Na Stella Aron, JamhuriMedia, Tanga

“Uboreshwaji mkubwa uliofanywa na Serikali kwa kuwekeza Bilioni 400 umeleta mapinduzi makubwa katika bandari ya Tanga ambapo hadi sasa umehudumia meli 29 zilizobeba tani 221, 440 na kuibadili bandari ya mkakati.

“Pia uwekezaji huo umeibadili bandari kwa kuongeza kina cha maji kutoka mita tatu hadi 13 eneoo la kuingilia meli la gati na la kugeuza na kuwa na uwezo wa kuhudumia tani milioni tatu za mizigo kwa mwaka,” amesema Meneja wa bandari ya Tanga Masoud Mrisha wakati akizungumza na wahariri waliotembelea kujionea utendajikazi wa bandari hiyo.

Bandari ya Tanga ni miongoni mwa Bandari kuu tatu za mwambao wa Bahari ya Hindi, zilizo chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA); iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Bandari No.17 ya mwaka 2004. Sheria hii ilitungwa na kuchukua nafasi ya sheria ya zamani “Tanzania Harbours Authority”.

Lengo kuu la kutungwa kwa sheria ya Bandari ya Mwaka 2004 ni kutumia fursa za kijiografia za nchi ya Tanzania ili kuhudumia nchi za jirani na hivyo basi kuipatia TPA majukumu ya kuendesha Bandari za Pwani ya Bahari ya Hindi na Maziwa Makuu.

Kupitia Sheria hiyo, kifungu cha 12 (1) (a) hadi (w) kinaipa nguvu za kisheria TPA kutekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo uendelezaji wa Bandari zote Tanzania zikiwemo zile zilizoko katika Maziwa Makuu.

Bandari ya Tanga ilianzishwa miaka ya 1880 na Ukoloni wa Kijerumani ikijulikana kama “Marine Jetty”. Ujenzi wa gati ya kwanza lenye urefu wa mita 221 ulifanyika mwaka 1914, na gati ya pili lenye urefu wa mita 229 mnamo mwaka 1954.

Mrisha anasema kuwa gati zote mbili zenye jumla ya urefu wa mita 450 zilikuwa na kina cha maji (draft) mita 3 na uwezo wa kuhudumia shehena tani 750,000 kwa mwaka. Hali hiyo ilisababisha Bandari kutokuwa na uwezo wa kupokea meli gatini, na kufanya kazi ya upakuaji na upakiaji kufanyika nangani umbali wa Kilometa 1.7 kutoka gatini.

Aidha, eneo la Bandari ya Tanga lina jumla ya Hekta 400 ambapo Hekta 17 kati ya hizo ndipo ilipo Bandari ya sasa, Hekta 176 zipo eneo la Mwambani na Hekta 207 zipo katika kijiji cha Chongoleani eneo ambalo linatarajiwa kujengwa gati ya kuhudumia shehena ya Mafuta.

“Maboresho mengine yalifanyika katika Bandari ya Tanga kuanzia Mwaka 2019 ikiwa ni kuboresha magati mawili ya awali yenye urefu wa mita 450, kuongeza kina cha maji kutoka mita 3 hadi 13 (chart datum) kwenye eneo la kuingilia meli, eneo la gati pamoja na eneo la kugeuzia meli. Hivyo kufanya Bandari ya Tanga kwa sasa iwe uwezo wa kuhudumia tani 3,000,000 kwa mwaka,” anasema.

MWENENDO WA SHEHENA KATIKA KIPINDI CHA MIAKA MITANO ILIYOPITA (2018/19 – 2022/23),UTENDAJI KAZI WA MIEZI NANE (JULAI-FEBRUARI, 2024)

Anasema kuwa bandari ya Tanga imekuwa ikihudumia shehena mbalimbali, kati ya sheheza hizo kuna zinazoshushwa na zipo zinazopakiwa kwenda nchi mbali mbali. Shehena zinazoshushwa katika Bandari ya Tanga ni, mali ghafi za viwanda kama vile; Pet-coke, clinker, Ammonium Nitrate, Sulphur, vipuri vya magari na mitambo mbalimbali, mitambo ya viwandaji, mafuta ya petroli, dizeli, mafuta ya kula n.k.

