Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Serikali ya Tanzania imesema imeandaa mbinu na nyenzo maalum za utoaji wa taarifa na hatua za kuchukua kwa makundi ya watu wenye ulemavu ili kuhakikisha hawawaachwi nyuma kuelekea msimu wa mvua za El Niño zilizotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA).

Hayo yamesemwa Septemba 28,2026 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Watu Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba Kabudi wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la uratibu na utekelezaji wa mpango kazi wa kitaifa wa haki na ustawi wa watu wenye ualbino(MTHUWWU).

Prof Kabudi ameeleza kuwa hatua hizo tayari zimeshaandaliwa ili kukabiliana na madhara ya mvua hizo kwa makundi maalum ikiwa ni pamoja na watu wenye uoni hafifu, viziwi na wenye ulemavu mbalimbali.

Aidha amesema kuwa Jukwaa hilo limekutanisha wadau mbalimbali wa serikali,taasisi za kimataifa, asasi za kiraia pamoja na vyama vya watu wenye ulemavu kujadili changamoto mbalimbali zinazodidimiza haki na ustawi wa watu wenye ualbino Nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla kupita mtandao wa watu wenye ualbino barani Afrika (Africa Albinism Network)

Akiangazia hali ya ulinzi na haki za watu wenye ualbino,Prof.Kabudi ameeleza kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa ikilinganishwa na mataifa mengine ya Afrika ambapo bado changamoto za unyanyapaa, ubaguzi na ukatili zinaripotiwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama Cha Watu wenye Ualbino Tanzania, (TAS), Godson Mollel ameipongeza Serikali kwa jitihada zake za kutokomeza mauaji na ukatili dhidi yao,huku akibainisha kuwa utekelezaji wa mpango huo mpya unatoa matumaini makubwa katika kuboresha maisha yao na fursa sawa za elimu, ajira na huduma za afya.

Hata hivyo Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Huduma na Maendeleo ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2004 ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia na mahitaji ya sasa ya kijamii na kiuchumi.