Serikali inalenga kufanya mabadiliko ya kiuundo wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kupitia mabadiliko ya sheria iliyounda Chama hicho.

Kupitia muswada wa mabadiliko ya sheria mbalimbali namba 8, serikali inapendekeza kuanzishwa kwa ‘matawi’ ya TLS mikoani na katika kanda ambayo yatatoa wajumbe wengi katika mkutano mkuu wa mwaka wa TLS ambao pia hutumika kuchagua viongozi wa juu wa chama hicho.

Muswada huo umeshachapishwa kwenye tovuti ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na TLS imeshaanza mjadala kuhusiana na mabadiliko hayo yanayopendekezwa na serikali.

“Ni kweli tumeyaona mabadiliko hayo na leo (Jumamosi) wanachama wa TLS wamekutana kujadili na sisi kama Council (Baraza) tunasubiri wanachama watupe maelekezo ya nini cha kufanya,” alisema rais wa TLS, Rugemeleza Nshala, alipozungumza na JAMHURI mwishoni mwa wiki iliyopita.

Wakizungumza bila kutaka kutajwa majina yao kwa sababu suala hilo bado linajadiliwa, baadhi ya wanasheria ambao ni wanachama wa TLS, wameliambia JAMHURI kuwa hawatakubaliana na mabadiliko yanayolenga kuidhoofisha TLS.

“Tunajua kuwa kwa muda mrefu serikali ina dhamira ya kuifanya TLS kuwa dhaifu ili itumike kirahisi, hilo hatutakubaliana nalo na kama lengo la mabadiliko haya ni hilo, basi serikali inajisumbua tu,” alisema mwanachama mmoja wa TLS.

Kuanzisha matawi

Moja kati ya mambo yanayopendekezwa ambayo kwa kiasi kikubwa yanabadili muundo wa TLS ni kuanzishwa kwa matawi mikoani na katika kanda.

Serikali inapendekeza kuongezwa kifungu cha 17A katika sheria ambayo inaelekeza kuanzishwa kwa matawi ya TLS katika mikoa itakayoteuliwa kama ambavyo Baraza litaona inafaa.

Aidha, kifungu kidogo kipya cha pili kinaeleza kuwa kutakuwa na matawi ya kanda yatakayoanzishwa na Baraza kwa ajili ya kusimamia utendaji kazi na utawala wa masuala ya matawi hayo.

Kifungu kidogo kipya cha tatu kinalipa Baraza nguvu ya kutunga kanuni zinatazotumika kuendesha matawi hayo.

Moja ya mambo ambayo yatayata matawi hayo nguvu ni kuwa yatatoa wajumbe wengi wa Mkutano Mkuu wa TLS ambao ndio hufanya uamuzi wa mambo makubwa ya chama hicho ikiwemo uchaguzi wa viongozi wake wa juu.

Kwa mujibu wa mapendekezo ya mabadiliko yanayoletwa na serikali, Sekretariati ya TLS itaundwa na Rais, Makamu wa Rais, Mhasibu na wajumbe wanane ambao watakuwa wamechaguliwa katika Mkutano Mkuu wa TLS.

Lakini, mabadiliko hayo yanataka kati ya wajumbe hao wanane watakaochaguliwa na Mkutano MKuu, saba wawe ni kutoka katika matawi na mmoja wao awe ni mwakilishi wa mawakili vijana.

Aidha, chini ya mapendekezo hayo, serikali inataka kuwepo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa TLS badala ya Katibu Mtendaji kama ilivyo sasa. Mkurugenzi huyo ndiye atakuwa mtendaji mkuu wa Sekretariati mwenye mamlaka ya kuajiri watumishi wa TLS, kutunza hesabu za chama na kuendesha shughuli za kila siku za TLS.

Madabadiliko hayo yanaelekeza kuwa Mtendaji Mkuu huyo anapaswa kuwa na sifa ya wakili wa Mahakama Kuu mwenye uzoefu usiopungua miaka kumi ambaye anaheshimika katika jamii.