Shehena inayopakiwa kupitia Bandari ya Tanga kwenda nchi mbalimbali ni kama mazao ya misitu, mafuta ya petroli na dizeli, shaba, kahawa, mkonge, viungo, macadamia n.k.

SHEHENA

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita (2018/19– 2022/23) kiwango cha shehena kwa jumla wake kilichohudumiwa na Bandari kilikuwa kikiongezeka kwa wastani wa asilimia 12.2 kwa mwaka. Shehena iliongezeka kutoka tani za mapato 667,976 mwaka 2018/19 hadi tani za mapato 987,828 mwaka 2022/23 kama inavyooneshwa kwenye Jedwal Na 1.

IDADI YA MELI KATIKA KIPINDI CHA MIAKA MITANO (2018/19 – 2022/23)

MELI ZA KIMATAIFA NA MWAMBAO

Anasema kuwa idadi ya meli za kimataifa na mwambao zilizohudumiwa zimeongezeka kutoka meli 125 Mwaka 2018/19 hadi meli 197 Mwaka 2022/23 sawa na wastani wa ongezeko la asilimia 16.2 kwa mwaka.

Aidha ukubwa wa meli (GRT) umeongezeka kutoka GRT 677,922 mwaka 2018/19 hadi GRT 969,986 mwaka 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia11.3.

SHEHENA YA MAKASHA

Idadi ya jumla ya makasha yaliyohudumiwa iliongezeka kutoka Makasha 6,259 TEUs kwa mwaka 2018/19 hadi Makasha 7,244 TEUs kwa mwaka 2022/23, sawa na ongezeko la wastani wa asilimia 4.3 kwa mwaka.

Anaongeza kuwa pamoja na maboresho katika Bandari ya Tanga bado Bandari ya Tanga ina changamoto ya upatikanaji wa shehena ya makasha sababu kubwa ikiwa ni uhaba wa shehena ya kupeleka nje ya nchi (Export), hii inapelekea wamiliki wa meli kutoleta meli kubwa na hivyo Bandari ya Tanga kuhudumia feeder vessels kwa shehena ya makasha.

ABIRIA WALIOHUDUMIWA KWA KIPINDI CHA 2018/19-2022/2023

Idadi ya abiria waliohudumiwa katika Bandari ya Tanga kwa kipindi cha miaka mitano imekuwa ikiongezeka kwa wastani wa asilimia 3.5 kwa mwaka.
Mwaka 2018 – 19 idadi ya abiria waliopanda walikuwa 31, 726 na mwaka 2019-20 walipanda ni 34, 975, mwaka 2020- 21 walipanda ni 26, 539, abia waliopanda mwaka 2021- 22 ni 49, 703 na mwaka 20222- 2 waliopanda ni 31,473.

UTENDAJI KAZI KATIKA BANDARI YA TANGA 2023/2024 KWA KIPINDI CHA MIEZI NANE (JULAI-FEBRUARI 2024)

Shehena iliyohudumiwa katika kipindi cha Julai 2023 – Machi 2024, kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ilifikia tani 868,957 DWT ikiwa ni sawa na asilimia 116.1 ya shehena iliyohudumiwa kawa kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2022/23 ambapo jumla ya tani 748,742 DWT zilihudumiwa. Tazama Jedwali Na 1 kwa ufafanuzi Zaidi.

MELI

Meneja huyo anasema kuwa jumla ya meli 217 zenye ukubwa wa GRT 1,160,799 zilihudumiwa katika kipindi cha Julai 2023 hadi Febuari, 2024. Meli 94 zikiwa za Kimataifa (Deep Sea) na Meli 123 zikiwa meli za Mwambao (Coastal vessel).

Idadi hiyo ya meli zilizohudumiwa ni asilimia 35.6 juu ya meli zilizohudumiwa kipindi kama hicho kwa mwaka 2022/23 ambapo meli 160 zenye ukubwa wa GRT 710,655 zilihudumiwa.

