Na Mwandishi wetu
Serikali imefanikiwa kuokoa jumla ya Sh bilioni 13.77 katika kipindi cha mwaka 2019/20 hadi 2021/22 kutokana na shughuli za ugomboaji wa mizigo ya Serikali kufanyika kupitia mifumo na taasisi zake, badala ya kutumia mawakala binafsi.
Mafanikio hayo ni miongoni mwa hatua zilizopatikana katika eneo la ugomboaji na uondoshaji wa mizigo ya Serikali kutoka bandarini, viwanja vya ndege na mipakani.
Kwa mujibu wa wataalam mbalimbali kutoka Wizara ya Fedha waliowasilisha mada katika semina ya waandishi wa habari na wamiliki wa mitandao ya kijamii iliyofanyika Morogoro Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya mwaka 2025, Serikali iliokoa fedha hizo ambazo zingetumika kugomboa mizigo kupitia mawakala binafsi.
Katika eneo hilo, ugomboaji na uondoshaji wa mizigo ya Serikali unasimamiwa na Wakala wa Huduma za Ununuzi Serikalini (GPSA), huku Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) likiwa na jukumu la ugomboaji wa makinikia, kemikali zinazotumiwa na kampuni za madini, nyara za Serikali na wanyama hai.
Aidha, Bohari ya Dawa (MSD) imepewa jukumu la kugomboa na kuondosha bidhaa za afya zinazonunuliwa kutoka nje ya nchi kwa ajili ya vituo vya kutolea huduma za afya.
Mafanikio mengine ni kujengwa na kuanza kutumika kwa mifumo ya kielektroniki ikiwemo Mfumo Jumuishi wa Forodha (TANCIS) na Mfumo Jumuishi wa Kielektroniki katika Utoaji wa Huduma za Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GIMIS), ambayo imerahisisha upatikanaji wa taarifa kuhusu uagizaji, ugomboaji na uondoshaji wa mizigo ya Serikali.
Aidha, fursa zilizopo katika eneo la ugomboaji na uondoshaji ni pamoja na kuimarika kwa miundombinu ya shughuli hizo, matumizi ya mifumo ya kielektroniki na kuongezeka kwa mapato ya Serikali.
Fursa hizo zinaweza kuongeza ufanisi wa shughuli za ugomboaji na uondoshaji, kupunguza gharama na muda wa kushughulikia mizigo pamoja na kuongeza tija katika usimamizi wa mnyororo wa ugavi wa Serikali.
Pamoja na mafanikio hayo, kumekuwepo na upungufu wa kutofungamanishwa kwa shughuli za ugomboaji na uondoshaji wa mizigo ya Serikali, hali ambayo imesababisha changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa shughuli hizo.
Changamoto hizo ni pamoja na gharama kubwa za ugomboaji na uondoshaji zisizozingatia bei ya soko, pamoja na ucheleweshaji wa ugomboaji wa mizigo unaoweza kusababisha uharibifu wa mizigo na hasara kwa Serikali.
Hali hiyo inaonesha umuhimu wa kuendelea kuboresha mfumo na taratibu za ugomboaji na uondoshaji wa mizigo ya Serikali ili kutumia kikamilifu fursa zilizopo na kuimarisha udhibiti wa gharama.
Katika hatua nyingine, eneo la upokeaji na urejeshaji wa bidhaa, vifaa, huduma, kazi za ujenzi au mali linatekelezwa kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura ya 410.
Sheria hiyo inaelekeza taasisi nunuzi kuunda kamati za wataalamu wenye weledi na uzoefu kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa kitaalamu kabla ya kupokea bidhaa, vifaa, huduma, kazi za ujenzi au mali kwa kuzingatia ithibati ya ubora.
Katika eneo hilo, mifumo ya kielektroniki ikiwemo Mfumo wa Uhasibu Serikalini (MUSE) na Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) imewezesha utunzaji wa kumbukumbu za bidhaa, vifaa, huduma, kazi za ujenzi na mali zinazopokelewa na kugawiwa kwa watumiaji, huku mifumo hiyo ikiwa pia ni fursa ya kuendelea kurahisisha utekelezaji wa shughuli hizo.










