Serikali yaonyesha nia kumaliza kiu Mabadiliko ya Sheria ya Habari’

Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Dar

WAKILI wa kujitegemea na mwakilishi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),
amesema kuwa katika mchakato wa Mabadiliko ya Sheria ya Habari,Serikali imeonyesha nia ya kufanyia kazi vipengele mbalimbali hivyo mchakato huo utapata majibu yatakayomaliza kiu sekta ya habari.

Akizungumza leo Agosti 27, 2022 Kipindi cha Jicho Letu Ndani ya Habari kinachorushwa na Televisheni ya Star (Star TV),amesema kuwa nia ya Serikali ni kuhakikisha muafaka unapatikana katika Mapendekezo ya Marekebisho ya Sheria ya Habari, wadau wa habari wamekiri kuwepo kwa nia hiyo.

“Kwa hatua hii tunaona kuwa Serikali imeonyesha nia katika kuhakikisha kuwa mabadiliko yua sheria ya habari yanafanyikiwa kazi na kupata muafaka wa vipengele vya Sheria ya Habari vyenye ukakasi inaonekana wazi,” amesema.

Wadau wa habari wamekuwa wakilenga vifungu vinavyotisha waandishi na uhai wa tasnia ya habari nchini na kwamba, sio sheria yote ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 hazifai.

“Kabla ya kuwapo kwa sheria hiyo, kulikuwa na sheria ya mwaka 2006 ambayo ilikuwa na changamoto kubwa sana ya udhibiti na uchapishaji.Sheria hiyo ilikuwa ikimpa mamlaka makubwa sana Waziri wa Habari kudhibiti uchapishaji wa magazeti,” amesema Marenga.

Na kwamba, mamlaka hayo kwa waziri, sheria mpya ilipotungwa (Sheria ya Huduma za Habari ya 2016) ikayahamisha na kuyapeleka kwa wenda Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo ambapo sasa anaweza kufunga magazeti, kunyima leseni wanahabari na hata kutoa hukumu kwa vyombo vya habari.

Naye Mwenyekiti wa TEF Deodatus Balile,amesema kuwa kwa hatua ya kuonyesha nia Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kusimamia suala hii ni hatua ya kupongezwa.

“Kuna utofauti kwa Serikali ambayo imeonyesha nia ya kutusikiliza katika kusimamia suala hili,kwani imeitisha mkutano na wadau katika kushughulikia suala hili,’’ amesema Balile.

Wakati huo huo,Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari amenukuliwa akisema kuwa, ni wakati Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo akapunguziwa mamlaka.

Kauli hiyo aliitoa Agosti 24,mwaka huu, wakati akizungumza na Mtangazaji Regina Mziwanda katika Kipindi cha Dira ya Dunia kinachorushwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).

Alisema, si jambo linalokubalika kwa mtu mmoja kuwa mlalamikaji katika kesi, msikilizaji katika kesi hiyo hiyo na mwisho akatoa hukumu, akisisitiza hukumu hiyo haowezi kuwa sawa.

“Duniani kote ukitaka haki itendeke, ni muhimu anayelalamika, anayetengeneza mashitaka na anayekwenda kusikiliza mashitaka wawe ni watu tofauti ili haki itendeke,” alisema.