MAKASHA

Makasha yaliyohudumiwa katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024 yalifikia makasha (TEUs) 5,182 ikilinganishwa kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2022/2023,Makasha yamepungua kwa asilimia 11.8 kwani Julai 2022- Machi 2023,jumla ya makasha (TEUs) 5,872 yalihudumiwa.Tazama Jedwali Na 3 kwa ufafanuzi zaidi.

ABIRIA

Anaongeza kuwa katika kipindi cha miezi tisa Julai 2023-Machi 2024, idadi ya abiria waliohudumiwa walifikia 41,077 sawa na asilimia 65.3 ya abiria waliohudumiwa kwa kipindi kama hicho kwa mwaka 2022/23 ambapo jumla ya abiria 62,916 walihudumiwa. Upungufu huu wa abiria umechangiwa na meli iliyokuwa ikitoa huduma kusitisha huduma zake toka mwezi Februari 2023,hata hivyo huduma ya kusafirisha abiria imeanza kutolewa tena mwezi Novemba 2023.Tazama Jedwali Na.4 kwa ufafanuzi zaidi.

MRADI WA MABORESHO BANDARI YA TANGA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Uchukuzi chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ilitekeleza miradi miwili ya kimkakati katika awamu mbili yenye jumla ya thamani ya fedha TZS. 429.1 bilioni katika Bandari ya Tanga.

AWAMU YA KWANZA (PHASE I):

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania iliingia mkataba na Mkandarasi M/S China Habour Engineering Company (CHEC) tarehe 3/8/2019 na kuanza rasmi utekelezaji wa kazi mwezi Oktoba 2019 na kukamilika mwezi Juni 2022 kwa thamani ya TZS. 172.3 bilioni.

Pia mnamo Oktoba 24, 2019 TPA iliingia mkataba na kampuni za M/s NIRAS A/S (AS A LEAD Firm) ya Denmark kwa ushirikiano na M/S Maritime & Transport Business Solution, M/S ILF Consulting Engineers na M/S Anova Consult Company Limited ya Tanzania kwa kufanya upembuzi yakinifu na kusimamia mikataba ya ujenzi wa gati pamoja na kuongeza kina (draft) katika Bandari ya Tanga kwa niaba ya TPA.

Menja bandari Mrisha anasema kuwa mradi huu ulihusisha upanuzi wa eneo la kuingia na kutoka Bandarini (entrance channel) lenye upana wa mita 73, uongezaji wa kina cha maji (dredging) kutoka mita 3 hadi kufikia mita 13 (draft), upanuzi wa eneo la kugeuzia meli (turning basin) kuwa na kipenyo cha mita 800, ununuzi wa mitambo kumi na sita (16) ya kuhudumia shehena.

“Eneo la Ununuzi wa mitambo ya kuhudumia shehena ulihusisha vifaa vya
Diesel Electrical Operated Mobile Habour Crane tani 100 2Pc, Forklift tani 16 1P, Forklift tani 5 1Pc, Bale Clamp (Forklift) tani 3 2Pc , Front loader tani 50 1Pc , Empty container handler tani 16 1Pc , Terminal Tractor (TT) 2P, Grab tani 15 1Pc , Rubber Tyred Gantry (RTG) tani 45 1Pc , Spreader 40 ft 2Pc, Spreader 20 ft 2Pc na kufanya jumla 16Pcs” anaongeza.

Anasema kuwa mradi huu wa awamu ya kwanza ulishakamilika kwa asilimia 100 na meli kubwa zimeanza kuingia na kufunga katika eneo la maegesho na mitambo inafanya kazi ya kupakia na kupakua shehena kwa ufanisi.

AWAMU YA PILI (PHASE II):

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania iliingia mkataba na Mkandari M/S China Habour Engineering Company (CHEC) tarehe mnamo tarehe 30 July, 2020 kwa ajili ya kuboresha Bandari ya Tanga awamu ya pili na kuanza kazi mnamo tarehe 16 Disemba 2020.

