NA MWANDISHI WETU

DAR ES SALAM

Wiki iliyopita kimefanyika kikao baina ya jumuiya ya wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo na mawaziri watatu; Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwezeshaji, Charles Mwijage; Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isaac Kamwelwe.
Kikao hicho kimefanyika kwenye Ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam huku wafanyabiashara wakionyesha kutoridhishwa na namna Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inavyowatendea hasa kwenye ushuru.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa Kariakoo, Mchungaji Silver Kiondo, anasema wafanyabiashara ndogo ndogo (wamachinga) ni lango la kutorosha mapato ya serikali, kwa kuwa kuna wafanyabiashara wakubwa Karikaoo ambao wamekuwa wakifunga maduka na kusambaza mizigo yao kupitia wamachinga.
Mchungaji Kiondo, ambaye wakati akitamka maneno hayo alikuwa akishangiliwa na kundi la wafanyabiashara, anasema serikali inapoteza mapato yake kutokana na wamachinga, ameshauri kwamba hatua madhubuti zinapaswa kuchukuliwa ili kukabiliana na hali hiyo.
“Tukiwa wazalendo wamachinga wanatupa mzigo wa kukusanya kodi…wamachinga hatuna ugomvi nao, ni Watanzania wenzetu, ni wadogo zetu, ila serikali isipoweka utaratibu wenye uzalendo wa kweli, tukichukulia jambo hili kisiasa, tunaua uchumi wa nchi yetu. Sasa hivi kuna watu ambao hawafungui maduka, wanaweka mizigo stoo na wanasambaza kupitia wamachinga.
“Wafanyabiashara tumekuwa tukisema na tunaendelea kusema kwamba mapato yanapotea, hii nchi ni yetu sote na kama wafanyabiashara tunaomba jambo hili liangaliwe kwa sura ya pili ya kiuchumi ili kutimiza azima nzuri ya Rais John Magufuli pasipokuwa na hujuma ya uchumi,” anasema Mchungaji Kiondo.
Ameitaja kero nyingine kwa wafanyabiashara wa Kariakoo kwamba wengi wamekuwa wakifunga biashara zao kutokana na ‘kamatakamata’ inayofanywa na TRA na polisi kusaka wasiofunga mashine za kukusanya mapato kielektroniki (EFDs).
Kiongozi huyo wa wafanyabiashara anasema bandarini kuna upotevu mkubwa wa mapato kutokana na kutokuwapo uwazi wa kodi, jambo ambalo baada ya ufafanuzi kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Bandari, Mhandisi Deusdedit Kakoko, anasema TRA ndio wanahusika na tozo na ushuru.
Mchungaji Kiondo anasema kero nyingine ni kuondolewa kwa kamati ya pamoja iliyokuwa inahusisha watu kutoka Ofisi ya Rais – Ikulu; Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Anasema kamati hiyo ilikuwa inasaidia kuweka baadhi ya mambo sawa na kuepuka mkanganyiko.
“Leo ukizungumza kuhusu hiyo kamati unaonekana umepitwa na wakati… kamati hii imeuawa na TRA. Wafanyabiashara wanaamini Serikali ya Awamu ya Tano haina mpango na sisi na inataka kutuua, hatutakufa kwa wakati mmoja, wengine watabaki.
“Hiki ni kikwazo kabisa…tunashauri ile kamati ifufuliwe na endapo haitafufuliwa shida itakuwa kubwa zaidi. Kuwepo na uwazi wa kodi pale bandarini,” anasema Mchungaji Kiondo.
Anasema uagizaji wa bidhaa kutoka nje umeshuka kiasi ambacho hata wafanyabiashara wa Kariakoo wamepoteza wateja kutoka Kongo DRC, Zambia, Malawi, Uganda na Rwanda.
Wafanyanbiashara hao wamewaambia mawaziri kwamba vitendo vya rushwa vimeongezeka kutokana na baadhi ya watumishi hao wasio waaminifu, hivyo kuikosesha serikali mapato. Wanasema wafanyabiashara kutoka nje wamekuwa wakilikimbia Soko la Kariakoo kutokana na usumbufu wanaoupata, hivyo kufanya soko kukosa utulivu.
Wamesisitiza kwamba wanaunga mkono juhudi za serikali katika kudhibiti viwango vya ubora wa bidhaa, ila wameshauri taasisi zinazofanya kazi ya ukaguzi zinatakiwa ziwe kitu kimoja.
Wamezitaja taasisi hizo ambazo ni Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) pamoja na Tume ya Ushindani wa Haki (FCC) kila moja inafanya kazi kivyake, hivyo kuwasababishia wafanyabiashara wa bidhaa mchanganyiko hasa wa urembo, ambao makontena yao yana mchanganyiko wa bidhaa zaidi ya 100, kukwama endapo bidhaa moja ikibainika ina kasoro.
Mmoja wa wafanyabiashara ya vitenge, Daniel Gervas, amehoji Serikali ya Awamu ya Tano, imewaweka wafanyabiashara wanaoagiza bidhaa kutoka nje ya nchi katika nafasi gani? Pia amehoji, serikali inawasaidiaje kuanzisha viwanda?
Gervas ameinyoshea kidole TRA, akisema wamekuwa wakiwaita wafanyabiashara waongo, hasa linapokuja suala la kutangaza bidhaa zilizoagizwa na kufungashwa kwenye makontena.
“Wanatuita waongo katika bei tunazowaambia, nadhani ingekuwa busara katika kutulea wafanyabiashara wadogo kama sisi wakaondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), walioko chini ya Sh milioni 100 wasitozwe na wanaoanzia zaidi ya hizo watozwe…TRA wamekuwa wanatoza kodi kubwa kwenye bidhaa za Polyster kama bidhaa zitokanazo na pamba,” anasema Gervas.
Akijibu kero na malalamiko ya wafanyabiashara hao, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mpango, anasema wameyapokea na watayafanyia kazi kama wizara ili kutoa majibu na mrejesho muafaka, ambao utaleta matokeo chanya kwa wote.
Waziri huyo anasema serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri na wezeshi kwa wafanyabiashara ili waendelee kufanya biashara zao na kulipa kodi. Anasema serikali imekuwa na utaratibu kila Novemba na Desemba, kutoa tangazo na kupokea maoni ya mabadiliko ya kodi kila mwaka.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwezeshaji, Charles Mwijage, anasema serikali itaendelea kuruhusu bidhaa kutoka nje kuingia nchini kwa kuwa hata Watanzania wanauza nje.
Mwijage amewataka wafanyabiashara hao kuwa waaminifu kwa kuwa wengine walikuwa wakiingiza bidhaa zisizofaa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isaac Kamwelwe, alitaka mamlaka zinazohusika na ukaguzi na utoaji wa mizigo bandarini kuhakikisha wanaangalia uwezekano wa kuzuia mizigo inayoonekana ina kasoro katika makontena na kuitoa ambayo haina tatizo ili kutowakwamisha wafanyabiashara. Mkutano huo ni utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli la kuwataka mawaziri kukutana na wafanyabiashara ili kujua changamoto wanazokutana nazo katika biashara ili wazifanyie kazi.

Mwisho

Please follow and like us:
Pin Share