Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema Serikali imefanya utafiti kuhusu teknolojia mbadala wa zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu nchini.

Amesema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya hatua zilizofikiwa juu ya uratibu na utekelezaji wa Mpango-kazi wa Taifa wa Kupunguza Matumizi ya Zebaki (2020 – 2025) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira.

Kwa mujibu wa Mhe. Khamis, utafiti umeonesha teknolojia za kuchoma (smelting) kwa kutumia borax na teknolojia za sianadi (cyanidation) ndio zinatumika kwa wingi nchini na nchi zinazoendelea.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akiwasilisha taarifa ya hatua zilizofikiwa juu ya uratibu na utekelezaji wa Mpango-kazi wa Taifa wa Kupunguza Matumizi ya Zebaki (2020 – 2025) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira jijini Dodoma leo tarehe 22 Agosti, 2023. Kulia ni Kaimu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Switbert Mkama.

Amesema Mradi wa Kudhibiti Athari za Zebaki kwa Afya ya Binadamu na Mazingira Kwenye Shughuli za Uchimbaji Mdogo wa Dhahabu Nchini umejikita katika kufanyia kazi teknolojia zinazotumika zaidi nchini.

”Lengo ni kutekeleza malengo la Mkataba wa Minamata hususan kipengele cha saba kinachohusu kupunguza matumizi ya zebaki kwenye uzalishaji wa dhahabu inayozalishwa na wachimbaji wadogo na pale itakapowezekana kuondoa kabisa matumizi ya kemikali hiyo katika kuzalisha dhahabu kwa wachimbaji wadogo,” alifafanua.

Pia, Naibu Waziri Khamis alitaja shughuli za mradi kuwa ni kuimarisha na kujenga uwezo na ujuzi wa taasisi na wachimbaji wadogo kuhusu namna ya kudhibiti athari zinazotokana na utumiaji wa zebaki kwenye uzalishaji wa dhahabu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Mhe. Jackson Kiswaga akiongoza kikao cha kupokea taarifa ya hatua zilizofikiwa juu ya uratibu na utekelezaji wa Mpango-kazi wa Taifa wa Kupunguza Matumizi ya Zebaki (2020 – 2025) iliyowqasilishwa na Ofisi ya Makamu wa Rais jijini Dodoma leo tarehe 22 Agosti, 2023.

Aidha, katika kutekeleza Mpangokazi wa Taifa wa Kupunguza Matumizi ya Zebaki, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeandaa Mwongozo wa Uingizaji, Matumizi na Utupaji Salama wa Zebaki.

Mhe. Khamis amesema kuwa Mwongozo huo unalenga kutoa utaratibu wa njia salama za usimamizi wa Zebaki pasipo kuathiri afya ya binadamu na mazingira.

Mradi huo wa miaka minne unafadhiliwa na Global Environmetal Facility (GEF) kwa ruzuku ya Dola za Marekani 7,339,450 sawa na Shilingi za Kitanzania bilioni 18.3.unatekelezwa katika mikoa saba ya Geita, Mwanza, Mara, Shinyanga, Singida, Mbeya na Songwe.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira pamoja na wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais wakiwa katika kikao cha kupokea taarifa ya hatua zilizofikiwa juu ya uratibu na utekelezaji wa Mpango-kazi wa Taifa wa Kupunguza Matumizi ya Zebaki (2020 – 2025) iliyowqasilishwa na Ofisi ya Makamu wa Rais jijini Dodoma leo tarehe 22 Agosti, 2023.
(PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)