GHARAMA NA MUDA WA MRADI

Mradi huu ulitekelezwa kwa kutumia fedha za ndani za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia TPA chini ya Wizara ya Uchukuzi. Mradi huu umegharimu kiasi cha fedha TZS. 256.8 bilioni ikiwa ni gharama za ujenzi kwa Mkandarasi.

Kwa ujumla mradi huu umekamilika kwa asilimia 100 ya utekelezaji wake na kwa sasa tupo katika kipindi cha matazamio (Defect Liability Period) ambacho kitaisha mwezi Aprili 2024.

UKUBWA WA MRADI

Mradi huu una Gati lenye urefu wa mita 450, kina cha mita 13CD na yadi ya makasha (Container yard) ya mita za mraba 7,230. Gati hili lina uwezo wa kuhudumia meli za makasha 2 zenye urefu wa mita 220 na kubeba tani mpaka 60,000 kwa wakati mmoja.

MAWANDA YA MRADI

Mrisha anasema kuwa radi wa Ubunifu na Ujenzi wa Gati hili ulihusisha utekelezaji wa vipengele vikuu vitatu (3): Huduma za Usanifu Yakinifu (Detailed Design Services), Huduma za upimaji wa eneo la mradi (Site Survey), Utafiti wa kina cha bahari, mawimbi ya bahari na utafiti wa udongo na miamba (Bathymetric and Geotechnical Surveys); usanifu wa Gati na Yadi (Design of Berth and Terminal)

Sehemu ya pili ni ujenzi wa Gati (berth) kwa kuongeza mita 50 upande wa Mashariki kuelekea baharini na mita 92 upande wa Magharibi kuelekea baharini, Yadi (terminal) na Kuongeza kina cha Bahari kwenye mkondo wa Bahari upana wa mita 73 na eneo la kugeuzia meli (Dredging) kipenyo cha mita 800.

Tatu ni ujenzi wa kazi za huduma ikijumuisha mifumo ya Tehama, zimamoto, maji na umeme.

USHIRIKI WA WAZAWA

Ajira kwa wazawa upande wa Mhandisi Mshauri aliajiri Wahandisi wazawa 4 na kwa upande wa kada nyingine aliajiri wafanyakazi 3 wakati wa utekelezaji wa mradi huu.

Kwa upande wa Mkandarasi Mjenzi wafanyakazi wazawa 151 mpaka 581 wa kada mbalimbali waliajiriwa kwa kipindi chote cha utekelezaji wa Mradi.

LENGO LA MRADI

Lengo la mradi huu ni kuimarisha na kuboresha magati mawili (2) yenye urefu wa mita 450, kuongeza mita 50 upande wa Mashariki na mita 92 upande wa Magharibi kuelekea Baharini, ikiwa ni pamoja na kuongeza kina cha maji (Draft) kutoka mita3 hadi mita 13CD.

“Kabla ya kujengwa gati hili, Bandari ya Tanga ilikuwa ina uwezo wa kuhudumia shehena tani 750,000 kwa mwaka. Baada ya upanuzi, Bandari imekuwa na uwezo wa kuhudumia shehena mpaka tani 3,000,000 kwa mwaka na Makasha yameongezeka kutoka 12,000 TEUs hadi 50,000 TEUs kwa mwaka” anasema.

Anasema kuwa shehena ya mizigo inatarajiwa kuongezeka kutokana na sababu kuongezeka kwa ufanisi kwa kupunguza muda wa kuhudumia meli kutoka siku 5 hadi siku 2. Gharama za uendeshaji zitapungua kutokana na uwezo wa Bandari ya Tanga kuhudumia meli gatini.

Pia kuongezeka kwa wateja walioonesha nia ya kuitumia Bandari ya Tanga kwa Makampuni mbalimbali. Kuongezeka kwa ufanisi na tija katika kuhudumia shehena ya mizigo mbalimbali.

