua ambapo ni sehemu ya matumizi yaliyorekodiwa katika mwaka wa fedha 2022/23,Ukiondoa tukio la moto
la mwaka 2020, ambalo lilisababisha kupungua kwa ukusanyaji wa mapato, Serikali imekuwa ikilipa gharama za uendeshaji wa kampuni, ikiwa ni pamoja na mishahara ya wafanyakazi na gharama zingine, “inaeleza

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya CAG katika mwaka wa fedha 2022/23, Serikali ilitenga shilingi milioni 671.15 kwa ajili ya mishahara ya wafanyakazi na shilingi milioni 518.68 kwa matumizi mengineyo ambapo pamoja na Ruzuku kutoka Serikalini, Shirika la Masoko la Kariakoo linaendelea kupata hasara.

Kwa upande wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) limepata hasara mfululizo kwa miaka
miwili iliyofuatana ambapo Katika mwaka wa fedha 2022/23, shirika lilipata hasara ya shilingi bilioni 100.70, ikilinganishwa na hasara ya shilingi bilioni 190.01 katika mwaka wa fedha 2021/22.

Aidha Shirika limeendelea kupata hasara licha ya kuwa linapokea ruzuku kutoka Serikalini.

Please follow and like us:
Pin Share