Serikali yabainisha mikakati ya kupambana na changamoto utoaji mimba usio salama

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia-WF,Dodoma

Naibu Waziri wa Afya Dkt.Godwin Mollel amebainisha juhudi zinazofanywa na Wizara ya Afya katika mapambano dhidi ya changamoto ya utoaji mimba usio salama ikiwemo, kutoa elimu juu ya afya ya uzazi kwa watoto wa kike ambao wapo chini ya umri wa kuzaa.

Dkt.Mollel amesema hayo leo Juni 2,2023 wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu Mhe. Judith Salvio Kapinga katika Bunge la kumi na mbili Mkutano wa kumi na moja kikao cha 39, Jijini Dodoma.

Ameendelea kusema, Wizara kupitia vitengo vyake imeendelea kutoa elimu kwa klabu za vijana na vijana balehe kutojihusisha na ngono zembe (abstinence) ili kuepuka kupata mimba zisizotarajiwa ambazo hupelekea kuongezeka vitendo vya utoaji mimba usio salama.

Aidha, Dkt. Mollel amesema, Wizara inaendelea kusimamia utoaji wa huduma za uzazi wa mpango katika vituo vya huduma bila malipo ili kuwawezesha wanawake na wanaume kuzuia mimba zisizotarajiwa.

Sambamba na hilo, Dkt. Mollel amesema, ametoa wito kwa jamii kuhakikisha mimba zote zinapatikana kwa mpango ili kuondokana na changamoto ya utoaji mimba usio salama unaoweza kuathiri afya za wajawazito.

Pia, amewataka wajawazito kuhudhuria katika kliniki za uzazi wa mpango ili waweze kupatiwa elimu ya afya ya uzazi ikiwemo jinsi ya kuepukana na mimba zisizotarajiwa ili kuondokana na uavyaji wa mimba usio salama.

Hata hivyo daktari bingwa katika masuala ya Afya ya Mama na Mtoto, Dkt.Peter Kibacha amesema kuwa kuna sababu nyingi zinazochangia vifo vya uzazi kama utokwaji damu usio wa kawaida, tatizo linalochangia kwa asilimia 24, kifafa cha mimba asilimia 12 na utoaji mimba au uviaji asilimia 13.

Amesema kuwa kuna mimba milioni 20 zisizotarajiwa hutolewa kwa njia isiyo salama duniani hususani katika nchi zisizoendelea kila mwaka hili ni tatizo kubwa.

Watafiti waligundua kwamba utoaji mimba kwa siri hutokea mara nyingi na huchangia kwa kiasi kikubwa kwenye vifo na kuumia kwa wajawazito.

Utafiti huo, uliofanywa na watafiti kutoka taasisi ya Guttmacher iliyoko Marekani, Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili zilizoko hapa Tanzania.