MANUFAA YA MRADI KIUCHUMI

Anasema kuwa tangu kukamilika na kuanza kutumika kwa mradi wa gati jipya, Bandari ya Tanga imeweza kuongeza shehena ya mizigo kutoka tani 735,524 kwa mwaka 2020/2021 mpaka kufikia tani 987,829 kwa mwaka 2022/23.

Baada ya kukamilika kwa mradi huu Bandari ya Tanga imeweza kuhudumia meli kubwa gatini zilizobesha shehena mbalimbali kama inavyoonyeshwa kwenye jedwali;

UJIO WA MELI KUBWA KATIKA BANDARI YA TANGA

Baada ya kukamilika kwa maboresho Bandari ya Tanga imeweza kuhudumia jumla ya Meli 29 mpaka sasa zilizobeba jumla ya tani 221,440 DWT ambaapo kati ya hizo Bandari ya Tanga imeweza kuhudumia Shehena za Ammonium Nitrate tani 40,398DWT, Sulphur tani 50,001DWT, Copper tani 8,837 DWT, Pet-coke tani 98,856DWT

BANDARI YA TANGA KUANZA KUPOKEA MELI KUBWA ZA KONTENA.

Kampuni ya MAERSK imeanza kutoa huduma katika Bandari ya Tanga kwa kuleta meli kubwa iliyobeba makasha matupu 350 yenye jumla ya TEUs 770.

Hata hivyo makampuni mengine kama CMA-CGM,PIL yapo mbioni kuleta meli kubwa za makasha katika Bandari ya Tanga.

MIRADI MIPYA INAYOTARAJIWA KUTEKELEZWA

“Baada ya kuona mafanikio chanya ya Mradi huu ambayo imeweza kufungua ushoroba la kaskazini kibiashara Mamlaka inampango wa kutekeleza miradi mbalimbali katika mwaka huu wa fedha ikiwa ni utekelezaji wa mpango mkakati wa Shirika mpaka kufikia mwaka 2025.

“Miradi inayotarajiwa kutekelezwa ni pamoja na kuongeza gati lenye urefu wa mita 300, mita 250 upande wa Magharini na mita 50 upande wa Mashariki.

“Ununuzi na usimikaji wa mashine tatu (3) aina ya Ship to Shore Grantry Cranes (SSG) kwa ajili ya kuhudumia mzigo wa kontena. Usanifu na ujenzi wa eneo la kuhifadhia Makasha karibu na geti na. 2” anasema Mrisha.

Pia kujenga eneo la kuhudumia abiria (Passenger terminal) pamoja na eneo la kupaki majahazi., kukarabati majengo ya ofisi na karakana zilizopo katika Bandari ya Tanga., ujenzi wa matenki ya kuhifadhia mafuta pamoja na gati la kuhudumia meli za mafuta.

SABABU ZA WATEJA KUTUMIA BANDARI YA TANGA

Anasema kuwa sababu za wateja kutumia bandari ya Tanga kutokana na kuwepo kwa punguzo/msamaha wa tozo kwa ajili ya kuwavutia wateja kama tozo ya kuhifadhi shehena iendayo nje ya nchi inaanza baada ya siku 15 badala ya siku 7 za hapo awali ambapo kwa upande wa makasha matupu tozo inaanza baada ya siku 25.

Anasema sababu nyingine ni upande wa mawakala wa meli tozo ya kupakua na kupakia shehena melini (stevedoring charges) imepungua kwa asilimia 25. Pia maboresho yaliyofanywa na Serikali kwa Bandari ya Tanga kwa kuongeza kina cha maji,mlango wa kuingia na kugeuzia meli,ujenzi wa ghat yamepelekea meli kuhudumiwa gatini badala ya nangani kama ilivyokuwa hapo awali na hivyo kuboresha ufanisi na tija kwenye kuhudumia meli na shehena.

“Pia mazingira halisi ya kibiashara kwa mji wa Tanga,hakuna msongamano wa magari wakati wa kuleta na kutoa shehena bandarini.Bandari ya Tanga imeongezewa vifaa mbalimbali vya kisasa kwa ajili ya shughuli ya kupakia na kupakua na hivyo kupelekea huduma za upakuaji na upakiaji kufanyika kwa ufanisi na tija,” anasema.