Mtu atakayeajiriwa kama Mkurugenzi Mkuu wa TLS atashika nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano na anaweza kuajiriwa kwa kipindi cha pili cha miaka mitano iwapo ataonekana kuwa anafaa kuendelea kuishikilia nafasi hiyo.

Hata hivyo, kwa mujibu wa mapendekezo ya serikali, Mkurugenzi Mkuu wa TLS anaweza kuondolewa madarakani na Baraza kwa kupigiwa kura na theluthi mbili ya wanachama wa TLS ikibainika kuwa amepoteza uwezo wa kutekeleza majukumu yake, ukiukwaji mkubwa wa maadili, akifilisika, akikimbia ofisi au majukumu yake, akipatikana na hatia ya kosa la jinai na kuhukumiwa kifungo kisichopungua miaka miwili. 

Baraza la TLS

Aidha, muswada huo umefuta kifungu cha 16 cha sheria mama ambacho kinaainisha nguvu na majukumu ya Baraza la TLS na kutunga kifungu kipya kwa ajili hiyo.

Hata hivyo, wakati kifungu kilichopo kinalipa nguvu Baraza la TLS dhidi ya kanuni zozote zinazoweza kutungwa chini ya sheria hiyo, mabadiliko yanayopendekezwa yameondoa kabisa nguvu hiyo.

Chini ya kifungu kipya cha 16, Baraza la TLS linapewa jukumu jipya la kuanzisha matawi mikoani na kwenye kanda pamoja na majukumu mengine ya kawaida yatakayohakikisha kuwa Baraza litatumika kama chombo cha kutekeleza dira na dhima ya TLS.

Aidha, serikali inapendekeza mabadiliko ya Mkutano wa mwaka wa Baraza la TLS. Wakati chini ya sheria iliyopo Baraza la TLS inapaswa kufanya mikutano hiyo mara mbili kwa mwaka, mabadiliko yanayoletwa na serikali inataka kufutwa kwa kifungu 21 na kuleta kifungu kipya ambacho kinaelekeza kuwepo kwa mkutano wa mwaka wa Baraza mmoja tu wa mwaka utakaofanyika wiki ya pili ya Aprili kila mwaka.

Hata hivyo, kifungu hicho kipya kinaeleza kuwa Baraza linaweza kuitisha mkutano mwingine mkuu iwapo mazingira yataruhusu.

Mkutano mkuu wa mwaka

Chini ya kifungu hicho kipya kinachopendekezwa na serikali, ujumbe katika Mkutano Mkuu wa TLS utakuwa wa uwakilishi.

Kifungu hicho kinaanisha kuwa wajumbe wa mkutano mkuu watakuwa ni wajumbe wa Baraza, wajumbe wa kamati za kudumu za TLS, viongozi wote wa matawi wakihusisha wawakilishi wa mawakili vijana, wanawake, mawakili wa muda mrefu na walemavu, ambao huchaguliwa kila mwaka na matawi yao katika mikutano mikuu ya matawi hayo.

Wajumbe wengine wa Mkutano Mkuu wanatajwa kuwa ni wajumbe wa kamati za utendaji za kanda, wajumbe wawili kutoka katika kanda na mtu mwingine yeyote ambaye Baraza litaona anafaa kualikwa.

Serikali pia inapendekeza kufutwa kwa kifungu cha 22(1) ambacho kinatoa nguvu kwa wanachama 15 wa TLS kulitaka Baraza kuitisha mkutano mkuu.

Badala yake, chini ya mabadiliko yanayopendekezwa na serikali, ombi kama hilo linaweza kufanywa na theluthi moja ya wanachama wa TLS ambao nusu yao ni lazima wawe ni wawakilishi kutoka katika kila tawi.

Madhumuni na sababu

Serikali inasema mabadiliko yanayopendekezwa yanalenga kuboresha uwakilishi wa wajumbe wa Baraza Kuu la TLS ili kuweka usimamizi bora wa Baraza. 

Aidha, serikali inasema marekebisho mengine yameltwa ili kutambua Ofisi za kanda, kuondoa Mkutano Mkuu wa nusu mwaka kwa lengo la kupunguza gharama za uendeshaji wa Baraza. 

By Jamhuri