Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imedhamiria kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji katika Sekta ya Utalii ili ichangie kikamilifu katika Uchumi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ameyasema hayo alipokuwa akifungua mkutano wa Tatu (3) wa Wizara ya Maliasili na Utalii wa majadiliano baina ya Sekta ya Umma na binafsi katika utalii (ministerial public Private dialogue – MPPD) uliofanyika leo Mei 13, 2025 katika hotel ya St. Gasper jijini Dodoma.

“Amesema Wizara inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kukuza utalii ikiwa ni pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma, miundombinu ya utalii na utangazaji wa vivutio vya utalii imeongezeka na kufikia 5,360,247 ambapo watalii wa ndani ni 3,218,352 na watalii wa nje 2,141,895 na mapato yatokanayo na shughuli za Utalii
yapatayo Dola za Kimarekani Bilioni 3.3.
Kufuatia ongezeko hilo, Tanzania imetajwa na Shirika la Utalii Duniani (UN – Tourism) kuwa nchi ya kwanza Afrika kwa ongezeko kubwa la watalii wa kigeni ikilinganishwa na kabla ya UVIKO mwaka 2019.
“Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) kupitia taarifa yake ya World Tourism Barometer ya Januari, 2024 imeitambua Tanzania kuwa miongoni mwa nchi ambazo zimevunja rekodi ya idadi ya juu ya watalii wa kimataifa (best performing destinations January to December, 2023).

Kadhalika, Tanzania imeshika nafasi ya 12 duniani kwa ongezeko la watalii ikitanguliwa na Uturuki, Qatar, Saudi Arabia, Albania, El Salvador, Colombia, Andorra, Ethiopia, , Curacao, Jamhuri ya Domican na visiwa
vya US virgin” amesisitiza Mhe. Chana.
Aidha, ameweka bayana kuwa Tanzania imeendelea kutambulika Kimataifa na kupata Tuzo mbalimbali za Utalii kwa mwaka 2024. Baadhi ya Tuzo hizo ni pamoja na Eneo linalovutia zaidi kiutalii (Africa’s Leading Destination); Eneo linaloongoza kwa utalii wa safari duniani (World’s Leading Safari Destination); Hifadhi ya TaifaSerengeti kuendelea kuwa hifadhi bora Duniani; Mlima Kilimanjaro kuwa kivutio bora cha utalii barani Afrika (African Leading Tourism Attraction) pamoja na Bodi ya Utalii Tanzania kuwa Bodi Bora Afrika.
Mhe. Chana ametumia fursa hiyo kutoa rai kwa wadau wa utalii kuendelea kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kusimamia na kuendeleza Sekta ya utalii kwa maslahi mapana ya Taifa.

Kwa upande wake Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt.Hassan Abbasi amefafanua kuwa malipo ya fedha za kigeni ni kwa ajili ya miamala ya ndani hivyo malipo ya Kimataifa katika sekta ya utalii yataendelea kufanyika kama kawaida.
Katika hatua nyingine, Dkt. Abbasi amewaahidi wadau wa utalii kwamba hakutakuwa na tozo za ghafla katika kipindi hiki na kwamba ikitokea huko mbeleni wadau wa Sekta ya Utalii watahusishwa kikamilifu.
Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala ww Utalii Tanzania (TATO), Wilbard Chambulo ameiomba Serikali kuendelea kuboresha miundombinu katika maeneo ya hifadhi ili kuvutia wawekezaji sambamba na kuruhusu matumizi ya fedha za kigeni (USD) kwa wafanyabiashara za utalii kimataifa.
Pia, ameongeza kuwa ni vyema Serikali ikashughulikia suala la Bima kwa waongoza watalii na wapagazii na suala la mikataba ya uwekezaji iwe na usawa kwa wawekezaji wote Serikalini.