MIUNDOMBINU NA VIFAA KATIKA BANDARI YA TANGA

Bandari ya Tanga ina miundombinu na mitambo ya kuhudumia meli, shehena ya makasha na mizigo mchanganyiko kama ilivyoainishwa hapa chini Miundombinu

Gati mbili hizi zina lina kina cha mita 13 (CD) na urefu wa mita 225 kila moja na uwezo wa kuhudumia meli yenye uzito wa 50,000DWT.

YADI KABLA YA MABORESHO
Bandari ya Tanga ilikuwa na yadi moja yenye ukubwa wa mita za mraba 29,000 na uwezo wa kuhifadhi makasha 12,000 (TEUs) kwa mwaka.

YADI BAADA YA MABORESHO

Anasema kuwa baada ya maboresho Bandari ya Tanga itakuwa na yadi yenye ukubwa wa Kuna yadi ya kuhifadhia Makasha yenye ukubwa wa mita za mraba 51,950 na uwezo wa kuhudumia makasha 50,000 (TEUs) kwa mwaka.

Kuna maghala matatu ya kuhifadhia shehena (ghala namba 6,7 &8) yenye ukubwa wa 13,400 mita za mraba.

MIKAKATI YA MATUMIZI ENDELEVU YA BANDARI YA TANGA

Anasema kuwa ili kuongeza matumizi na uwezo wa Bandari, mamlaka imeanza kutekeleza mambo yafuatayo; kuendelea kusafirisha shehena ya Shaba, Pet-coke,Clinker kuendelea kuhudumia shehena ya mkonge kwenda masoko ya nje ya nchi.

Pia kuhudumia shehena ya saruji kwenda Zanzibar, kuhudumia shehena ya mafuta kwa kila mwezi; Kuendeleza ushirikiano wa karibu na taasisi binafsi na Serikali ikiwemo ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Wilaya na TCCIA – Tanga.

Kufanya vikao na wadau wa usafirishaji wakiwamo ‘Shipping line, Transporters, Exporters & Importers, Shipping Agents, Clearing and Forwarding Agents’ ili kuwezesha shehena zinazozalishwa katika mikoa ya kaskazini zinasafirishwa kwenda masoko ya nje kupitia bandari ya Tanga.

CHANGAMOTO ZINAZOIKABILI BANDARI YA TANGA

Pamoja na mafanikio yanayoendelea kupatikana katika Bandari ya Tanga, bado Bandari hii inakabiliwa na changamoto mbalimbali. Changamoto hizi ni pamoja na:-
Uhaba wa eneo la kufanyia kazi ndani ya Bandari ya Tanga.Kutokana na Bandari ya Tanga kuwa na eneo finyu la hekta 17.

Kutokuwa na Oil Terminal na Tank Farm Bandari ya Tanga inayopelekea upotevu wa mapato kutokana na kampuni ya GBP kumiliki miundombinu hiyo.

MIKAKATI YA KUTATUA CHANGAMOTO,

Mrisha anasema kuwa mikakati ya kutatua changamoto ya bandari ya Tanga kwa kushirikiana na Serikali imeanza zoezi la utwaaji wa maeneo yaliyozunguka Bandari. Kuomba sekta binafsi kuchangamkia fursa za uwekezaji wa Maghala na ICDs katika Mkoa wa Tanga.

“Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania imeanza mchakato wa ujenzi gati (jetty oil) la kuhudumia meli za mafuta ikifuatiwa na ujenzi wa matanki (storage tank farms).

“Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imedhamiria kuboresha utendaji wa Bandari ya Tanga ili kunufaika na fursa kubwa zilizopo.

“Rai yetu ni kuomba Serikali na wadau wengine kama sekta binafsi waendelee kutekeleza mipango ya kuboresha miundombinu ya usafirishaji wa nchi kavu hasa reli na kuwekeza katika ujenzi wa maghala na ICDs katika jiji la Tanga ili kurahisisha shughuli za kibandari,” anasema.

Please follow and like us:
Pin Share